Bukobawadau

ZITTO AIBUKA KIDEDEA MAHAKAMANI

Dar es Salaam. Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ameshinda maombi yake dhidi ya chama hicho mahakamani.
Katika maombi hayo namba 1 ya mwaka 2014, Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, aliiomba Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kuizua Kamati Kuu (CC) ya Chadema kumjadili au kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama wake.
Zitto kupitia kwa Wakili Albert Msando alikuwa akiiomba Mahakama itoe zuio hilo la muda hadi kesi yake ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Katika uamuzi wake jana, Mahakama Kuu ilikubaliana na maombi na hoja za Zitto na kutoa zuio kwa Kamati Kuu ya Chadema na au chombo chake chochote cha uamuzi kumjadili na kutoa uamuzi wowote kuhusiana na uanachama wake, hadi kesi yake ya msingi itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Awali, Mawakili wa Chadema wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu, Tundu Lissu na Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu, Peter Kibatala walipinga maombi hayo wakidai kuwa hayajakidhi matakwa ya kupewa zuio la muda.
Katika uamuzi wake, Jaji John Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili Msando kuwa maombi hayo yametimiza matakwa yote ya kupewa zuio hilo.
Matakwa hayo ni pamoja na kuwapo kwa mgogoro baina ya pande mbili, hasara au madhara yasiyoweza kufidiwa na usawa katika athari kwa pande zote.
Jaji Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili Msando kuwa iwapo Mahakama haitaingilia kati na kutoa zuio hilo, mtoa maombi ataathirika zaidi kuliko wajibu maombi.
Akijibu hoja ya Wakili Lissu aliyepinga hoja ya mtoa maombi kuathirika pamoja na wananchi wa jimbo lake kwa kukosa uwakilishi bungeni, kuwa hata akipoteza ubunge kwa kuvuliwa uanachama utaitishwa uchaguzi mdogo, Jaji Utamwa alisema uchaguzi mdogo huwa unachukua mchakato mrefu.
Baada ya kurejea vifungu mbalimbali vya sheria, kanuni, amri na uamuzi wa kesi mbalimbali za Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na za nje, Jaji Utamwa alisema anakubaliana mtoa maombi.
“Kwa hiyo ninatoa zuio la muda kwa Kamati Kuu ya Chadema na au chombo chake chochote cha uamuzi kwamba kisimjadili na kutoa uamuzi wowote dhidi ya mleta maombi kuhusiana na uanachama wake kusubiri kusikilizwa na kuamuriwa kwa kesi yake ya msingi,” alisema Jaji Utamwa.
Kabla ya kufikia uamuzi huo, Jaji Utamwa alitupilia mbali hati ya kiapo kinzani ya Chadema iliyotolewa na Wakili Kibatala baada ya kuwekewa pingamizi na Wakili Msando ambaye alidai kuwa katika hati hiyo, kuna taarifa za kusikia ambazo hakueleza alipozitoa.
Huku akirejea vifungu vya sheria, kanuni, amri na uamuzi wa Mahakama mbalimbali, alisisitiza kuwa ingawa wakili anaweza kuapa kwa niaba ya mteja wake, lakini anapaswa kueleza chanzo cha taarifa anazozitoa katika kiapo hicho.
Baada ya kutupilia mbali kiapo hicho, Jaji Utamwa alisema hata vielelezo vya wajibu maombi vinakufa kifo cha kawaida na kwa hali hiyo, maombi ya mtoa maombi yanabaki bila kupingwa na kwamba hakuna haja pia ya kujadili hoja za upande wa wajibu maombi.
Baada ya Jaji kutoa uamuzi huo, Zitto, aliwafuata mawakili wa Chadema na kupeana nao mikono kisha akaongozwa na walinzi wake kutoka nje ya Ukumbi wa Mahakama akipitia mlango maalumu unaotumiwa na jaji.
Kabla ya hukumu
Zitto aliyekuwa amevalia suti ya kijivu na shati la michirizi myeupe na ya kijivu aliwasili mahakamani hapo saa 7:45 mchana akiongozana na walinzi wake binafsi (mabaunsa), wapambe na wakili wake.
Baada ya kufika alikwenda katika chumba maalumu ambako alipumzika hadi saa 9:45 alasiri alipoingia katika ukumbi na kukaa katikati ya wapambe wake huku nyuma yake wakiwapo walinzi wake.
Jaji Utamwa aliingia mahakamani saa 9:56 alasiri na kuanza kusoma uamuzi wake akianzia na pingamizi la Zitto kwenye hati ya kiapo kinzani cha Chadema kisha akamalizia na uamuzi wa maombi ya msingi. Hukumu hiyo ilimalizika kusomwa saa 11:10 jioni.
Baada ya hukumu
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Wakili Msando alisema wameupokea kwa furaha uamuzi huo wa mahakama na kwamba hiyo ni hatua mojawapo ya haki akisema anaamini kuwa mteja wake atapata haki anayoitafuta.
Hata hivyo, Lissu na Kibatala kwa nyakati tofauti walisema kuwa ingawa wanakubaliana na uamuzi huo, hajawaridhika.
Maombi hayo ya Zitto yaliyotolewa uamuzi jana yanatokana na kesi ya msingi aliyofungua mahakamani hapo Januari 2, mwaka huu, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema.
Katika kesi hiyo anaiomba Mahakama izuie chama hicho, wakala wake na vyombo vyake vya uamuzi kumchukulia hatua zozote wala kumjadili kuhusiana na uanachama wake, hadi hapo rufaa anayokusudia kuikata Baraza Kuu la Chadema kupinga kuvuliwa nyadhifa zake itakaposikilizwa.

Kesi hiyo ya msingi imepangwa kutajwa Februari 13, 2014.
Mapambano tena
Wafuasi wa Chadema wanaomuunga mkono Zitto na wale wa uongozi wa juu, jana walipambana tena mahakamani kwa ngumi na mawe kisha kusababisha watu wawili kujeruhiwa.
Vurugu hizo zilitokea saa 7.55 mchana muda mfupi baada ya Zitto kuingia mahakamani.
Katika vurugu hizo, mmoja wa wafuasi hao ambaye jina lake halikujulikana mara moja, aliumizwa kichwani baada ya kupigwa na jiwe na mwingine alipigwa jiwe tumboni na kupelekwa hospitali.
Kutokana na vurugu hizo, polisi waliyatenganisha makundi hayo katika sehemu tofauti na kukaa katikati ili kuyatenganisha.
Wakati Zitto akiwasili mahakama hapo, wafuasi wake walikuwa wakiimba `Zitto Zitto kama Mandela’ hali iliyowalazimu wafanyakazi wa Mahakama kuingilia kati na kuwazuia.
Makundi hayo ya wafuasi wa chama hicho yalifika mapema saa 6:30 mchana mahakamani hapo kusikiliza uamuzi uamuzi wake.
Ulinzi katika eneo lote la Mahakama uliimarishwa, makundi ya polisi wa kawaida na wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), waliokuwa na silaha pamoja na mabomu ya machozi walitanda sambamba na askari wa kikosi cha mbwa, magari manane ya polisi na matatu ya maji ya kuwasha.
Kama ilivyokuwa juzi, ni wafuasi wachache walioruhusiwa kuingia ndani ya chumba cha Mahakama.
Baada ya mahakama kutangaza uamuzi wake, wafuasi wa Zitto walishangilia kwa nguvu na kuondoka wakiimba nyimbo za kumsifu kiongozi huyo.
Mtei amwonyesha mlango Zitto
 Mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei amemtaka Zitto aunde chama chake au atafute kingine cha kujiunga nacho kwa kuwa kwa sasa hana nafasi.
Pia ameshauri kuwa kama ana ndoto za kuwania urais ni vizuri akatafute vyama vingine kama CCM au CUF kwa kuwa ndani ya Chadema kwa sasa hahitajiki.
Mtei alisema kuwa kama anataka kubakia na uanachama wa Mahakama wao hawana shida... “Lakini huwezi kuwapeleka viongozi wako kortini na bado ukaendelea kubaki kuwa mwanachama wetu.”
Alimtuhumu kwa kuwagonganisha viongozi mbalimbali ndani ya Chadema na hata kuzua mitafaruku ya hapa na pale huku akisema kwamba uamuzi wa Kamati Kuu ndiyo wa mwisho.
KWA HISANI YA MWANANCHI
Next Post Previous Post
Bukobawadau