Bukobawadau

TUACHE MASLAHI BINAFSI TUTAFUTE KATIBA YA NCHI

Na Prudence Karugendo
MCHAKATO  wa kuandika Katiba mpya ya taifa letu umefika mahali pagumu. Ni pagumu kwa vile mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba hauonyeshi kutoa kile ambacho wananchi wanakisubiri kwa hamu sana.
Bunge hili ambalo ni hatua ya mwisho ya mchakato wa kuipata Katiba mpya kabla ya wananchi kuamua kama inawafaa kwa kuiridhia au kuikataa, linaonekana limejaa watu wenye malengo na matamanio yanayotofautiana sana, kama vile wametoka nchi mbalimbali tofauti, ila wote wakijiita Watanzania!
Sio kwamba tofauti ninazoziona na kuzisema zinatokana na kile kilicholiunda Bunge hilo, yaani makundi ya wanasiasa, ikiwa ni wa upande wa chama tawala na wa upinzani, Wazanzibari na Watanganyika pamoja na wa makundi mengine kulingana na ilivyomfurahisha rais katika uteuzi wake wa wajumbe wa Bunge hilo. Ninachokiona ni kitu tofauti kabisa.
Utofauti wake uko hivi; wamo wanasiasa walio katika pande mbili hasimu, yaaniwa upinzani na wa chama tawala, ila uhasimu wao unafanana kwa namna moja au nyingine, maslahi binafsi. Wale wa CCM wanaonekana kuutetea u CCM wao ambao inajionyesha wazi kuwa hawautetei kwa kukipenda sana chama chao ila kwa maslahi yao binafsi waliyoyawekeza kwenye chama hicho. Vilevile kwa upande wa upinzani nako wapo wanaoonekana kuutetea upande huo wakionekana kuyasaka maslahi binafsi wanayoyaona huko.
Wote hao, wa upinzani na wa chama tawala, hakuna wanaosukumwa na uzalendo kwa nchi yao kuyatetea wanayoyaona yanafaa kwa nchi yao na watu wake.
Ila pia wapo wanaoonyesha uzalendo wa kweli wakionekana kukipigania kilicho bora kwa nchi yao, hata kama  hakitawanufaisha wao kwa wakati huu, ila wakiangalia mbele wanaona kuwa kuna vizazi vijavyo.
Kitu cha kwanza kilichonishtua na kunifanya nijiulize inakuwaje, ni pale mwenyekiti wa Bunge hilo alipokuwa anatoa shukurani baada ya kuchaguliwa. Furaha aliyoionyesha ilionekana kumvua uzalendo wake, sababu hakuonekana kama kakabidhiwa jukumu la umma bali jukumu binafsi!
Furaha aliyoipata ilimfanya awashukuru hata ambao hawakuhusika kumchagua! Maana tukimuacha mke wake, ambaye naye ni mjumbe wa Bunge hilo Maalumu, pia aliwashukuru watoto wake, majirani zake, waumini anaosali nao kanisa moja nakadhalika!
Furaha hiyo ya mwenyekiti, kusema ukweli,  ilininyima amani. Sikuuona uzalendo wowote katika furaha hiyo. Ile ilikuwa ni furaha binafsi ikionyesha mafanikio binafsi, haikuonyesha mafanikio ya umma yanayoweza kuashiria uzalendo wa mtu kwa nchi na watu wake.
Katika kudhihirisha ninachokisema, tulimuona mwenyekiti wa Bunge Maalumu akibadilisha au kukiuka kanuni za Bunge hilo mara tu alipokalia kiti chake. Alibadilisha kanuni ili Jaji Warioba aanze kuwasilisha Rasimu hata kabla ya Bunge kuzinduliwa.
Mbali na mwenyekiti pia tulimsikia mbunge mmoja akidiriki kumwaga machozi akikataa mambo yasiende kinyume na matakwa ya chama chake. Ni wazi mbunge huyo hakuwa anaililia nchi yake wala chama chake, isipokuwa maslahi yake binafsi aliyoyawekeza kwenye chama chake.
