Bukobawadau

HOTUBA YA MKUU WA MKOA MHESHIMIWA KANALI (MSTAAFU) FABIAN I. MASSAWE AKIFUNGUA KIKAO CHA KAMATI YA USHAURI MKOA (RCC) TAREHE 16 JANUARI, 2014


“Kagera Amani na Maendeleo, Amani na Maendeleo Kagera”
Kwanza kabisa nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na asili ya mema yote kwa kutulinda mwaka 2013 na kutuwezesha kuingia mwaka mpya wa 2014 tukiwa wazima.  Sambamba na hilo namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuhudhuria kikao cha leo ili tuweze kujadili mambo kadhaa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa mkoa wetu.  Aidha, nachukua fursa hii kuwakaribisha kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa kinachofanyika leo hii.
Ndugu Wajumbe, kikao cha leo ni cha kwanza katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, cha muhimu sana na cha kihistoria katika mkoa wetu.  Aidha, katika kikao hiki pamoja na agenda zingine tutapokea na kujadili taarifa utekelezaji wa mfumo mpya wa ufuatiliaji na usimamizi miradi ya maendeleo wenye kuleta Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now – BRN), taarifa ya Programu ya usambazaji umeme vijijini na hali ya umeme mkoani Kagera, taarifa ya hali ya ukuaji wa uchumi katika Kanda ya Ziwa Viktoria, taarifa kuhusu mchango wa taasisi za kifedha katika maendeleo na ustawi wa mkoa na Mapendekezo ya kuongeza vijiji na Vitongoji kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014.  Aidha, tutapokea taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Matumizi ya Kawaida na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka wa fedha tunaoendelea nao wa 2012/2013, 2013/2014 (Julai hadi Septemba) na Mapendekezo ya bajeti na mpango wa fedha kwa mwaka wa fedha 2014/2015. 
 Wajumbe

Ndugu Wajumbe, tofauti na ilivyozoeleka huko nyuma mwaka huu Serikali imeamua kubadilisha mzunguko wa kuandaa, kujadili, kupitisha na kutekeleza Bajeti ya Serikali.  Jambo hili linatugusa moja kwa moja na hivi leo kikao chetu kitapokea, kujadili na kupitisha Bajeti na Mpango wa Maendeleo wa Mkoa wetu wa mwaka wa fedha 2014/2015.  Aidha, nichukue nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wetu, kuitetea kwa nguvu zenu zote Bajeti ya Mkoa wetu katika Bunge la Bajeti linalotarajia kuanza mapema mwezi Aprili, 2014.





MFUUMO MPYA WA UFUATILIAJI NA USIMAMIZI WA MIRADI – MATOKEO MAKUBWA SASA

Ndugu Wajumbe, Mfumo wa tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) ni mfumo mpya wa ufuatiliaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo ambao umeanzishwa na serikali ili iweze kuleta matokeo ya haraka ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wetu.
Ndugu Wajumbe, napenda kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu mfumo huu wa Matokeo Makubwa Sasa kutokana na mkanganyiko wa kiuelewa juu ya dhana na malengo yake kwani baadhi ya watu wanautafsiri kuwa ni mpango huku wengine wakiutafsiri kuwa ni programu. Napenda ieleweke wazi kuwa serikali inao mpango wa miaka mitano mmoja wa 2011/2012 hadi 2015/2016. Hivyo, katika kuhakikisha kwamba malengo ya mpango huu yanafikiwa kwa wakati seriakali imeanzisha mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa. 
Ndugu Wajumbe, kwa kuanzia serikali inatekeleza mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa katika sekta za Kiwizara sita (6) ambazo ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Wizara ya Maji, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Nishati na Wizara ya Fedha. Katika Wizara ya Elimu na Mafunzo serikali imelenga kuongeza ubora wa elimu kwa kushughulikia changamoto zinazohusiana na masuala yanayohusu walimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, usimamizi wa mfumo wa elimu, tathmini ya ubora wa elimu na masuala mtambuka.

Aidha, kwenye Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika katika mkoa wa Kagera unalenga kuendeleza kilimo cha kibiashara kwa zao la miwa katika shamba la Kitengule lenye ukubwa wa hekta 16,500 liliko wilaya ya Karagwe. Katika mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa mkoa wetu unalenga kuongeza wa uzalishaji wa sukari tani 50,564 kwa kipindi cha 2013/2014 – 2015/2016 kwa kushirikisha Kiwanda cha Sukari cha Kagera.

