Bukobawadau

SEHEMU YA 2: UONGOZI WA KCU (1990)LTD UNANIOFIA KWA SABABU YA MADHAMBI YAKE

Na Prudence Karugendo
HII ni sehemu ya pili na ya mwisho ya mahojiano kati ya mwakilishi wa chama cha msingi cha Kamachumu, Muleba, Kagera, Archard Felician Muhandiki, na mwandishi wa makala hii kuhusu mwenendo wa chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. cha mkoani Kagera.
Karugendo: Unaonaje juhudi zako za kuupigania ushirika namna zinavyochukuliwa na serikali?
 

Muhandiki: Siridhiki na serikali inavyozichukulia juhudi zangu hizo, ila sikati tamaa.
 

Karugendo: Kwa nini huridhiki na jinsi serikali inavyozichukulia juhudi zako za kuhakikisha ushirika unasalimika, na kama ni hivyo ni kitu gani kinakufanya usikate tamaa?
Muhandiki: Nimefukuzwa mara mbili kwenye mkutano mkuu wa chama kikuu, KCU (1990) Ltd., ambacho mimi ni mwakilishi halali wa chama changu cha msingi, na pia nikafukuzwa kwa waziri, Mhandisi Christopher Chiza, ambaye kwa hapa ndiye serikali.
Karugendo: Sasa waziri anaingiaje kwenye suala lako la kufukuzwa kwenye mkutano mkuu wa chama chako kikuu cha ushirika?
 

Muhandiki: Nilipeleka malalamiko yangu kwake kimaandishi, kutokana na yeye kuwa Waziri wa Ushirika, lakini ajabu waziri akairudisha barua yangu hiyo ya malalamiko kwenye chama changu kikuu cha ushirika akikishauri kinishughulikie!
Yaani badala ya yeye kuyashughulikia malalamiko yangu akayapeleka kwa ninaowashitaki akiwataka wao ndio wanihukumu! Hiyo ni sawa na mtu anayeshitaki kwamba fulani kamwibia halafu mahakama ikatoa ushauri kuwa anayeshitakiwa ndiye aandike hukumu!
Karugendo: Je, umeishaona dalili zozote zinazoonyesha kuwa chama chako kikuu, KCU (1990) Ltd., kinayafanyia kazi maelekezo kiliyopewa na waziri ya kwamba kikushughulikie, yakiambatana na barua yako ya malalamiko uliyoipeleka kwake?
Muhandiki: Ndiyo, dalili ni nyingi tena zilizo wazi. Dalili hizo ni pamoja kuzuiwa kuingia kwenye mkutano mkuu wa dharura wa KCU (1990) Ltd., ambapo yalitumika mabavu na vitisho vya kila aina vilivyosimamiwa na wahuni, kwa vile kihalali hakuna mwenye haki ya kunizuia kuingia kwenye mkutano huo unaonihusu, nikiwa mwakilishi, tena niliyejigharamia kutoka Dar es salaam hadi Bukoba, kwa ajili ya kuwawakilisha wanaushirika wa chama changu cha msingi.
Karugendo: Inasemekana Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, ni mmoja wa wasaidizi wa rais wenye usaidizi duni sana, unayahusishaje madai hayo na malalamiko yako?
Muhandiki: Nayakubali kabisa madai hayo, waziri huyo ni dhaifu sana na mzigo mkubwa kwa rais katika usaidizi wa kuwahudumia wananchi. Ila nashangaa kuona kwamba anayoshitakiwa nayo Chiza, suala la KCU (1990) Ltd. halimo, wakati yeye ndiye kachangia kwa kiasi kikubwa kukidhoofisha chama hicho.
Karugendo: Kuna fununu kwamba wenyeviti wa vyama vya msingi, ama wameandamana au wanapanga kuandamana, kwenda makao makuu ya KCU (1990) Ltd. kudai pesa ya wakulima iliyocheleweshwa sana na chama hicho kikuu cha ushirika, unazichukuliaje fununu hizo?
Muhandiki:Nazifurahia sana fununu hizo.
Karugendo: Kwa nini unazifurahia?
Muhandiki: Naona kwamba walau wakulima chini ya viongozi wao wa vyama vya msingi wameamka, wamefumbua macho na kuliona baya na jema. Sababu wamekuwa wakidanganywa sana na viongozi wa chama kikuu na wao kukaa kimya.
Karugendo: Kwa nini unadhani kwamba wakulima wamekuwa hawazitilii maanani hila zinazofanywa na chama chao kikuu cha ushirika dhidi yao?
 

Muhandiki: Ni kwa sababu walio wengi hayaelewi vya kutosha masuala ya ushirika. Chama cha ushirika ambacho kina jukumu la kuwaelimisha na kuwaelewesha wakulima juu ya ushirika na hivyo kuwapa nguvu ya kuuendeleza kinafurahia kutokuelewa kwao! Kinatumia ile dhana ya kwamba ukila na kipofu usimshike mkono!
Ni kwamba chama hicho kinaitumia hali hiyo ya ukosefu wa weledi katika ushirika walio nao wakulima, ili kujinufaisha chenyewe badala ya kuwanufaisha wakulima.
Karugendo: Ni kitu gani kinakupa hisia hizo?
Muhandiki: Ni kwamba chama kikuu cha ushirika ndicho kinachomuamlia mkulima mahali pa kuwekeza ambapo ukiangalia utaona mkulima hana faida yoyote anayoipata. Na mkulima anajikuta hana nguvu za kukubali wala kuukataa uwekezaji huo wa kitapeli.
Karugendo: Unataka kusema kwamba hakuna utaratibu unaomhusisha kila mwanaushirika kwenye maamuzi ya chama chake kikuu?

 

Muhandiki: Utaratibu upo, ila unavurugwa makusudi ili uonekane kama haupo. Wanaochaguliwa na wanaushirika kwenye vyama vya msingi wakawe wawakilishi wa vyama hivyo wanatengenezewa mazingira yaliyo na ushawishi wa kuwasahaulisha uwakilishi wao, na badala yake wanayaelekeza mawazo yao kwa wale wanaopaswa kuwawajibisha kwa niaba ya wanaushirika waliobaki. Badala ya kuwawajibisha wawakilishi wanajifanya ni sehemu ya wanaotakiwa kuwajibika! Mpaka hapo uwakilishi unakuwa hauna maana yoyote.
Ndiyo maana wawakilishi tunaojitahidi kuifanya ipasavyo kazi ya uwakilishi tunaonekana maadui na kutolewa nje ya mikutano ya chama kikuu na wakati mwingine kuzuiwa kabisa tusiingie kwenye mikutano hiyo. Hayo yanafanywa na uongozi wa chama kikuu.
Karugendo: Mbali na uongozi wa kuchaguliwa KCU (1990) Ltd. inao uongozi wa kuajiriwa, vipi uongozi huo wa kuajiriwa unawajibika ipasavyo, kwa mtazamo wako?
Muhandiki: Hapana. Kusema ukweli uongozi wa kuajiriwa ndio unaoupotosha uongozi wa kuchaguliwa na kuufanya ujiingize kwenye vitendo vya ufisadi. Sababu uongozi wa kuajiriwa unadiriki hata kutoa rushwa kwa uongozi wa kuchaguliwa ili ukawanyonge wakulima. Ni kwa vile uongozi huo wa kuajiriwa unatumia uelewa mdogo katika masuala ya ushirika, ulio nao uongozi wa kuchaguliwa, ili kuwaibia wakulima bila wao kujua wala uongozi wao wa kuchaguliwa kujua, wakati mwingine.
Karugendo: Uonavyo wewe ni upande upi unaoupotosha mwingine kati ya uongozi wa kuajiriwa na wa kuchaguliwa?
Muhandiki: Kwa maelezo niliyokwishayatoa inajionyesha wazi kwamba ni uongozi wa kuajiriwa ndio unaoupotosha ungozi wa kuchaguliwa.
Karugendo: Katika hali hii ya kudorora kwa ushirika, tena kudorora kunakosababishwa na uzembe katika uongozi, unadhani ni kitu gani kikifanyika kinaweza kuufanya ushirika urudie uimara wake kama ulivyokuwa miaka ya nyuma?
 

Muhandiki: Ni ukweli na uwazi. Bila ukweli na uwazi hakuna ushirika. Nasema hivyo kwa vile sheria na kanuni za ushirika havifuatwi hata kidogo katika KCU (1990) Ltd.. Ni kwamba uongozi wa ushirika huo umebaki kuendesha mambo kwa kutegemea mazoea tu!
Mazoea ya kwamba wanaushirika walio wengi wana uelewa mdogo juu ya sheria na kanuni za ushirika, hivyo ni vigumu kwao kuhoji mambo ya msingi yanayohusu ushirika wao. Serikali nayo inaonekana kuwatupa mkono wakulima, haionyeshi jitihada za kutosha za kuulinda ushirika, hasa kwa kutumia sheria na kanuni vilivyowekwa wazi kwa ajili ya kuuhami ushirika.
 

Karugendo: Mwisho, kwa nini wanaushirika wanautukuza uongozi pamoja na waajiriwa wa ushirika ilhali wao wakiwa ndio wenye mali? Unadhani nini kifanyike kuibadili hali hiyo na kuurudisha ushirika kwa wenye mali?
 

Muhandiki: Ni kwa sababu ya uelewa mdogo walio nao wanaushirika juu ya ushirika wao. Hawapewi elimu ya kutosha juu ya kitu hicho. Kwa maana hiyo hawana imani kuwa ushirika ni mali yao, ndiyo maana wanakosa amani wakidhani viongozi na waajiriwa wa ushirika ni mabosi wao! Papo hapo wanawaona kama waokozi wao wakiwachukulia kama miungu watu!
Hivyo wanaushirika inabidi waelimishwe juu ya kitu hicho. Kwa mfano, waelewe kwamba meneja mkuu wa chama chao kikuu cha ushirika ni mtu wanayemwajiri wao, mwenyekiti wa chama chao kikuu anasimamia tu ushirika akiwa ametokana na wao, sio kwamba kuchaguliwa kwake kuwa mwenyekiti tayari anapata umiliki wa chama chao kikuu na kukifanya ni mali yake.
Pia wanaushirika waelewe kwamba kuporomoka kwa bei ya zao lao kuu katika soko, kwa maana ya kahawa, hakupaswi kuwaathiri wao tu, ni lazima kuguse pia mishahara na malupulupu ya viongozi na waajiriwa wa chama chao. Baada ya kuelimishwa na kuelimika, wakayaelewa hayo, ni lazima ushirika utakuwa umerudi kwa wenye mali. Hivyo viongozi na waajiriwa wa ushirika ni lazima wataanza kuwaheshimu wanaushirika, na ushirika ni lazima utashamiri. Hilo ndilo ninalolipigania.
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau