Bukobawadau

KAMA TUNAUTETEA NA KUULINDA MUUNGANO TUSIUCHOKONOE

Na Prudence Karugendo
MNYUKANO  unaoendelea kwa sasa katika Bunge Maalumu la Katiba ni wa muundo wa Muungano wa Tanzania. Ni katika mjadala wa serikali mbili dhidi ya serikali tatu kama zilivyopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba Mpya.
Mnyukano huo umefikia kuwafanya UKAWA, Umoja wa Katiba ya Wananchi, kususia vikao vya Bunge Maalumu. Hilo tuliache kwanza, tuangalie mjadala unavyoendelea.
Baadhi ya wajumbe wanaonekana kuijadili Rasimu ya Katiba Mpya wakiwa wameiweka pembeni kabisa dhima iliyopewa tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakionekana kutoelewa sababu yoyote iliyosukuma mpaka Tume hiyo ikaundwa na rais. Wanachokizingatia ni kwamba wao ni wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba basi. Wanajifanya kutokuwa na uelewa wowote wa kwamba Bunge hilo ni matokeo ya uwepo wa Tume hiyo wanayoikashfu!
Wajumbe hao, ambao wengi wanadai wanawasemea  wananchi ilhali wakielewa kwamba hawajachaguliwa na wananchi kwa ajili ya kazi hiyo, wanaonekana kulazimisha mawazo yao ndiyo yaingizwe kwenye Katiba ya nchi yetu, hasa muundo wa serikali mbili, kitu ambacho hakimo kweye Rasimu,  tena kikiwa ndicho moja ya sababu kubwa za kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Wajumbe hao wanaotetea muundo wa serikali mbili katika Muungano wa Tanzania wanadai lengo lao ni kuulinda Muungano huo. Sina hakika na madai yao hayo. Kinachonikosesha uhakika huo ni hoja wanazozitoa zilizojaa mapengo.
Mapengo katika hoja zao nayaona kupitia katika misimamo yao wanayoionyesha kwamba ni ya kuulinda Muungano huku kauli zao zikionekana sumu kali kwa Muungano huo.
Ni kwamba Tanganyika na Zanzibar zilipoungana mwaka 1964, baadaye kidogo lilibuniwa jina linalofaa kwa muungano huo, jina hilo ni Tanzania, ikawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yakiwa yameunganishwa majina ya Tanganyika na Zanzibar.
Baada ya hapo yakaja majina mawili ya Bara na Visiwani ili kutofautisha ni sehemu gani ya muungano inayolengwa. Hiyo ni kwa sababu kutajwa Tanganyika kulionekana ni kuuchokonoa Muungano kama ilivyokuwa kwa kuitaja Zanzibar.
Lakini baadaye ikaanza kutajwa Zanzibar na Tanzania Bara, kitu ambacho ni kosa kubwa kwa ustawi wa Muungano wa Tanzania. Sababu ukishataja Zanzibar kinachobaki ni Tanganyika wala sio Tanzania Bara. Tukumbuke kwamba hakukuwepo kitu kinachoitwa Tanzania Bara kabla ya Muungano. Hakikuwahi kuwepo na hakina maana yoyote nje ya Muungano.
Mazoea hayo ya kuuchokonoa Muungano yameendelea mpaka leo, hata wanaodai wanautetea Muungano wanaitumia njia hiyohiyo ya kuuchokonoa, eti Tanzania Bara na Zanzibar! Kana kwamba huku Tanganyika nako kulikuwepo na sehemu inayoitwa Zanzibar. Hiyo ni sumu kubwa katika Muungano huo.
Kwa kulishadidia hilo la kuungana, hebu tuzitazame mila za Kiafrika. Katika tamaduni za Kiafrika mwanamke anayeolewa akang’ang’ania kutumia jina lake la ukoo ni lazima aonekane hana nia njema na ndoa yake. Hiyo ni kwa sababu mahari inayotolewa na upande wa mume, pamoja na mambo mengine, ni gharama ya kubadilisha ubini wa anayeolewa.
Hata kwa wazungu iko hivyohivyo, anayeolewa anaitwa Mrs. fulani, ubini wa alikoolewa.
Kwahiyo mwanamke aliyeolewa kwa kutolewa mahari kuendelea kung’ang’ania ubini wake ni kuitia ndoa yake kwenye misukosuko isiyo ya lazima. Tofauti iko kwenye tamaduni za Kiarabu ambako mahari inaliwa na anayeolewa.
Mfano, hapa kwetu mama mmoja aliolewa akaachana na jina la ubini wake, akaanza kutumia jina la ukoo wa alikoolewa. Hata baada ya kuachana na mumewe bado anaendelea kutumia jina la ukoo wa alikoolewa.
Ni mtu aliyejiendeleza kibiashara na kupata umaarufu mkubwa kitaifa na kimataifa, akiwa analitumia jina hilo kama alama ya biashara (Trade mark).
Kwa maana hiyo, ni kwamba jina lina maana kubwa, iwe katika kuungana au kibiashara. Kulichokonoachokonoa ni kuingiza mitafaruko kwenye muungano au kwenye biashara husika.
Ndiyo maana nawashangaa wanaodai wanaulinda na kuutetea Muungano kuona hawalioni kosa hilo. Wao wamekomalia Tanzania Bara na Zanzibar bila kujali kwamba tayari majina hayo yanauvunja Muungano. Ni lazima walio makini waulize maana ya neno Tanzania wanapoiona Zanzibar ikiwa pembeni.
Utasemaje unakilinda kitu unachokichokonoa makusudi kuona kama kitaanguka au kubaki kimesimama?