Baada ya kujiridhisha kuwa limo tatizo la ubinafsi katika mchakato huu wa uandikaji wa Katiba mpya ya nchi yetu, wananchi sote kwa pamoja, kama wazalendo, tunachotakiwa kuwashauri wajumbe waliomo katika Bunge hilo maalumu ni kitu gani wanapaswa kukifanya ili tuweze kukipata kile tunachokitarajia.
Na ushauri wenyewe ni wa kwamba wayaweke pembeni maslahi binafsi kwanza, wawe kitu kimoja wakiongozwa na uzalendo kwa nchi yao, tuipate Katiba ya nchi kwanza na mengine yaendelee baadaye.
Ni kwa sababu Katiba ya nchi haipaswi kuwa kitu cha wananchi kukitumia kukomoana, badala yake Katiba ndio muongozo wa wananchi kufikia maelewano na hatimaye makubaliano.
Maana ikiandikwa Katiba inayoonekana kukibana chama kilicho madarakani kwa sasa huku ikitoa unafuu kwa upinzani na kuuwezesha kushika madaraka kirahisi, tutakuwa tumerudi kulekule tunakotoka. Tutakuwa tumetengeneza mchezo wa mzunguko ambao Waingereza wanauita “marry go round”.
Sababu inaaminika kwamba Katiba iliyopo inatumiwa vibaya na chama tawala, CCM, kwa manufaa yake. Itawezekanaje hiyo mpya itakayoandikwa ionekane inawapendelea wapinzani kiasi cha kuwaingiza madarakaini kirahisi nao wasiweze kuitumia vibaya kwa manufaa yao dhidi ya wale ambao hawako madarakani? Je, na hao ambao watakuwa hawako madarakani watakosaje kudai Katiba nyingine mpya? Si utakuwa mchezo wa kuandika Katiba kila chama kinapoondolewa madarakani?
Kwa upande wa CCM ni kwamba hawatakubali itengenezwe Katiba itakayowanyang’anya tonge mdomoni. Ndiyo maana tunaona kwamba huu mchakato wa Katiba mpya umegubikwa na makada wa chama hicho.
Mbali na chama hicho kuwa na wabunge wengi, ambao ni kama robo tatu ya wabunge wote, bado kuna makada wa chama hicho walioingizwa kwenye Bunge Maalumu kupitia kwenye makundi ya vijana, wafugaji, wavuvi, waganga wa kienyeji nakadhalika.
Sio kwamba makada hao wa CCM wamekuwa kwenye makundi hayo kwa bahati mbaya tu, la hasha, ni wazi kwamba huo ni mpango mahususi wa chama hicho kuyalinda maslahi binafsi ya makada wake ya wakati uliopo, kukiwa hakuna fikra ya kwamba kuna wakati ujao na vizazi vijavyo huko mbele katika nchi hii!
Inawezekanaje chama ambacho hakikuwa na wazo la Katiba mpya, kikiwa na imani kwamba Katiba hii iliyovaa matambara yenye viraka vinavyopachikwa kulingana na matamanio ya wakati, ndiyo inayofaa kudumu muda wote,  leo hii kiwajaze makada wake kwenye mchakato wa kuandika Katiba mpya? Nani anayeweza kuamini kuwa kuna nia njema katika wingi huo wa wajumbe walio makada wa CCM?
Kwahiyo tunapoiangalia hivyo CCM, kwamba haina nia njema na Katiba mpya, hatunabudi kujivua umakundi na kuuvaa uzalendo ili CCM ipate fundisho. Ni uzalendo pekee utakaowezesha Katiba mpya ipatikane.
Lakini tukiendelea kuinyoonyea tu kidole CCM huku tukiwa tumejibanza kwenye u Chadema, u NCCR, u CUF nakadhalika, hatuna namna yoyote tunayoweza kuwashawishi CCM wajiondoe kwenye u CCM wao. Tutabaki kila mtu na kikundi chake tukicheza mchezo wa mwenye kupata apate na mwenye kukosa akose.
Nilishasema, na sasa narudia, kwamba Katiba ya nchi ya Marekani, taifa kubwa na lenye nguvu za kila aina karibu kupita mataifa yote duniani, ilitengenezwa na watu 10 tu! Watu hao hawakuwa na mlolongo wa mambo ya kupoteza muda bure kama hawa wa kwetu zaidi ya 600.
Wale ni watu waliouvaa uzalendo wa nchi yao wakiwa hawana ukada wowote wala umakundi wa aina yoyote.
Walichokifanya bado kinaheshimika hata baada ya miaka 226!
Je, hawa wa kwetu zaidi ya 600, ambao wanachokifanya hawawezi hata kukiheshimu wao wenyewe, kitaweza kuheshimika kwa wananchi hata kwa miaka 2 ijayo?
Sababu kinachoonekana ni kila mjumbe kulipigania kundi lake. Mpaka tumeanza kushuhudia matusi ya nguoni yakiwatoka baadhi ya wajumbe. Hivi kweli katika kutengeneza Katiba ya nchi, kwa manufaa ya watu wote waliopo nchini kwa sasa na vizazi vijavyo, yanaweza yakamtoka mtu matusi ya nguoni?
Je, naye huyo tumuite mzalendo au ni mtu tu anayesukumwa na tumbo lake kuyatetea maslahi anayoyaona kwa sasa bila kujua kama kuna kesho?
Wakati Jaji Warioba anawasilisha Rasimu  kwa kitu ambacho kilikuwa hakijawa Bunge Maalumu, kwa vile lilikuwa bado halijazinduliwa, alishauri Katiba mpya itambue serikali tatu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya hapo ndipo Rais Kikwete akaja kuzindua Bunge. Kabla ya kuzindua akaanza kuijibu minong’ono aliyoikuta ya serikali tatu. Naita minong’ono sababu rais aliikuta kabla ya kulizindua Bunge Maalumu. Kitu chochote kilichokuwepo kabla ya hapo hakikuwa rasmi sababu Bunge halikuwepo. Yaliyokuwepo ni maandalizi tu.
Kwa maelezo yaliyokuwepo ni kwamba Bunge Maalumu lingeanza kuitwa Bunge baada ya kuzinduliwa na rais.
Katika majibu yake kwa minong’ono iliyokuwepo ya serikali tatu rais alionekana wazi kutetea serikali mbili. Sikumshangaa rais kutokana na mambo mawili. Kwanza yeye alikula kiapo cha kulinda nchi yenye serikali mbili. Kwa maana hiyo ni lazima akitetee kiapo chake. Nadhani nje ya hapo ingemwia vigumu kuendelea kujitambua kama rais, rais wa nchi gani?
Kitu cha pili ni kwamba, unapotaja serikali tatu maana yake ni kwamba Tanzania haipo tena,  na Muungano ndiyo basi. Kwahiyo Katiba inayoandikwa ni ya nchi gani? Si bora ingesemwa kwamba inatafutwa Katiba ya Tanganyika kwa vile Zanzibar tayari inayo Katiba ya kwake? Kusema ukweli kwa hilo rais nilimuelewa.
Nimalizie kwa kusema kwamba vyama 15 vya siasa visivyokuwa na wabunge, vinavyounda Baraza la Vyama vya Siasa,  vinajiwakilisha vyenyewe na si wananchi. Walau vingekuwa na mbunge mmoja mmoja ningeamini kwamba vinawawakilisha hao walioviwezesha vikapata mbunge mmoja mmoja.
Mwisho, ni kwamba ingekuwa vema CCM nayo ikajiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi, UKAWA, kama kweli chama hicho kinaitafuta Katiba ya wananchi. Kitendo cha kuwa nje ya UKAWA kinadhihirisha kuwa CCM haitafuti Katiba ya wananchi bali inachokifanya inakijua yenyewe!
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau