Bukobawadau

HIVI NDIVYO DR.KITILA ALIVYO MJIBU NGURUMO

Ndugu Ngurumo,

Nashukuru sana kwa maoni yako . Mimi binafsi ni muumini wa kutofautiana kimawazo katika msingi wa hoja. Siogopi hata kidogo mtu kupinga hoja zangu madamu tu anafanya hivyo kwa hoja. Hivyo naheshimu maoni yako pamoja na kwamba sikubaliani nawe.
 

Nadhani utakuwa hujasoma makala zangu zote za hivi karibuni na hasa ya juzi iliyochambua matokeo ya udiwani. Nasema hivi kwa sababu nimeogopa sana unaposema najenga hoja zangu kwa hisia bila ushahidi wa takwimu. Hapana. Soma makala zangu vizuri. Mimi ni muumini wa evidence based writing na nimejitahidi sana katika makala zangu kufanya hivyo.

Makala yako ina maoni mengi, ya msingi na mengine siyo ya msingi sana kama hilo la kusema kwamba ninaandika ninavyoandika sasa hivi kwa sababu nimetoka (nimefukuzwa) CHADEMA. Hii siyo hoja ya msingi kwa sababu hata wewe unajua ukweli kwamba mimi siungi au kukosoa jambo kwa minajili ya uchama, bila kujalai mimi ni wamachama wa husika au la. Sijaanza kuikosoa CHADEMA leo. Nilliikosoa CHADEMA nilipokuwa mwanachama ndani na nje ya vikao. Tofauti pekee. Nitakukumbusha matukio machache.

i) Tarehe 20 Nov 2013 niliandika makala iliyochapishwa katika Gazeti la Raia Mwema nikijadili umuhimu wa kutokuwakatisha tamaa wanaofanya vizuri katika jamii yetu. Katika makala haya, pamoja na mambo mengine, nilikosoa tabia ya viongozi wa CHADEMA ya kumzodoa mwenzao Zitto kwa kukataa posho. Nikaeleza waziwazi kwamba Zitto anapigwa vita ndani na nje ya chama kwenye mambo ya posho. Kwenye kikao cha Kamati Kuu cha tarehe 21 Nov 2013 Mhe Lema alinilalamikia kwamba kwa nini nawasema viongozi magazetini. Nikajibu kwamba mimi ninaandika kama mtu huru na kama mwanataaluma na ninapotoa mawazo yangu katika umma siangalia mambo ya vyama. Nitatoa maoni yangu kadri fikra zangu na evidence niliyo nayo zinavyonielekeza. Kwa kifupi, kama alivyowahi kusema Steve Biko, 'I write what I like'.

ii) Kwenye matokeo ya udiwani wa mwaka 2012 ambapo CHADEMA ilipata viti 5 kati ya viti 29 vilivyokuwa vinagombaniwa niliandika nikasema CHADEMA inakuwa lakini kwa kasi ndogo. Nikaeleza kwamba kasi ya ukuaji wa chama hiki ni ndogo ukilinganisha na ukubwa wa hamasa na mapenzi kwa chama yaliyopo mitaani. Nikajenga hoja kwamba ni muhimu kikajitathimini kwa nini hakipata kura sawasawa na aina ya hamasa iliyopo. Nikaeleza kwamba kwa kiwango hiki cha ukuaji, kinaweza kuongeza idadi ya madiwani na wabunge, lakini hakitaweza kushinda uchaguzi wa mwaka 2015 kwa maana ya kushika dola. Jambo hili nililieleza pia ndani ya Kamati Kuu lakini kwa ukali zaidi. Wenzangu hawakufurahishwa na wakasema kwamba mimi sielewi mambo ya field. Nikakubali yakaisha.

iii) Mwaka jana huohuo niliwapinga viongozi wangu wa chama ndani na nje ya vikao kuhusu kumuunga mkono Mbatia kwamba nchi yetu haina mtaala wa elimu. Niliwaeleza viongozi wangu kitaaluma jambo hili si kweli kwa sababu nchi haiwezi ikatoa elimu bila mtaala, na kwamba mtaala sio lazima uwe kwenye document moja inayoitwa mtaala. Niliandika hadi makala. Niliongea kwa simu na kiongozi wa chama akiwa Dodoma kuhudhuria vikao vya bunge. Wapo walionielewa na wengine hawakunielewa.

Kwa hiyo ndugu Ngurumo unaposema kwamba nilikuwa sikosoi kabla sijatoka CHADEMA unanionea au umeamua tu kujiridhisha juu ya hoja yako.

Unasema kwamba kusema CHADEMA si mbadala bila kuonyesha mbadala ni kuwachanganya wasomaji? Kwamba nasema hivi kwa sababu ya uchungu, hasira na chuki. Yes, nina uchungu na hasira, lakini sina chuki hata kidogo. Nina uchungu na hasira kwa sababu chama ambacho nilikitegemea kijenge taswira mpya ya siasa katika nchi hii kimeshindwa. Kinafanya mambo yale yale ambayo CCM wameyafanya kwa miaka chungu nzima. Nitaeleza kidogo hili.

Vyama vingi vilipoanza, CCM walipanick sana wakawa wanawatukana sana wapinzani. Wakawapa kila aina ya majina: mbwa, wanafiki, wasaliti, n.k., kisa wanatofautiana na wao kimsimamo. Lakini leo hii baada ya upinzani (soma CHADEMA) kukua na kujipatia wafuasi nao wanaanza kufanya mambo hayohayo ya kijinga waliyofanya CCM miaka ya tisini: kukebehi, kukejeli, kuwapaka matope na kuwaita wasaliti watu wanaotofautiana nao kimwazo na misimamo. Wapinzani wamejikuta wanauvaa uCCM bila wao kujua.

Sura ya chama inajengwa katika msingi wa hoja na uadilifu wa viongozi. Mambo yote haya hayapo katika upinzani wetu. Viongozi wetu nao wanapenda matumizi ya kutanua huku wakikandia serikali katika matumizi mabaya. Viongozi wetu wanabariki na kupokea maposho ya ajabuajabu bungeni huku wafanyakazi wengine katika nchi hii wakiteseka na viujira vidogo na wakijua msingi mojawapo wa chama ni usawa. Viongozi wanatukana na kukandia mashangingi ya serikali lakini wao wenyewe wananunua hayohayo kwa pesa za uma walizokopeshwa bila riba, na wengine wanachukua mashangingi ya serikali na kutembea nayo barabarani kwa madaha. Sasa huu si ndio uCCM wenyewe au? Unataka CHADEMA ionekana tofauti kwa kuuvaa uCCM?

Tukisema mnasema tuna hasira na uchungu. Ndio tuna uchungu kwa sababu chama hiki tulichokitegemea sana kimeuvaa uCCM na haiwezekani kikaaminika na kuchagulika kwa kuendeleza utamaduni wa uCCM. Ndio maana tunahitaji mbadala. Kwamba kwa sasa hivi hatuna mbadala haimanisha tusitamani na kutafuta mbadala. Tukishakujenga hoja ya uhitaji watu wanaojua namna ya kuanzisha mbadala wataanzisha. Kazi yangu ni kutoa mchango tu na wapo wengine nao watatoa mchango wao.

Mwisho, unaandika kana kwamba maoni yako ndiyo ukweli kiasi cha kusema kwamba sisi tuliyoenda shule tunapaswa kuyajua haya unayoyaandika, ebo kwani maoni yako ndiyo yamekuwa 2+2 ndugu yangu? Maoni yako ni maoni yako kama ambavyo ya kwangu ni maoni yangu, sio sheria. Hatuna uwezo wa kulazimisha watu wakubaliane na maoni yetu. Tunachofanya ni ushawishi tu wa hoja. Wapo watakaoshawishika na wapo ambao hawatashawishika kwa sababu zao: ama kwa kuona au kutoona uzito wa hoja au kwa kuwa tu wanampenda au hawampenda mwandishi wa hoja husika. Hiyo ndiyo tabia ya hadhira na huna namna ya kubadilisha hili. Tujifunze kuheshimu maoni ya wengine bila kulazimika kukubaliana nayo. Na tujifunze pia kutokulazimisha maoni yetu kuwa ndiyo ukweli!

Ahsante

Kitila
Next Post Previous Post
Bukobawadau