Ndugu Wajumbe, chini ya mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa serikali imelenga kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi wetu. Kama inavyofahamika ni kwamba hali ya sasa ya upatikanaji wa maji kwenye maeneo ya vijiji ni asilimia 55.3, upatikanaji wa maji katika Manispaa ni asilimia 79 na kwenye makao makuu ya wilaya upatikanaji wa maji ni asilimia 69. Napenda kutoa wito kwa viongozi na watendaji mbalimbali wa wilaya kusimamia kikamilifu miradi ya maji inayoendelea kujengwa ili ikamilike na kutoa huduma kwa wananchi wetu. Vivyo, hivyo usimamizi ufanyike katika sekta za uchukuzi, nishati na Wizara ya Fedha ili halmashauri ziweze kuongeza mapato yake ya ndani.

USAFI WA MAZINGIRA
Ndugu Wajumbe, kutokana na ufanisi katika kuyatunza mazingira yetu na kuyaweka katika hali ya usafi, naendelea kuwapongeza viongozi na wananchi wote tunaoshikamana pamoja katika kuuweka Mkoa wetu katika hali ya usafi.  Nichukue nafasi hii pia kuwapongeza viongozi na Watendaji wa Manispaa ya Bukoba kwa kutunza mji wetu na kuufanya kuwa mshindi wa tatu (3) katika usafi wa miji ya Manispaa Kitaifa, hii pia ni fahari kwetu wana Kagera.  Aidha, niendelee kusisitiza kwa viongozi na Watendaji wa Halmashauri zetu zote kupanda miti kwa wingi ili kukamilisha lengo la Mkoa wetu la kupanda miti 13,479,000 kwa mwaka 2013/2014 idadi ambayo ni ndogo kama tutaamua kwa dhati kufanya kazi hiyo muhimu.  Ni matarajio yangu kuwa mnafahamu wazi suala la usafi wa mazingira kuwa ni pamoja na kuhakikisha takataka zinakusanywa na kuwekwa mahali panapostahili ili zichomwe au zifukiwe, utunzaji wa vyanzo vya maji, kuhakikisha kila kaya ina choo na siyo bora choo bali choo bora na kuyaweka majengo yetu katika hali ya kupendeza kwa kuyapaka rangi.  Ni imani yangu kuwa maelekezo haya yatatiliwa mkazo na miti itaendelea kupandwa kando kando ya barabara zote za Mkoa huu wa Kagera.  Haya ni maagizo ya Mheshimiwa Makamu wa Rais ambayo hatuwezi kuyakiuka.  Mvua zinazoendelea kunyesha zitumike vizuri ili kuhakikisha malengo ya upandaji miti yanafikiwa.

HALI YA CHAKULA MKOANI KAGERA
Ndugu wajumbe, Mkoa wetu kwa mwaka wa 2013/2014 ulilenga kulima hekta 721,597 za mazao mbalimbali ya chakula zilizotarajia kuzalisha jumla ya tani 3,199,334 zikiwa nafaka tani 337,562; kunde tani 148,799; ndizi tani 1,506,020 na mazao ya mizizi tani 1,231,611.  Wakati huo huo eneo lililolengwa kulimwa mazao ya biashara ni hekta 74,120 kwa lengo la kuvuna jumla ya tani 68,450 zikiwa kahawa za maganda tani 58,030; majani mabichi ya chai tani 7,845; pamba mbegu tani 1,575 na tumbaku tani 1,000.  Pamoja na kwamba mwaka huu mtawanyiko wa mvua kwa kipindi cha mvua za vuli haukuwa mzuri sana kwa maeneo kadhaa hata hivyo hali halisi kwa mavuno mashambani inaridhisha na tathmini inaonesha kuwa mkoa mzima hadi hivi sasa tuna ziada ya chakula.  Kwa pamoja tuzidi kujishughulisha katika kilimo cha kisasa na chenye tija kwa kufuata kanuni za kilimo.  Aidha, hali ya chakula kwa mkoa ni nzuri, hata hivyo nichukue nafasi hii kuwataka wajumbe waalikwa na wadau wengine kwenye mkoa wetu kuendelea kuhamasisha wananchi ili wazitumie mvua hizi za masika kwa kulima mazao yetu ya kawaida bila kuacha yale yanayokomaa kwa muda mfupi ili kuepuka kupatwa na njaa na ituwezeshe kuzalisha chakula cha ziada na tusaidie maeneo ambayo yatakuwa na upungufu wa chakula. Sehemu mbalimbali za nchi kuna taarifa za njaa.  Kwa bahati nzuri mkoa wetu hauko katika orodha ya mikoa ambayo iko katika hali hatarishi ya njaa. 

