Bukobawadau

BUNGE MAALUMU:KUNOGA KUSISAHAULISHE CHUNGU

Na Prudence Karugendo
JUMA lililopita niliandika nikionyesha namna ukosefu wa hoja, hekima, umakini, busara na haki na badala yake ukatamalaki ubabe, unavyoweza kuipeleka nchi kuzimu. Nilitoa mifano kadhaa iliyo hai kukishadidia kitu hicho, katika kutahadharisha kwamba hali tuliyo nayo Tanzania, amani na utulivu, tunaweza tukaipoteza tusipokuwa makini na vitu hivyo.
Wasomaji wengi wamenishauri niuendeleze mjadala huo wakisema kwamba unafaa sana kwa mustakabali wa nchi yetu hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaandaa utaratibu mpya wa kujiendesha, uandaaji wa Sheria Mama au Katiba Mpya ya nchi.
Wapo wasomaji waliofikia kunikumbusha usemi wa Kihaya wa “Bagambira balinsi baliguru kuhurira” wenye maana ya kwamba wanaambiwa walio chini lakini walio juu, ambao ndio walengwa, wanasikia na kupata ujumbe. Usemi huo unatokana na hadithi ya kwamba mnyama mmoja alienda kwa mganga ili ampatie tiba, kinga, inayomdhibiti mnyama mwingine aliyewamaliza wenzake kwa kuwala.
Wakati mganga ameanza kutoa tiba na maelekezo, yule mnyama mla wanyama wenzake akatokezea, ikabidi yule anayetafuta tiba apande kwenye mti harakaharaka kusudi asije kufumaniwa chini na kutafunwa na huyo nyamaume.
Wakati mganga akiendelea kutoa tiba yule mnyama mla wenzie akafika akimuangalia mganga bila kuelewa anachokisema, mganga akimaliza kutoa maelekezo ana “send message” akisema wanaambiwa walio chini walio juu wanasikia! “Bagambira balinsi baliguru kuhurira”, yule aliye juu anapata ujumbe na kuelewa cha kufanya!
Msomaji mmoja wa Arusha amechangia mjadala huu akisema kwamba ni bora hili la kuichokonoa amani na utulivu tulivyo navyo tukalijadili kwa upana kutokana na hali halisi tuliyomo kwa sasa nchini mwetu. Akaongeza kwamba kwa wakati huu Mungu haleti tena manabii wa kutabiri yatakayojiri, isipokuwa inaonekana kazi hiyo kaiacha ifanywe na waandishi.
Akaongeza kwamba kupitia kwa waandishi tunaweza tukaiona hatari iliyo mbele yetu, kwahiyo tukaamua kuepukana nayo au kukaidi tukaamua kuiingia hali hiyo ya hatari lakini tukiwa hatuna kisingizio cha kwamba hatukujua.
Tuendelee na mjadala wetu. Kwa wakati huu tumo katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya nchi yetu. Sote tunaelewa kuwa Katiba ya nchi ndio utaratibu mama ambao kila mwananchi na yeyote anayekuwa nchini mwetu, hata akiwa mgeni, anatakiwa na kulazimika kuufuata. Ni kwa maana hiyo hakuna anayepaswa kuwa juu ya Katiba ya nchi. Hata rais, aliye kiongozi mkuu, anakula kiapo cha kuiheshimu, kuitumikia na kuilinda Katiba ya nchi. Yuko chini ya Katiba.
Ni mahali hapo ninapoona kwamba, katika mchakato huu, hatukuhitaji mtu wa kutuchagulia au kututeulia mtu au kikundi cha kuwakilisha mawazo au mitazamo yetu kuhusu ni utaratibu gani tunaohitaji uongoze nchi yetu. Ni kwamba sisi wenyewe, katika makundi yetu, ndio tulitakiwa tupendekeze majina miongoni mwetu ya kwenda moja kwa moja, bila kupitia kwingine, kwenda kuunda kitu kinachojulikana kama Baraza la Kutunga Katiba au Bunge Maalumu la Katiba.
Hii maana yake ni kwamba nchi yetu, mbali na wananchi katika makundi yao, pia ina mihimili mitatu inayoifanya isimame kama nchi. Inao mhimili wa Uongozi au Utawala chini ya Rais, Mahakama chini ya Jaji Mkuu na Bunge chini ya Spika.
Kwahiyo tunapotengeneza utaratibu mama wa kuendesha nchi yetu tulitakiwa sote tuwe sawa kwa maana ya utawala kupendekeza wawakilishi wake, Bunge wawakilishi wake, mahakama wawakilishi wake na wananchi katika makundi yao kuwa na wawakilishi wao.
Kwa mpangilio huo ningetegemea wawakilishi toka kundi la wananchi kuwa na idadi kubwa ya uwakilishi kuliko makundi mengine matatu niliyoyataja kutokana na wingi wa wananchi katika makundi yao tofautitofauti. Lakini bahati mbaya mambo yamekuwa kinyume!
Idadi kubwa ya wajumbe wa Bunge Maalumu tumeona ilivyokwenda kwa wanasiasa, hasa wabunge, ambao nafasi zao za ubunge na uwakilishi, kwa upande wa Visiwani, zimekuwa tiketi za moja kwa moja kwenye Bunge Maalumu, jambo linaloonekana kufuta maana halisi ya neno Bunge Maalumu.
Bunge hili linakuwaje maalumu wakati sura ni zilezile za Bunge la Jamhuri na Baraza la Wawakilishi? Nilitegemea tunaposema Bunge Maalumu tuwe na kitu maalumu kwa maana halisi, sura mpya na maalumu. Na kupitia katika upya na umaalumu huo ndipo nilitegemea kipatikane kitu kipya na maalumu, Katiba Mpya.
Lakini kwa sura hizi tulizozizoea, tukiondoa chache zilizochomekwachomekwa, na nyingi zikiwa ni zile zilizozoeleka katika duru za siasa, hasa kwa upande wa chama tawala, ninayo mashaka makubwa ya kukipata kitu kipya ambacho tutakiita Katiba Mpya.
Kama tunavyoelewa Katiba Mpya imeshinikizwa iwepo katika kujaribu kuuondoa mfumo kongwe ambao ni kama umeifanya nchi yetu idumae. Tuelewe kwamba upande wa chama tawala Katiba Mpya ni neno lililokuwa halijulikani kabisa kwenye msamiati wake. Upande huo ulitaka katiba iliyopo iendelee, kwa vile pengine ndio ulioiboresha mwaka 1977 kutoka ile iliyorithiwa kwa wakoloni.
Hapana shaka kwamba katiba hii tuliyo nayo kwa sasa ilikuwa inaupendelea sana upande ulioiboresha, kwa ufupi upande wa CCM. Labda hiyo ndiyo iliyokuwa siri ya CCM kujigamba kuwa itaitawala nchi milele. Na hiyo ilikuwa na maana ya kwamba nchi yetu ingeendelea kuwa changa milele yote! Kwa kufuata kaulimbiu ya kudumu ya CCM ya kwamba nchi yetu ni changa!
Pamoja na hilo, tatizo kubwa linaloikabili nchi yetu ni la kutopenda kuwa na mtazamo wa milele kwa manufaa ya wananchi wote, waliopo kwa sasa na hata vizazi vijavyo. Kinachoonekana ni mtu kutaka kujinufaisha yeye binafsi mpaka pale anapodhani uhai wake utakuwa haupo tena. Kwa maana ya kujinufaisha kwa muda mfupi, hakuna anayelenga mbele ya muda wa uhai wake.
Ndiyo maana tuliwaona wajumbe wa Bunge Maalumu wakitanguliza posho bila kujali unyeti wa kazi waliyokabidhiwa!
Wakati nafuatilia mijadala ya awali ya Bunge Maalumu nimesikitika kuwasikia baadhi wajumbe wakisema kwamba hapa wanatengeneza kitu cha kati ya miaka 25 na 50! Sijamsikia mwenye mtazamo wa kitu cha milele! Sijui hiyo ni kutokana na nchi yetu kuendelea kujivunia uchanga!
