Bukobawadau

SOMA MAONI YA MDAU JUU YA SIASA ZA BUKOBA NA MH. KAGASHEKI

Kwa bahati mbaya Mh. Balozi Kagasheki MB, alipohutubia maelfu ya wakazi wa jimbo analoliongoza la Bukoba mjini, alijisahau kwamba siku hizi dunia ni kijiji na hivyo hotuba yake ingeliweza kusikiizwa na kufuatiliwa kutoka kila pembe ya dunia tena ndani ya muda mfupi sana. Inawezekana kabisa kwa kulisahau hilo alijiaminisha kuwa amesikilizwa na watu ambao kwa bahati mbaya sana na wakiwa ni wahanga wa mfumo wa uongozi wetu, hawana uwezo wa kuisikiliza na kuichambua hotuba yake na kumuelewa zaidi ya yale aliyokuwa akiyatamka.


Mheshimiwa hakujua kuwa, Tanzania ya leo siyo ile ya zamani, upashanaji habari ni mkuwa sana. Tumemsoma kwenye magazeti na hata kukusikiliza yote uliyoyaongea. Baada ya kuisikiliza video ya hotuba yake, nimegundua mambo kadhaa ambayo ninapenda kuwashirikisha wadau:
i.              Ameonyesha mfano mbaya kwa jamii, kuitisha mkutano wa hadhara kwa ajili ya kumshambulia na kumdhalilisha Meya wa Manispaa ya Bukoba. Kumwambia mtu hodari wa siasa kama Mh. Amani kwamba yeye ndiye umemchonga ni dharau kubwa sana. Wengi tunao uhakika kuwa kama ni siasa, Mh. Amani ni mwanasiasa wa siku nyingi ambaye amekwisha wahi kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa kagera, miaka ya mwisho ya 90 mpaka mwaka 2000. Anafahamu fika kwamba hawachezi katika ligi moja kwenye uwanja wa siasa. Hivyo inawezekana tu alimshawihi na pengine kumpa uwezeshaji wa kifedha lakini siyo kumchonga! Na alikiri kuwa alimuona kuwa anao uwezo wa kusukuma maendeleo.
ii.            Kumbe alitaka baada ya kuwa amemsaidia katika yote mpaka akawa meya, basi Mh. Amani awepo tu na asifanye lolote la kusukuma maendeleo, mbona sasa haeleweki huyu Mh. Kagasheki!
iii.           Miradi yote ambayo Mh. Amani ameipa msukumo hakuianzisha yeye na wala hajawahi kulidai hilo. Ni miradi iliyofanyiwa maamuzi na kuidhinishwa na mabaraza ya madiwani katika miaka ya nyuma wakati wa uongozi wa mzee Luhangisa, ambaye kwa kipindi chote cha uongozi wake tuliishuhudia Bukoba ikidumaa na kubaki kuwa kama pimbi katika kila eneo. Mh. Amani alichokifanya wakati wake ni uhodari na ujasiri wa kuweka mikakati na kuisimamia kuhakikisha mipango hiyo inatekelezwa. Hata Mh. Kagasheki amekiri kuwa mradi wa soko ni moja kati ya mipango aliyoahidi lakini je amefanya jitihada gani ili kufanya utekelezaji? Kuwa na mipango bila kuwa na mbinu za kuitekeleza haina maana yoyote.
iv.           Mh. Kagasheki, amedhihirisha kuwa yeye alitoa tu ahadi lakini hakuwa na uwezo wa kuzitekeleza. Hakujua ni nini la kufanya ili hiyo mipango iweze kutekelezeka. Kwa bahati mbaya mamlaka yenye uwezo wa kutekeleza miradi ni manispaa kupitia kwenye baraza la madiwani. Kwa kuwa Mh. Kagasheki hakuwa anahudhuria vikao vya baraza la madiwani ni dhahiri yeye aliisha jiweka kando na mipango ya Bukoba. Sasa ameonja uwaziri kamili, ndiyo anakumbuka kuwa oh, kumbe yeye ni mbunge! Na siyo siri miradi yote ikitekelezwa na hata isipotekelezwa aliyeikwamisha tumekwisha mjua. Kajitangaza hadharani ni Mh. Kagasheki.
v.            Kwa aliyoyasema mwenyewe wakati wa mkutano wake ni dhahiri kuwa Mh. Kagasheki, hapingi utekelezaji wa miradi hasa ule wa soko bali anahofia utekelezwaji wa mradi huo utampatia sifa lukuki Mh. Amani, kwani ni juhudi zake zilizowezesha kupatikana kwa taasisi ya kutoa mkopo kwa ajili ya huo mradi. Ukweli ambao Mh. Kagasheki aliukwepa kuuweka wazi japo anaufahamu kama msomi na mtu ambaye kwa bahati nzuri ameishi kwa sehemu kubwa ya maisha yake katika nchi zilizoendelea, ni kwamba miradi yote ambayo Mh. Amani, Baraza la madiwani na uongozi wa manispaa wameipa kipaumbele, ni miradi yenye uwezo wa kujiendesha. Soko ni mradi wenye vyanzo imara vya kuzalisha fedha kwa ajili ya manispaa, alikadhalika mradi wa stendi na ule wa viwanja elfu tano, yote ni miradi ambayo inao uwezo wa kutengeneza fedha na ikajilipa. Ndiyo maana wameweza kuiuza miradi hiyo na ikaonyesha kuwavutia taasisi za kutoa mikopo na wawekezaji. Na hilo ndilo ambalo Mh. Kagasheki hakutaka kuueleza umma kwa nia na lengo la kupotosha ukweli.
vi.           CHADEMA katika mkutano wao kesho yake, kama ilivyoandikwa kwenye gazeti la Tanzania Daima la leo (27 Novemba 2012) kwamba Mh. Kagasheki anachochea vurugu na hilo liko wazi. Mkutano wake wa juzi ilikuwa ni kuwachochea wanachi wamchukie Meya wao ili wamuone kama mtu asiyefaa. Inasikitisha kwa mbunge kufundwa na viongozi wa CHADEMA wa ngazi ya wilaya. Na bado wakaonyesha kuwa wao hawapingi mradi wa soko bali walisimamia kuhakikisha wafanyabiashara wajulikane wanahamishiwa wapi. Katika gazeti la Tanzania Daima la jana (26 Novemba 2012) ililipotiwa kwamba katika kikao cha Baraza la madiwani ambacho Mh. Kagasheki alihudhuria, taarifa iliyotolewa ni kwamba mipango ya kuwahamisha wafanyabiashara kwenye eneo la soko la muda inaendelea vizuri. Yeye mwenyewe katika hotuba yake hili kalisema. Pi suala la utafiti wa udongo na meza ya maji pia alikiri kuwa kikao kilitaarifiwa kuwa limo mbioni kufanyika. Je, kama siyo kuwa Mh. Kagasheki anapinga mradi kwa sababu zake na uroho wa madaraka ni nini? 
vii.          Madai yake ya kutoshirikishwa katika maamuzi ya Manispaa hayana msingi na ni uongo mtupu, kwani yeye ni Diwani kwa mujibu wa sheria kwa hiyo anapaswa ki-kanuni kuhudhuria vikao vyote vya Baraza la ma-diwani. yeye amekuwa Naibu waziri na baadaye Waziri kamili, gazeti moja liliandika kuwa kikao cha wiki iliyopita ndicho kilikuwa cha kwanza kuhudhuria tangu baada ya uchaguzi mkuu wa 2010. Je, kama alitelekeza wajibu wake wa kuhudhuria vikao, ni sahihi kwamba Baraza la madiwani lisikutane kumsubiri yeye? Je, imo katika kanuni za uendeshaji wa mabaraza ya madiwani? Haya ni mapungufu makubwa sana aliyoyaonyesha!
viii.        Mh. Kagasheki, amedhihirisha kulewa u-waziri na wala siyo ubunge! Amejipa nguvu ya kuwa na kura ya turufu (VETO) juu ya baraza la madiwani. Huu ni udhalilishaji wa demokrasia. Alihutubia ule mkutano kama kwamba yeye ndiye peke yake anayepaswa kuamua juu ya jambo lolote linalohusu Bukoba. Hii ni dharau kubwa sana! Japo, hili halishangazi maana haya yanatokea katika majimbo mengi na ndilo chimbuko la migogoro kati ya wabunge na ma meya na wenyeviti wa ma baraza ya madiwani. Wabunge wamekuwa wakijikuta kwamba siyo watekelezaji wakuu wa shughuli za Kanseli zao ambako ki-utaratibu maMeya na wenyeviti ndiyo wenye mamlaka za usimamizi chini ya kanseli zao. Na hivyo baadhi ya wabunge wenye kutaka kuhodhi nafasi hizo kama inavyojidhihirisha kwa Mh. Kagasheki wamekuwa wakileta mitafaruku isiyo na sababu.
ix.           Mh. Kagasheki, alitoa orodha ya miradi aliyoichangia kabla hajawa mbunge. Ninayoikumbuka ni pamoja na shule kule kata ya Nshambya, kuweka taa za barabarani na kuweka kifusi na zege eneo la wauza ndizi kwenye soko kuu. Ninampongeza sana kwa kuyafanya hayo yote wakati huo akiwa anatafuta ubunge na kweli yalimsaidia akaupata. Lakini kwa watu tunaotaka kuwa na maendeleo makubwa na na endelevu, hatutakiwi kuona kwa kutumia taa ya baiskeli! Hivi vitu vyote alivyovifanya Mh. Kagasheki, vilikuwa na mtizamo mdogo, finyu na malengo binafsi zaidi kulio ya umma. Hakuna unaloweza kuliweka katika mzani pamoja na miradi mikubwa inayosukumwa na Mh. Amani, Kanseli na uongozi wa manispaa! Mh. Kagasheki analeta mzaha wa wazi katika hili. Je, tangu awe mbunge, ni lipi la ubunifu na lenye mtizamo mpana na wa muda mrefu ambalo amelifanya katika jimbo? Kusaidia wafiwa na wagonjwa, na kutoa michango kwenye vikundi vya akina mama ni mambo ya kupita tu (hand outs). Tuonyeshe mradi wa shilingi bilioni mbili tu! Kagasheki ameshindwa kuelezea manufaa ya kuwa na miradi mikubwa kama hiyo inayoingiza pesa nyingi katika eneo dogo kama la Bukoba na mguso (effects) wake katika hali nzima ya jamii na unchumi wa eneo, hususan kuleta ajira na kuongeza mzunguko wa pesa hivyo kupunguza umaskini wa kipato. Amelifanya hilo makusudi lakini anachowakosesha watu wa Bukoba ndicho ambacho hawakijui, kwamba kutekelezwa kwa miradi mingi katika eno fulani ndiyo neema. Bukoba imekuwa nyuma sana kwa kuvutia miradi mikubwa na hivyo kuyakosa hayo manufaa, ndiyo maana umasikini unazidi kuongezeka siku hadi siku. Kagasheki, kama kiongozi angelitegemewa awe mtu wa mwishio kufanya jambo lolote linaloweza kuichelewesha au kuikwamisha hiyo miradi.
x.            Kagasheki ni mtu mwenye husuda, anayafanya hayo kwa kuhofia kuwa miradi hasa wa soko kwa sababu una mguso kwa idadi kubwa ya wapiga kura japo siyo wengi na hata wangelikuwa wengi maendeleo yamekuwa na tabia ya kuleta maumivu kabla ya kuleta faraja. Kagasheki analifahamu vyema hilo. Anapozungumzia mradi wa kiwanja cha ndege japo anajipatia sifa zisizo za kwake kwani huo mradi ulikuwemo kwenye mipango ya serikali kabla hata hajawa mbunge. Lakini pamoja  na hayo, aliusemea bungeni baada ya kuwa mbunge hadi kuufanikisha, na hiyo ndiyo sifa anayoistahili pamoja na kwamba haikuwa na ubunifu binafsi. Anakumbuka vyema suala la kufidia nyumba zilizobomolewa kwa ajili ya kuutekeleza mradi huo.
xi.           Mradi wa soko una mazingira tofauti, hakuna suala la kulipa fidia bali ni utaratibu wa kuwahamisha wapangaji halali kwa muda wa utekelezaji wa mradi. Hili Kanseli imelizingatia na muda wa mradi ulitajwa kwenye kikao, kwa mujibu wa hotuba yake, bali yeye hataki uwe huo. Anafurahia kuwa kuna shauri liko mahakamani, kiasi inatia shaka kama hayuko nyuma ya wale waliopeleka shauri mahakamani. Kagasheki anadai mradi ukienda vibaya wote katika nafasi za uongozi watakuwa matatani! Kiongozi unashindwa kutekeleza jambo la maana kwa kutanguliza hofu ya kushindwa! Hivi Kagasheki anashindwa kutambua madhara ya kuchelewesha miradi mikubwa kama hii! Miradi mikubwa kama hiyo kadiri unavyouchelewesha ndivyo unayosababisha gharama za mradi kuongezeka. Kwa hiyo kwa anayoyafanya Kagasheki, yatatokea mawili, ama kuufanya mradi kwa gharama kubwa zaidi au kutokuufanya kabisa huo mradi.    
xii.          Kwa yote mawili hapo juu, yanamfanya Kagasheki aonekane ni mbinafsi na mroho wa madaraka kuliko anavyowasingizia wengine. Yupo tayari mradi usifanyke, ili apate kura za ubabaishaji kwa watu wasioelewa ni kwa kiasi gani maamuzi yake yamewaathiri kwa kuwanyima fursa ambazo huo mradi ungelizifungua kama nilivyozigusia hapo juu. Kwa hiyo Kagasheki, anasumbuliwa kufanya siasa za ghiliba ili awahadae wananchi kwa kutokujua kwao ili wamuone ndiye wa maana alafu baadaye wamchague tena kuwa mbunge wa Bukoba mjini. Ninawatahadhalisheni, huyu nia yake na kundi lake la ndugu zake linalomsumbua Mh. Amani wameingiwa na kasumba ya kwamba wao ndiyo familia bora hapo Bukoba kwa hiyo wanataka waendelee kuwa wao ndiyo watawala. Huu usultani wana Bukoba tuukatae. Mtu wa kuwa kiongozi apimwe kwa uwezo wake wa kuongoza kwa manufaa ya kuleta maendeleo kwa walio wengi na siyo kuwatumia watu wenye mtizamo mdogo kutokana na kukandamizwa kwao ki-elimu ili kuwatawala kwa maslahi binafsi. Kwa yale ambayo Mh. Amani ameonyesha kuyasimamia katika kipindi kifupi, katika kusukuma maendeleo ya Bukoba, anastahili kuungwa mkono na siyo kubezwa, kutukanwa na kudhalilishwa kama alivyofanya Mh. Kagasheki, ambaye amedhihirisha kukiogopa kitabu kipya. Bahati mbaya wale ambao Mh. Amani anawatengenezea mustakabali mzuri wa baadaye ili waweze kuishi na kufanya kazi katika mazingira mazuri ndiyo hao wasiolifahamu hilo.
xiii.        Wala sitaki nieleweke kwamba ninasema moja kwa moja kuwa Mh. Amani ndiye moja kwa moja tumfikirie kuwa mbunge wa Bukoba hapo mwaka 2015 ila ninasisitiza kuwa tuwe na uwezo wa kuupima uongozi wa kwa kazi zilizofanyika na siyo tu kuendelea kumpa mtu uongozi kwa mazoea. Kagasheki amekuwa mbunge sasa miaka saba inakwisha ni lipi analoweza kuliweka mezani tukamuona anafaa kuendelea kuwa mbunge wetu? Wale wote ambao tumechukizwa na kitendo cha Kagasheki kujionyesha kuwa na uchu wa madaraka kuliko kuleta maendeleo tusimame kidete kuuelimisha umma wa wale wasiotambua, wamjue ili waanze kumkataa na uchaguzi ujao tupate mbunge mwingine. Ni kosa kubwa kuongozwa na mtu mmoja kwa zaidi ya vipindi viwili, anabadilika na kujihisi yeye ndiye sultani wenu, ndilo chimbuko la kuzorota kwa maendeleo.

Ninayo mengi ya kuandika ila ninaishia hapa.

Nico Mutta
Kimara Temboni
Dar es Salaa, Tanzania
nikodamutta@gmail.com
Next Post Previous Post
Bukobawadau