Bukobawadau

BALOZI WA CHINA NCHINI TANZANIA AHAIDI UWEKEZAJI MKUBWA TOKA CHINA KATIKA MKOANI KAGERA

 Balozi Lu Youqing wa Kwanza Kushoto Akiwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Massawe Katikati na KatibuTawala wa Mkoa wa kagera Bw. Nassor mnambila.
 Balozi Lu Akiwa na mkarimani Wake Bw.Ren
Mkuu wa Mkoa wa kagera Mhe Massawe Akimkaribisha Balozi wa China Nchini Tanzania Dk. Lu Youqing Mkoani Kagera.
  Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Nassor Mnambila Akiwasilisha Mada kuhusu Fursa za Uwekezaji Mkoani Kagera
  Balozi Lu Youqing Akifurahia Jambo
  Mkoa wa  wa Kagera ukiongozwa na Mhe. Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe umefanya mkutano wa uwekezaji na nchi ya China iliyowakilishwa na ujumbe ulioongozwa na  Balozi wa China  nchini Tanzania Dk. Lu Younqing.
Balozi Lu Younqing  na ujumbe wake walifika  mkoani Kagera  tarehe 16/04/2014 kwa lengo la kuhudhuria mkutano wa pamoja na mkoa wa kuhusu uwekezaji katika sekta mbalimbali na kujionea fursa zilizopo mkoani hapa kwa ajili ya uwekezaji.
Akimkaribisha Balozi Lu Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Massawe alimshukuru kwa kufikiria kuja mkoani hapa kujionea mwenyewe fursa zilizopo na kumhakikishia ushirikiano mzuri kwa wawekezaji toka nchini China kuja kuwekeza na kuinua uchumi wawananchi wa mkoa wa Kagera .
Katika mkutano huo wa pamoja wa uwekezaji mkoa wa Kagera uliwasilisha mbele ya Balozi Lu na ujumbe wake fursa muhimu na Sekta mbalimbali za kuwekeza ili kuinua uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla kama ifuatavyo:
Sekta na fursa  hizo  ni pamoja na Viwanda, Kilimo cha umwagiliaji, Uzalishaji na usafirishaji wa ndizi, Ufugaji wa kisasa, Usindikaji wa nyama na maziwa, Uvuvi na ufugaji wa samaki wa kisasa, Sekta ya uchimbaji madini, Sekta ya utalii na ukarimu, Usafirishaji, ufugaji wa nyuki na usindikaji wa asali.
Fursa nyingine ni pamoja na Michezo na burudani, pia kuwekeza katika huduma za jamii kama Haspitali, Shule, Vyuo vya elimu ya Juu na Ufundi. Hizo ni Baadhi ya fursa na sekta ambazo zinapatikana mkoani Kagera katika sekta ya uwekezaji.
Aidha fursa za kuwekeza haraka ambazo zipo tayari kwa sasa ni Kilimo cha mahindi  na mpunga katika Bonde la mto Ngono Wilayani missenyi, Ujenzi wa nyumba za kisasa katika manispaa ya Bukoba, Ujenzi wa Bandari ya kisasa Rwagati Kemondo Wilaya ya Bukoba, na Ufugaji wa kisasa wa  Samaki Ruhanga Wilayani Muleba.
Balozi Lu baada ya kusikiliza maeneo ya uwekezaji alisema kuwa  mkoa wa Kagera ni sehemu nzuri sana ya kuwekeza na kuinua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla pia alisema Tanzania kwa inahitaji soko la bidhaa zake ili iweze kupiga hatua katika uchumi.
Balozi Lu alisema atahakikisha kuwa anawashawishi wawekezaji toka nchini China wanakuja kuwekeza katika sekta mbalimbali hasa kwenye mkoa wa Kagera. Pia alisema kuwa mkoa wa Kagera umebarikiwa fursa nyingi za uwekezaji kuliko mikoa mingi ya Tanzania
“Mwezi  Juni 2014 Nchi ya China itafanya mkutano mkubwa wa uwekezaji nchini Tanzania na Mkutano huo unatarajiwa kuwa na wafanyabiashara wapatao 100 kutoka China kwa hiyo nitahakikisha mkoa wa Kagera unashiriki  na nitawashawishi wawekezaji hao kukubali kuwekeza  mkoni Kagera.” Alisema Balozi Lu.
Katika hatua nyingine Balozi Lu alihaidi kuwashawishi na kuwaalika wafanyabiashara wa Kichina Kuja kushiriki katika maonyesho ya Saba Saba na Nane Nane mwaka huu  2014 Mkoani Kagera ili kuweka ushindani na kubadilishana ujuzi wa biashara kati ya China na Mkoa wa Kagera.
“Tutayafanya yote hayo ili kuinua uchumi wa wananchi wa mkoa wa Kagera kwasababu Tanzania ina urafiki mkubwa na Nchi ya China zaidi ya Miaka 50 iliyopita na rafiki wa kweli ni Yule akusaidiaye kwenye shida, tutashirikiana kuwekeza na kutafuta masoko ya bidhaa za mkoa wa Kagera na Tanzania kwa ujumla .” Alimalizia Balozi Lu.
Waandishi wa habari Wakiwajibika Kupata Habari kwa Balozi Lu Youqing.

Imeandaliwa na:
Sylvester Raphael
AFISA HABARI
RS-KAGERA@2014


Next Post Previous Post
Bukobawadau