Ndugu wajumbe, pamoja na mkoa kutokuwa na tatizo la upungufu wa chakula bado inatakiwa tuongeze mbinu za uzalishaji ili tupate ziada itakayowezesha wakulima kuuza mazao na kujipatia kipato zaidi.  Hivyo matumizi ya pembejeo za kilimo na hasa mbolea na mbegu bora ni muhimu kwa watu wetu.  Matumizi ya zana za kilimo yatumike mfano matrekta n.k. tuachane na jembe la mkono.  Aidha, kwa mwaka 2012/2013 wakulima 25,000 walinufaika na mbolea za ruzuku katika Wilaya za Biharamulo, Missenyi, Karagwe na Ngara.  Idadi hii imepungua ikilinganishwa na wakulima 53,192 kwa mwaka 2011/2012.  Hii ni kwa sababu Wilaya ya Chato iliyokuwa kwenye mpango huo imehamishiwa Mkoa wa Geita na wakulima kadhaa wamemaliza miaka ya mkataba wao wa miaka mitatu (3) ya kupata mbolea za ruzuku.

Ndugu Wajumbe, imani yangu ni kwamba kwenye mkoa wetu pia tuna mifugo inayoweza kutupatia samadi ya kutosha kama wananchi wetu wataelimishwa, kutahamasishwa na kushirikishwa.  Ninasisitiza jamii zetu zihamasishwe kutumia samadi itokanayo na mifugo yetu, pasipo kusubiri mbolea za ruzuku tu ili zijiongezee uzalishaji.

HALI YA ELIMU
Ndugu wajumbe, kwa mwaka 2013 Mkoa wa Kagera ulisajili wanafunzi 43,154 kufanya mtihani darasa la saba. (Wav.20,257 na Was. 22,897) hawa ni 75% ya watoto 57,779 (Wav. 28,405 na Was. 29,374) walioandikishwa darasa la kwanza 2007, asilimia 25 kutomaliza elimu ya msingi si swala la kujivunia bali tunatakiwa tulilaani kwa pamoja na tupambane na sababu zote zinazofanya watoto wetu kutomaliza darasa la saba ambazo ni pamoja na utoro 418, mimba 16, vifo 13 n.k.

Kati ya wanafunzi waliosajiliwa kufanya mitihani ya darasa la saba, waliofaulu ni 24,546 (Wav. 11,919 na Was. 12,627) sawa na 58.1% ya wote waliofanya mitihani.  Katika mwaka huu wanafunzi wote waliofaulu mitihani ya darasa la saba wamepata nafasi za kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza. Kipekee ninachukua nafasi hii kuipongeza Halmashauri ya Wilaya Biharamulo kwa kuwa ya kwanza kimkoa ikiwa imefaulisha kwa asilimia 85.59 na Manispaa ya Bukoba asilimia 80.74 ambazo zimechangia mkoa wetu kuwa nafasi ya 7 Kitaifa. Vile vile nichukuwe nafasi hii kuziagiza Halmashauri za wilaya za Karagwe/Kyerwa (50.99%), Muleba (52.87%), Bukoba (53.41%) na Missenyi (58.59%) kuongeza bidii zaidi ili mwaka unaofuta ziweze kufaulisha kwa kiwango cha juu. Aidha, nichukuwe fursa hii kuwapongeza ninyi viongozi na watendaji mbalimbali kwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa miundombinu ya madarasa inayotosheleza mahitaji. Kipekee niwashukuru wananchi wote wa mkoa wa Kagera kwa kutoa michango yao ya nguvu na fedha ambayo imechangia kukamilika kwa miradi mbalimbali ya maendeleo hususan vyumba vya madarasa. Aidha, napenda kuwaagiza viongozi na watendaji wote wa serikali kuhakikisha mnasimamia na kushauri juu ya ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu ya maabara kwa kila shule ya sekondari ili kuongeza wigo wa watoto watakaosoma masomo ya sayansi.

UTEKELEZAJI WA OPERESHENI KIMBUNGA
Ndugu wajumbe, Mkoa wetu ni miungoni mwa mikoa ya pembezoni ambako zoezi la kuwaondoa wahamiaji haramu kutoka nchi za jirani linatekelezwa. Operesheni hii ilianza kufanyika kuanzia mwezi Oktoba, 2013 kwa kushirikisha wilaya na idara za serikali, hivi sasa operesheni inatekelezeka kwenye awamu ya nne ambapo katika awamu hii wananchi wanatoa taarifa kuhusu hali ya uhamiaji.

Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa kuwaondoa wahamiaji haramu katika ardhi ya mkoa Kagera ambao pamoja na athari zingine walihatarisha usalama wa wananchi wetu, uharibifu wa mazingira na kupokonya ardhi bila kufuata taratibu. Kipekee napongeza viongozi na wananchi kwa kutoa ushirikiano wa dhati wakati wote wa zoezi hili. Napenda kuwaagiza viongozi na watendaji wote wa wilaya kuendelea kushirikiana kwa kuwafichua wahamiaji na kuwachukulia hatua pale wanapoingia, tusisubiri wajenge himaya katika maeneo yetu. Aidha, tuendelee kutoa elimu kwa wananchi wetu ili wafahamu athari za uhamiaji hivyo washiriki kikamilifu katika kutoa taarifa zinazohusu wahamiaji haramu.  

Ndugu wajumbe, kama mnavyofahamu katika mwaka wa fedha wa 2013/14  mkoa wetu uliidhinishiwa kiasi cha fedha cha shilingi 174,925,757,000  kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya mishahara  na matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo.  Na hadi kufikia mwishoni mwa Oktoba, 2013 tulikwishapokea kutoka Hazina shilingi 49,924,168,457 sawa na asilimia 28.54. Katika kikao hiki tutapokea taarifa ya utekelezaji ya matumizi ya fedha hizo.
Katika utekelezaji wa bajeti ya 2013/2014 Mkoa ulijiwekea malengo ya kukusanya mapato ya ndani kwa Halmashauri zetu ambayo ni shilingi 13,737,670,000/=. Hadi Desemba, 2013 Halmashauri zilikuwa zimekusanya shilingi 4,541,794,736.5 sawa na asilimia 34.73, kwa mchanganuo ufuatao:- 
NA.
HALMASHAURI
MALENGO KWA MWAKA
MAKUSANYO HADI DESEMBA, 2013
ASILIMIA
1
Biharamulo
1,581,375,000
699,836,231.68
46.54
2
Bukoba
1,403,896,000
509,000,772.68
36.3
3
Manispaa
2,576,167,800
590,566,367.77
32.4
4
Karagwe
1,675,359,600
746,084,055.12
54
5
Kyerwa
1,798,538,040
550,219,015.00
31.18
6
Missenyi
1,090,000,000
365,093,020.60
34.12
7
Muleba
3,298,495,283
783,220,119.24
24.4
8
Ngara
1,577,130,001
297,775,154.41
18.9

JUMLA
13,737,670,000
4,541,794,736.5
34.73

Napenda kupongeze uongozi wa Wilaya za Karagwe kwa kuvuka lengo la asilimia hamsini (50%).  Wilaya hii inaonesha kuwa inaweza kufikia malengo waliyojiwekea, kwa Wilaya zilizobakia hali ya makusanyo sio ya kuridhisha ni vema kikao hiki kikajiridhisha ni kwanini Halmashauri hizo makusanyo ya ndani bado yako chini.

BAJETI NA MPANGO WA MAENDELEO WA 2014/2015
Ndugu Wajumbe, Kikao chetu hiki kitapata nafasi ya kujadili na kupitisha Bajeti na Mpango wa maendeleo wa Mkoa kwa mwaka ujao wa fedha wa 2014/2015. Mkoa unakusudia kuomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi 252,349,563,967 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo kwa Halmashauri zetu na Sektretarieti ya Mkoa kipindi cha mwaka wa fedha 2014/15. 

Ni matumaini yangu kwamba bajeti na mipango ya maendeleo kwa kila Halmashauri imejadiliwa na kupitishwa na vikao husika katika ngazi ya Wilaya.  Nachukua nafasi hii kuwataka wajumbe kupitia kwa makini Bajeti ya matumizi ya kawaida na maendeleo ya mkoa kwa ajili ya ustawi wa maisha ya wananchi wetu na maendeleo ya mkoa wetu.

Natumaini kuwa Waheshimiwa Wabunge wetu wataendelea kutetea bajeti ya Mkoa wetu katika Kamati za Bunge na kwenye kikao cha Bunge la Bajeti kilichopangwa kufanyika mwezi Machi, 2014.

Ndugu wajumbe, na waalikwa Mabibi na mabwana baada ya maelezo hayo natamka rasmi kwamba kikao chetu kimefunguliwa na nawatakia majadiliano mema.  


“KAGERA..... AMANI NA MAENDELEO, AMANI NA MAENDELEO........KAGERA”


Next Post Previous Post
Bukobawadau