Bukobawadau

SIRI YAFICHUKA MAUAJI Z'BAR

Zanzibar Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji (KZU) na Polisi wamefanikiwa kuvunja zege lililokuwa limejengwa kufunika kisima walichotupwa raia wawili wa Ufaransa, baada ya kuuawa na kupata sehemu za miili yao ikiwamo fuvu la kichwa.
Aidha, siri za mauaji hayo zimeanza kuvuja, ikielezwa kwamba waliotekeleza unyama huo walilenga kupora nyumba na kiasi kikubwa cha fedha.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI) Yussuf Illembo, alisema kuwa hadi jana mchana, mifupa miwili ya mapaja, fuvu la kichwa na miwili ya mbavu imepatikana kutoka ndani ya kisima hicho.
Alisema kwamba Kikosi Kazi cha Uokoaji kinaendelea kufanya kazi eneo hilo la Matemwe lililopo Shehia ya Kaskazini, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
“Kazi bado ni ngumu, tunaendelea kuzamia ndani ya kisima na itakapokamilika tutatoa taarifa. Tuacheni kwanza tufanye kazi hii nzito na ngumu kwa wakati huu,” aliomba DCI Illembo.
Zoezi hilo lilifanyika huku likishuhudiwa na ofisa mmoja wa Ubalozi wa Ufaransa nchini na kuelezwa kuwa marehemu hao walinunua eneo la ardhi na nyumba kwa Sh150 milioni kwa kutumia jina moja la mzawa wa Zanzibar, kutokana na sheria kutoruhusu wageni kumiliki ardhi visiwani humo.
Watu hao, Francios Chererobert Daniel, aliyekuwa mtumishi mstaafu wa ngazi za juu wa Serikali ya Ufaransa na mkewe Brigette Mary, walipotea tangu Desemba 27 mwaka jana.
Baadaye taarifa za kupotea kwa watu hao zilifikishwa Polisi ndipo msako wa kuwatafuta ulipoanza na baadaye kugundulika kuwa, kuna watu wameuawa na miili yao kutupwa katika kisima cha maji kilichopo ndani ya ua wa nyumba hiyo.
Hata hivyo, baadhi ya waokoaji na mashuhuda wa tukio hilo, waliliambia gazeti hili kwamba sehemu hizo za mwili zinazosadikiwa kuwa za Wafaransa hao, zimefukuliwa baada ya kazi kubwa ya kuvunja zege kwa kutumia mashine maalumu inayofanywa na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na wakazi wa eneo hilo.
“Tumefanikiwa kutoa sehemu ya miili, imehifadhiwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja,” alisema mmoja wa mashuhuda aliyeomba jina lake lisitajwe.
Alisema kuwa kazi ya kuvunja zege hilo ilikuwa ngumu, walilazimika kuwachukua vijana wengine raia wa kawaida ili kuifanikisha.
Akielezea mazingira waliyokutana nayo chini ya kisima walichotupwa Wafaransa hao, alisema kuwa baada ya zege kuvunjwa walikuta nguo nyingi zimejazwa chini yake na juu yake kujengwa zege hilo kabla ya kumwagwa saruji isiyochanganywa kitu ili kufunika kisima kwa lengo la kupoteza ushahidi.
Hata hivyo, vyanzo vya habari vinaeleza kuwa zoezi hilo lililazimika kusitishwa kutokana na sehemu ya chini ya kisima kupita mkondo wa maji ya bahari, hivyo kulazimika kutafuta mashine ya kuvuta maji.
“Kazi hiyo ikiweza kufanyika ndipo tutakapoweza kwenda katika kina kirefu zaidi cha kisima hicho ili kukusanya mifupa. Tukipata idadi ya mifupa na mafuvu yote, tutaweza kujua waliouawa ni wangapi,” kilieleza chanzo kimoja.
Sheha wa Shehia ya Matemwe Kusini, Denge Khamis Silima alisema kuwa wanapata faraja kuona zoezi hilo limepata mafanikio tofauti na siku ya kwanza na kwamba kazi hiyo inaendelea kufanyika kwa umakini huku akiitaka Serikali kuwapatia vifaa waokoaji ili kufanikisha kazi hiyo.
Siri ya mauaji
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa siri ya mauaji hayo ni baadhi ya watu kutaka kupora nyumba, waliyokuwa wakiishi Wafaransa hao pamoja na fedha zinazodaiwa walikuwa nazo raia hao wa kigeni wakitaka kununua eneo la kujenga hoteli kwenye ufukwe wa Urowa.
Inelezwa kuwa kabla ya kuingia Zanzibar, Wafaransa hao walifikia Nairobi nchini Kenya ambako inadaiwa kuwa mmoja wa wanasiasa wakongwe nchini humo aliwashauri kwenda Zanzibar kuishi na kuwekeza.
Taarifa zaidi kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zinaeleza kuwa mazingira ya tukio hilo yanaonyesha kuwa kabla ya watu hao kuuawa, mbwa wao aliyekuwa akifahamika kwa jina la Allan, alipewa chakula chenye sumu na kufa na kwamba sehemu ya mabaki ya chakula hicho yaliliwa na mbwa wa jirani ambaye pia alikufa.
Aidha, mifuko mitupu ya saruji inayosadikiwa kutumika katika ujenzi wa zege la kisima hicho, imeokotwa nyuma ya ukuta wa nyumba hiyo waliyokuwa wakiishi Wafaransa hao.
CHANZO MWANANCHI.
Next Post Previous Post
Bukobawadau