Katika uchangiaji kuhusu muundo wa Muungano, katika Bunge Maalumu,  wapo wachangiaji wanaojidhihirisha wazi kwamba hawakielewi wanachokifanya. Mfano mtu anapewa dakika 10 za kuchangia, anatumia dakika 8 au 9 kuwasakama wapinzani na kuitukana Chadema matusi ya nguoni. Dakika 1 au 2 anamalizia kwa kusema sera ya CCM ni serikali 2, kamaliza!
Kweli tutegemee kupata Katiba bora kwa michango ya mawazo ya aina hiyo?
Mwingine anadai serikali 2 ni mhimu kwa vile watu wa Zanzibar na Tanzania Bara wamezoeana na wanaoleana kwa muda mrefu! Huyo anachokiona katika serikali mbili ni hicho!
Mwingine atasema watu wa Zanzibar na Tanzania Bara wamezoea kufanya biashara pamoja. Hata rais alisema kitu cha aina hiyo, kwamba alikwenda mahali, mkoa mmojawapo wa Bara, akaambiwa mashamba anayoyaona ya vitunguu ni ya Wapemba!
Nasema baadhi ya wajumbe, hasa walio makada wa chama tawala, wanaonekana hawakielewi wanachokifanya. Maana wanashindwa kutofautisha Bunge Maalumu la Katiba na kikao maalumu cha chama chao! Mawazo yao yanajionyesha yanavyorudi nyuma zaidi ya miaka 25 iliyopita wakati chama chao kilipokuwa kimeshika hatamu za kila kitu kikiipeleka nchi kama farasi asiyejua anakoelekea, kibaya zaidi kikishindwa kumpa farasi huyo  walau dakika moja ya kunywa maji!
Wajumbe wa aina hiyo hawakumbuki kuwa chama chao kinao wanachama wasiofikia hata milioni 5, wakati wanachama hai, kwa maana ya wanaofuata kanuni zote za chama, hawazidi laki 5, wakati suala linaloshughulikiwa ndani ya Bunge Maalumu likiwa linawahusu wananchi wote wa Tanzania wanaokaribia milioni 50!
Kwahiyo kutojivua ukada wa chama wakati wa kuandika Katiba ya nchi ni tatizo kubwa sana. Ni tatizo linalotishia upatikanaji wa Katiba yenyewe pamoja na mustakabali wa nchi kwa ujumla. Ni suala la vizazi vilivyopo kutovitendea haki vizazi vijavyo.
Mambo ya kuzoeana na kuoleana kati ya Wazanzibari na Watanzania Bara, kama yanavyoelezwa na baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu, yanaingilianaje na suala la Katiba ya nchi? Au tuseme serikali tatu zinawezaje kuliondoa jambo hilo?
Hata kama ni nje ya Muungano kitu hicho kinawezaje kutoweka? Mbona Watanzania wanazoeana na hata kuoleana na Wakenya, Waganda, Warundi na hata Wanyarwanda? Ina maana wote hao wanashawishiwa na muundo wa muungano wa serikali 2 wa Tanzania?
Ieleweke kwamba Watanzania, kibinafsi, wamezoeana na hata kuoleana na watu wa mataifa ya mbali katika mabala kama Ulaya, Marekani, Asia na kwingineko, bila kuathiriwa na muundo wa serikali yao. Kwahiyo wanaotaka kuliingiza hilo katika muundo wa serikali linapokuja  suala la Muungano wa Tanzania waelewe wana yao mambo, kwa kulielewa jambo hilo au kwa kuburuzwa tu.
Wengine wanajenga hoja kwamba serikali tatu zitaongeza gharama za uendeshaji wa serikali hizo. Hao wanajifanya wanayajali sana matumizi ya serikali! Lakini wakichunguzwa vizuri si ajabu watu hao wakakutwa ndio haohao waliokuwa wanadai kwamba shilingi laki tatu kutwa kwa kila mjumbe wa Bunge Maalumu ni kidogo sana!
Sasa wanaposema gharama za uendeshaji wa serikali tatu zitakuwa kubwa sana ni kweli wanakimaanisha wanachokisema?
Kuhusu Wapemba kuwa na biashara Bara kunaingilianaje na serikali 3? Kwani wapo watu wa mataifa mangapi waliowekeza hapa kwetu Tanzania? Je, hao nao wanavutiwa na muundo wa serikali 2 katika Muungano wa Tanzania?
Mwisho kabisa yatubidi tuelewe kwamba taifa kubwa, lenye nguvu kubwa sana na uchumi imara sana dunaini, Marekani au “United States of America”, lina Muungano wa serikali 51.
Nchi, ambazo kwa sasa yanaitwa majimbo, 50 ziliungana, na kila jimbo likiwa na uchumi ulio imara kuzidi uchumi wa Tanzania kwa mbali. Juu ya serikali hizo 50 kuna serikali kuu inayoifanya idadi ya serikali za nchi hiyo kuwa 51.
Ni kitu gani kimeishaharibika kutokana na muundo wa muungano huo ulio na umri wa zaidi ya miaka 200? Kwa nini sisi tunapoangalia upya muundo wa muungano wetu tusivutiwe na muundo huo wa Muungano wa Marekani?
Kwa nini tuvutiwe tu na utajiri wa muundo huo huku tukijijengea uhalali wa kwenda kila mara kuomba misaada, tukijifanya vipofu bila kuangalia na kujifunza mbinu walizozitumia wenzetu kuwa imara kiuchumi kama hivi walivyo?
Marekani wanazo serikali 51 na ni matajiri kupindukia, katika Tanzania wapo wanaodai kwamba serikali 3 zitakuwa mzigo,  hatuziwezi! Je, hao wajumbe wenye madai ya aina hiyo wanakielewa wanachokifanya?
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau