SEARCH -TAFUTA

.

SIR.LOOM INC

13 December 2013

ZITTO, LEMA ,WEREMA WATIFUANA;Wabishania ukweli, ujasiri kuhusu mabilioni Uswisi

SAKATA la mabilioni yanayodaiwa kufichwa na Watanzania nje ya nchi jana lilileta zogo bungeni baada ya Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema, kutifuana na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, huku Mbunge wa Arusha Godbless akiwataka wote wawili wampe majina ayataje hadharani kama wanashikwa na woga.
Huku Zitto akisisitiza kuwa serikali haionyeshi nia ya kuwachukulia hatua walioficha pesa hizo nje ya nchi, Jaji Werema aliliambia Bunge kuwa Zitto mwenyewe ameshakiri chini ya kiapo ofisini kwake kwamba hana majina wala akaunti za watu hao, kinyume cha kauli yake huko nyuma alipowahi kusema kuwa anawajua.
Kwa mujibu wa Jaji Werema, kwa kuwa sakata hili liliibuliwa bungeni na Zitto, serikali iliunda kamati malumu ikitarajia kuwa mbunge huyo ndiye angetoa ushirikiano kurahisisha uchunguzi huo, lakini mara zote amekuwa akiikwepa kamati.
Alisema Zitto anapotosha Bunge na taifa kuhusu sakata hilo. Kauli ya Werema ilitolewa jioni wakati Bunge limekaa kama kamati, akijibu hoja ya Zitto aliyoitoa asubuhi akiishutumu serikali kwa kutokuwa na nia thabiti ya kufuatilia pesa hizo ili zirejeshwe.
Lakini kabla ya Mwanasheria Mkuu kujibu, Lema alikuwa amewataka serikali na Zitto kuacha kuchezea akili za Watanzania; kwamba wawe na ujasiri wa kutaja wahusika badala ya kupiga danadana.
Lema alisema kuwa kama wao wanaogopa kutaja wahusika, basi apewe yeye majina awataje hadharani, kwa maana hahitaji kinga ya Bunge kutaja wezi wa mali ya umma.
Jaji Werema alisisitiza kuwa Zitto ameshakiri chini ya kiapo ofisini kwa Mwanasheria Mkuu, kuwa hana majina wala akaunti yoyote iliyoko Uswisi.
Katika kusisitiza hoja yake, Jaji Werema alitoa mlolongo wa vikao ambavyo kamati iliyoundwa na serikali kuchunguza sakata hilo ulivyokuwa ukifanya, lakini Zitto alikuwa akiipiga chenga kabla ya kukiri kuwa hana majina wala akaunti.
“Kauli alizozitoa Mheshimiwa Mbunge Zitto Kabwe, kwamba serikali haina nia ya kurejesha fedha zilizofichwa nje, haziendani na tabia yake, haziendani na mwenendo wake na haziendani na kauli zake mbele ya kamati kwa sababu tumemuita mara kadhaa mbele ya kamati lakini hatokei.
Alisema kamati ilipoundwa, ilikuwa na majukumu ya kuchunguza kama fedha hizo ni haramu, kutambua benki zilikofichwa fedha hizo, kutambua waliozificha, kuandaa mashtaka na kisha kuishauri serikali.
“Februari 28, mwaka huu, kamati ilikutana hapa bungeni katika ofisi yangu na ilipomuita Mheshimiwa Zitto aje atoe ushahidi, alikuja akatwambia anazo nyaraka na taarifa ila akaomba ahakikishiwe usalama ili pale ambapo angezileta pasingelikuwa na mtu wa kumzonga.
“Pia, alitaka mimi nitoe kiapo ambacho baada ya kutaja hayo majina halafu ikawa siyo kweli, basi yeye awe ‘free’ (huru), kwa hiyo alitaka apewe kinga ya kiapo.
“Machi 23 tulipomuita aje akatukwepa, akasema anakwenda Tanga kwenye mafunzo ya mgambo, kwa hiyo, tukaona tumsubiri hadi atakapomaliza.
“Aprili 12, mwaka huu, tukakutana naye hapa Dodoma katika viwanja vya Bunge, akasema hawezi kutwambia chochote kwa sababu alikuwa akijiandaa kwenda Afrika Kusini.
“Mei 4 tulimuita tena kwenye kamati hapa Dodoma na katikati ya mahojiano alidai ana jambo muhumu lenye maslahi kwa taifa, akasema anaomba aondoke atarudi, kamati ilimruhusu, hata hivyo hakurudi tena.
“Tulipompigia simu alisema alikuwa Dar es Salaam na alikuwa ‘busy’ akijiandaa kwa kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere.
“Mei 24 kamati ilimfuata Dar es Salaam, akasema hana nafasi kwa sababu wakati huo alikuwa akijiandaa kuisaidia Timu ya Taifa,” alisema Jaji Werema na kuongeza:
“Kamati iliamua sheria ichukue mkondo wake kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Kifungu cha sita ndipo tukachukua maelezo ya Zitto Kabwe chini ya kiapo na akatwambia hakuwa na jina, wala akaunti ya Mtanzania yeyote aliyeficha fedha nje.
“Lakini, leo hapa amesema serikali haina nia ya kurudisha fedha zilizofichwa Uswisi. Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Naibu Spika, Zitto Kabwe ni mzito na nakubaliana na Lema (Mbunge wa Arusha Mjini) aliyesema hapa, kwamba Zitto alete majina hayo.
“Katika hili, nawashukuru wabunge 87 waliofika mbele ya kamati, nawashukuru wananchi wengine waliofika kwani sasa tumefika pazuri ila serikali inaomba iongezewe miezi sita ili ikamilishe jambo hili lakini hili suala la Zitto tutashughulika nalo kisheria kwa sababu huwezi kulidanganya Bunge halafu ukaachwa,” alisema Jaji Werema.
Kwa mujibu wa Werema, baada ya kamati kuona Zitto haipi ushirikiano, iliamua kumuandikia barua rasmi kwa wito maalumu ofisini kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Werema alisema kuwa Zitto aliitikia wito huo, na akazungumza na kamati chini ya kiapo, kwamba hana majina wala akaunti za Watanzania zilizo Uswisi.
Kutokana na hali hiyo, Werema alisema hakuelewa ni kwa nini Zitto alisema jana bungeni kwamba serikali inakataa kuchukua hatua, huku akijua kuwa ndiye aliyeanzisha suala hilo, na amekuwa anakwepa vikao na kamati iliyoundwa kumsaidia kuchunguza suala hilo, ambalo tayari ameiambia kamati kuwa hana majina wala akaunti.
VIA  DANSON KAIJAGE.

0 comment:

 

WASILIANA NASI KUPITIA 0715505043 / 0784505045 0768397241 / 0754505043

.

SIR.LOOM INC & MC BARAKA

.

IDADI YA WATU