Bukobawadau

USWAHIBA WA JK, KAWAMBWA UNAUA ELIMU;DK SLAA

Mbeya na Arusha. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema, uswahiba wa Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa ndiyo chanzo cha kuporomoka kwa cha elimu nchini.
Dk Slaa alisema hayo jana kwenye Viwanja vya Jojo Kata ya Santilya, Mbeya Vijijini ikiwa ni siku ya tatu ya Operesheni la Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), Pamoja Daima.
Alisema Dk Kawambwa hana uwezo wa kuongoza wizara hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa na Chadema kilishangazwa na mabadiliko aliyoyafanya Rais Kikwete katika baraza lake huku akimwacha waziri huyo katika nafasi hiyo.
“Kawambwa ni janga la elimu, hana uwezo. Chadema tutaendelea kumshtaki kwa wananchi. Mfumo mzima wa elimu nchini unahitaji mabadiliko, ili kufika huko wanahitajika viongozi wabunifu,” alisema Dk Slaa huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Aliongeza: “Elimu yetu iko shakani, sasa hivi mwenye shahada mbili anafanana na aliyemaliza darasa la nne la zamani.”
Alisema viongozi wa Serikali na CCM hawana uchungu kwa kuwa watoto wao wanasoma nje ya nchi hivyo aliwataka wananchi kuitosa CCM katika kila ngazi ya uchaguzi.
Dk Slaa alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama ‘Sugu’ aliwataka wananchi hao kumchagua mgombea Udiwani wa Chadema, Elisha Mwandele katika uchaguzi mdogo wa Kata ya Santilya utakaofanyika mwezi ujao.
“Ninyi wananchi ndiyo wenye mamlaka kwa kila kitu, nawaombeni mumchangue Mwandele ili awe diwani wa kata hii na mabadiliko yataendelea nchi nzima ili tutume salamu kwa CCM,” alisema Mbilinyi.
Katika hatua nyingine, Helikopta ‘Chopa’ inayotumika katika ziara hiyo ililazimika kukaa kwa zaidi ya saa mbili katika uwanja wa Jojo kutokana na mvua na ukungu.
Kabla ya kufika hapo helikopta hiyo ilikuwa ikitokea Kyela mkoani humo na baadaye hali ya hewa iliporejea katika hali ya kawaida ziara iliendelea kwa Jimbo la Mbozi, kisha kuelekea katika Mkoa wa Katavi.
Heche awabana Kinana, Nape 

Kutoka Arusha, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Heche amesema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape wanapaswa kujiuzulu, kutokana na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, kuwapuuza na kuwateua mawaziri waliowaita ni mizigo.
Mkutano huo ambao ulifanyika viwanja vya Ngusero Kata ya Sombetini, Heche alisema kama viongozi hao, walikuwa wanatoa kauli za kuwapinga kwa dhati mawaziri mizigo na siyo kuwalaghai wananchi wanapaswa kuwajibika wao kwa kupuuzwa na mwenyekiti wao.
“Sisi Chadema msimamo wetu upo wazi, hao mawaziri mizigo, tunajua hawana uwezo lakini CCM haina ubavu wa kuwang’oa,” alisema Heche.
Kwa upande wake, mwanasheria na Chadema, Tundu Lissu alisema Watanzania wasitarajie mabadiliko yoyote katika utendaji wa mawaziri.
Hata hivyo, Lissu alisema kazi kubwa ambayo wanapaswa kuifanya ni kujitokeza kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura ili wawe na uwezo wa kupitisha Katiba Mpya na kushiriki katika chaguzi.
Alisema msimamo wa chama hicho ni kuwa kama daftari la kura halitafanyiwa marekebisho wanachama wote wa chama hicho, watasusia kura ya maoni ya Katiba Mpya. Lissu alisema wanajua CCM ndio inafanya njama za kutoboreshwa daftari la kura kwa kuwa wanajua vijana wengi wakijiandikisha ndio utakuwa mwisho wa CCM.
Lissu pia alisema, CCM imeshindwa kuongoza ndiyo sababu imekuwa ikishindwa kusimamia hata rasilimali za nchi, yakiwamo madini, hifadhi za taifa na mambo mengi muhimu.
Awali, Lissu aliwataka wakazi wa kata hiyo kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili wamchague mgombea udiwani wa kata hiyo ya Sombetini kupitia Chadema, Ally Benanga.
“Mgombea wetu ni kijana wenu mnamjua, hivyo kazi ni moja tu kumpa kura siku ya uchaguzi Februari 9 mwaka huu,”alisema Lissu.
Taarifa ya nyongeza na Mussa Juma
Next Post Previous Post
Bukobawadau