Marekani, kwa mfano, ni taifa kubwa na kongwe. Sikuwahi kusikia ni lini taifa hilo lilikuwa changa. Lazima kuna wakati lilikuwa changa, lakini halikuwahi kujivunia uchanga. Ndiyo sababu uchanga wake haujulikani pengine.
Katiba ya Marekani inayotumika mpaka sasa iliandikwa na watu wasiozidi 10 wakipata ushauri toka kwa watu wasiozidi 63, mwaka 1787, na katiba hiyo kuanza kutumika mwaka 1788. Mpaka leo katiba hiyo ina umri wa miaka 226. Katika kipindi chote hicho yalipendekezwa marekebisho 33 lakini yakaridhiwa 27 tu.
Pamoja na uchanga wetu, hivi kweli tunaamini kwamba Wamarekani wanatuzidi akili kwa kiasi chote hicho? Yaani akili walizokuwa nazo mwaka 1787 hatujaweza kuzifikia hata baada ya miaka 226!
Fikiria watu wasiozidi 10, mwaka 1787 walitayarisha utaratibu wa kuiendesha nchi yao milele yote, wakati sisi, zaidi ya watu 600 bado hawaonyeshi dalili za kutengeneza utaratibu tunaoweza kuutumia walau kwa miaka 50!
Nimesikia mjumbe mmojawapo wa Bunge Maalumu akidai kwamba Katiba ya Marekani haikupata maoni ya wananchi. Hilo ni wazo potofu. Marekani kama tunavyoifahamu itakosaje Katiba yenye maoni ya wananchi halafu Katiba hiyo idumu kwa miaka 226? Na inawezekanaje Katiba isiyokuwa na maoni ya wananchi iliwezeshe taifa kuwa na mafanikio ya kutugeuza sisi wengine ombaomba wao wa kudumu?
Na je, kama kweli sisi tunajali maoni mbona maoni ya Watanzania yanayosema serikali tatu yanapigwa vita na chama tawala? Hayo maoni ya wananchi ni ya nini yasiyotakiwa kuheshimiwa na chama tawala?
Mimi naamini kwamba wale Wamarekani 10 waliweka umimi pembeni na kuvaa roho za Wamarekani wote, waliokuwepo wakati huo mpaka waliopo sasa hivi, wakaamua kufanya kazi hiyo, tena kwa kujitolea. Hao ni tofauti na hawa wa kwetu zaidi ya 600 ambao kipaumbele chao kilikuwa ni kuongezewa posho kwanza pamoja na ukweli kwamba posho wanayoipata ni kufuru tupu.
Zipo dalili za wazi kwamba mtindo wa kuendesha au kupitisha mambo yanayowahusu wananchi na nchi kwa kunogewa ndio unaoweza kutumika hapa kufikia maamuzi. Mtindo huo unaoegemea kwenye wingi wa uwakilishi, unaweza kuwafanya baadhi ya wawakilishi wetu wapitishe mambo kadiri ya kunoga uko kulivyo.
Pengine ndiyo maana tunaona muda wa Bunge Maalumu unacheleweshwa makusudi bila yeyote kutilia maanani kuwa Watanzania wanatakiwa wamlipe kila mjumbe kiasi kisichopungua laki tatu kila siku! Hata hivyo wajumbe hao wanaona kiasi hicho bado ni kidogo walitaka, na bado wanataka, kiongezwe! Sababu wao wanaonekana wamepata fursa ya kuvuna, mambo ya Katiba Mpya ni mengineyo.
Hapo ndipo nawashauri wajumbe wa Bunge Maalumu kwamba kunogewa kusiwafanye wakasahau chungu. Kule Libya wananchi wasiovumilia upuuzi majuzi walilivamia Bunge la nchi hiyo, ambalo kutokana na kunogewa, lilikuwa limejiongezea muda wa kuendelea kuwa madarakani, wakawapa chungu wabunge wao na kuwafanya wabunge hao wasilitamani tena Bunge!
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau