Bukobawadau

WARIOBA UMENIRAHISISHIA KAZI YA KUIFUFUA TANGANYIKA:MTIKILA

Mjumbe wa Bunge la Katiba, Mchungaji Christopher Mtikila amesema madai yake ya zaidi ya miaka 20 kuhusu Serikali ya Tanganyika yamerahisishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na ana imani Tanganyika inarejea muda mfupi ujao.
Akizungumza na gazeti hili nje ya viwanja vya Bunge, Mchungaji Mtikila, alisema amefarijika kuona Jaji Warioba amewafahamisha Watanzania kuhusu ukweli wa Muungano, hivyo wanaweza kuelewa sasa sababu za yeye kudai Tanganyika.
"Naamini sasa Tanganyika inarudi, lakini watu wachache wakizuia safari hii nitakwenda Mahakama ya Umoja wa Mataifa kudai Tanganyika kwani ndio ilipigania uhuru na tayari nina mawakili," alisema.
Aliongeza kuwa Jaji Warioba ameunga mkono hoja ya kudai Tanganyika kwani haiwezi kupotezwa na watu wachache kwani tayari Zanzibar imejitangaza kuwa ni nchi huru ndani ya Muungano.
Alisema Muungano ni suala la hiari, hivyo viongozi wachache wa chama tawala hawawezi kulazimisha Muundo wa Muungano ambao unapingwa na mamilioni ya Watanzania.
"Naamini wale waliokuwa wamechomwa sindano za usingizi wa miaka yote sasa watafufuka na kuungana na wazalendo waliopigania uhuru wa Tanganyika na sasa imekuwa koloni la Zanzibar," alisema Mtikila.
Alisema muundo wa Muungano uliopo sasa wa serikali mbili ni kongwa la utumwa wa kikundi cha watu wachache ndani ya CCM ambao ndio wananufaika.
Chanzo:Mwananchi
Next Post Previous Post
Bukobawadau