Bukobawadau

TATIZO LA ELIMU TANZANIA NA MFANO WA KIONGOZI WA WASIOVAA VIATU


Ni wakati mwingine wa kulalama na kupiga kelele za msimu. Kelele ambazo kwa historia ya Watanzania tumejifunza kuwa sawa na upepo uvumao usio na madhara wala usiochukuliwa tahadhari kwa madhari ya mbeleni.  Naamu! NECTA imetuletea kipande kingine cha filamu ya Elimu Tanzania. Ni kipande kitamu cha filamu ya kuogofya na inayoacha madhara kwa vizazi na vizazi. Mfululizo wa filamu ya hii umetengenezwa katika mtindo ambao kipande cha leo ni kikali zaidi kuliko kile cha jana. Huwezi kupata uondo wa filamu hii kama hukuangalia au umesahau vipande vilivyopita. Na kama umesahau wala usijisikie vibaya kwani hiyo ni moja ya jadi zetu. 

Basi ili twende sawa, nitakukumbusha vipande vichache vya filamu hii vilivyochezwa na kutoka miaka ya hivi karibuni. Ni vile tu ninavyokumbuka kwani nami ni Mtanzania origino! Filamu yetu itaanzia kwa watoto 5,000 waliofaulu kujiunga kidato cha Kwanza wakiwa hawajuhi kusoma wala kuandika. Hiki ni kipande (episode) cha awali na cha kusisimua. Mmoja wa wachezaji wa hiki kipande alinifurahisha pale alipoamua kuandika “mistari” kwenye mtihani. Kilipotoka, Watanzania wa kike kwa wa kiume, wafanyakazi kwa wakulima na wanasiasa kwa wanaharakati walisisimuka kweli kweli. Mwisho wa siku msisimko ukaisha na filamu ikapoteza mvuto bila kuacha hata funzo na wala kuchukua hatua.
Kitambo kidogo kikaletwa kipande kingine. Zamu hii Walimu wakiongozwa na Chama Chao (UWT) wakadai mazingira bora ya kazi, vitendea kazi na stahili zao ikiwemo malimbikizo mbalimbali. Kwenye hiki kipande nikiri kwamba nami sikumbuki chote. Ila siwezi kusahau pale dakika ya 85/90 Walimu waliposema “Si hamkutusikiliza? Kitaeleweka tu!” Kwa upole wa nyoka Walimu wakarudi kazini kwa amri ya mahakama na serikali pamoja na Wazazi tukasahau kuwa amri ya mahakama haiendi kuwasimamia au kukagua kujua nini hawa walimu wanafanya madalasani. Baada ya kutulia kwa takribani miezi nane, watazamaji walikwisha sahau kabisa habari ya kipande (episode) cha mgomo wa Walimu.
Katikati ya mapumziko ya filamu pendwa, ikawekwa jingle ya kukosekana kwa mitaala ya Elimu Tanzania. Miemko na tambo kubwa kubwa zikapigwa ili kuufanya ukweli uchanganyikiwe! Mwisho wa jingle, ukweli ukawa mtanzikoni (in dilemma), wasikilizaji wakabaki wamechanganyikiwa na kuduwaha kama ilivyo ada.
Wiki hii NECTA imeamua kutuletea kitu kipyaaa kabisa toka kwenye makalatasi. Kama kawa mzigo umewashika vilivilvyo Wa-Tz. Wakilala, wakiamuka wanalo—matokeo mabaya ya Kidato cha nne! Wanafunzi wamefanya yao. Wenye fani wamechora ma-ZOMBIE, wenye vipaji wametunga hadithi/filamu, Chokoraa wameandika matusi, Masharobaro/Wasafi wamekusanya pepa Nyeupeeee, na wachache walioweza wamejaribu kujitetea! Kwenye kipande cha kwanza tulipata wahitimu 5000 wasiojua kusoma na kuandika. Zamu hii tumezalisha wahitimu 270,289 walioshindwa mtihani sawa na asilimia 60%! Na ni hisia zangu kwamba yamkini hii nayo ni seti inayohusisha wasiojua kusoma na kuandika walau Kiswahili kwa ufasaha.


Hiki kipande cha matokeo cha wiki hii kimeanza kugawanyika katika vipande vingine vidogo vidogo vingi. Mimi nakipenda na nimekikalili kile ambacho Mkurugenzi wa NECTA anaelezea waliofanya Wanafunzi ndani ya chumba cha mtihani. Wacha nimnukuu  “Mwaka jana tulikutana na ‘single’ yaani waliandika mashairi kwa uchache, lakini mwaka huu tumepata albamu nzima… ni vituko vitupu, wengine wanaandika mapenzi, mwanafunzi anatumia ukurasa mzima kumlalamikia mpenzi wake. Miongoni mwa yaliyoandikwa ni mpenzi, umeniacha, natamani kunywa sumu, usiku silali nakuwaza wewe…” alisema Dk Ndalichako. Agha gha gha gha gha gha! Subiri tu-forward kidogo. sikiliza na hapa “Unakuta mwanafunzi anaeleza anavyolishangaa Bunge… mtu anaandika… nawashangaa wabunge, wamekaa kama wapo kijiweni, wabunge wamekosa ustaarabu, badala kujadili kero za wananchi waliowachagua, wanapokea timu zilizoshinda makombe… timu ikishinda Kombe la Kagame inapokelewa bungeni. Bunge limekuwa kama kijiwe, bungeni siyo ukumbi wa starehe kama mnataka kupokea timu hizo nendeni katika ofisi zao au viwanjani…” Mama Ndalichako mcheshi sana.
Mpendwa msomaji masimulizi yote hapo juu ni matokeo ya matatizo. Vyanzo vya matatizo haya ni vingi na kila mmoja, awe mzazi, Mwalimu au mwanafunzi ameshiriki kufanikisha na kukuza matatizo. Kwa kuwa hii ni makala ya porojo za kahawa ya jioni, basi nitaandika bila rejea na kwa kutumia mtazamo binafsi.

Moja ya sababu kubwa ya matatizo ya sekta ya Elimu ni kuwa na viongozi waliojikinga na kujitenga mbali na mahali yanakoibuka matatizo yanayoathiri jamii wanayoiongoza. Tuna viongozi waliovaa viatu, wanaotuongoza kutafuta suluhu ya tatizo la barabara kwa kutupitisha kwenye njia iliyojaa miiba. Hawachomwi na miiba hivyo hawana hisia za uchungu tuupatao, hawaoni simanzi kwenye nyuso zetu maana wametupa visogo vyao, na hata wakisikia tunaguna wao wanadhani tunaifurahia safari. Ni sababu hii hii unayosababisha viongozi wapalilie matatizo yaliyopo katika sekta ya afya. Hatuwezi kuwa na viongozi ambao watoto wao wanasoma shule zenye walimu wazuri, vifaa na mahabara zilizokamilika  tukategemea  wajue matatizo ya shule zetu za umma na wawe na uchungu wa kuziboresha. Sana sana tunawajengea mazingira ya wao kujifunza usanii wa kuonyesha nyuso zenye huzuni lakini rohoni na kichwani kumetulia, midomo yenye kupiga kelele na kulaani wakati kifuani kuko tuli. Najua kuna matatizo mengine ya kimfumo, kitaalamu na kimuundo katika sekta ya Elimu. Lakini haya yote ili yafanyiwe kazi kwa ufasaha tunahitaji wanaofanya maamuzi juu ya Elimu yetu na Watendaji katika sekta husika wapate msukumo wa ndani. Na huu msukumo hauji kama tunaendelea kuwaacha watuongoze kupita njia yenye miiba wakiwa mbele na wamevaa viatu. Lazima tuwavue viatu na wakae nyuma ya visogo vyetu kwanza ili nao wajue kwamba ukali wa tindikali hauonjwi kwa hisia. Wakubali ama sote tuvae viatu  au watembee peku nasi tuwafuate tukiwa tumevaa viatu.

Kwa ufupi kutafuta suluhu ya matatizo ya Elimu yetu tunahitaji kuwa na suluhisho la haraka, la muda wa kati na muda mrefu. Lazima tufikie mahali frameworks za sekta muhimu kama Elimu ziwe kama misahafu. Nisingependa kuendelea na porojo. Naomba kalamu yangu leo iishie hapa.

Imeandikwa na:
Ericus Kimasha
+255-713-177372
Next Post Previous Post
Bukobawadau