Bukobawadau

MUUNGANO WA SERIKALI MBILI NI ENDELEVU KISHERIA NA KISIASA

Ndugu zangu,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Maoni ya Wananchi
Rasimu ya Katiba imeandikwa kwa kuzingatia na kuongozwa na maoni ya wananchi, ambayo yamechambuliwa na kupewa tafsiri kwa makubaliano ya pamoja ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Naamini kwamba, hadi Tume inafikia makubaliano ya nini kiwekwe kwenye Rasimu ya Katiba na nini kiachwe, ulikuwepo mchuano mkali wa kubishanisha fikra ndani Tume. Hivyo basi, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inastahili kila aina ya pongezi kwa kufanikisha kazi hii kubwa, nzuri na ya maana sana kwa Tanzania yetu. Mwenyezi Mungu akulipeni kheri na baraka. Pia nitumie fursa hii kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa busara wa kuiunda Tume hii.
Kila Kazi Ina Mapungufu
Hakuna kazi isiyokuwa na mapungufu isipokuwa kazi za Mwenyezi Mungu tu. Katika kujadili mapungufu au mazuri katika ya kazi za wenzetu tujadili hoja katika kazi hizo na tujiepushe kabisa kuwajadili watu wanaohusika, kwa namna moja ama nyingine, katika mchakato wa kuziandaa kazi hizo. Kuwajadili watu hawa ni kuupeleka mjadala ndiko siko; ni ukosefu wa hoja ya kujibu hoja iliyoko mbele yako. Na matokeo yake ni kejeli, matusi na kutunishiana misuli.
Rasimu ya Katiba si msahafu kutoka kwa Mola Mwenyezi kwamba ni haramu kubadilishwa hata herufi moja. Rasimu ya Katiba, kama kazi nyinginezo za wanadamu, inayo mapungufu yake, kwa mfano, INAUZIKA UJAMAA. Lakini pia inayo mambo mengi mazuri sana, kwa mfano, MIIKO YA UONGOZI. Mapungufu haya ni lazima yajadiliwe. Kuzuia kuyadili mapungufu yaliyoko katika Rasimu ya Katiba si jambo la hekima. 
Misingi ya Mjadala-shirikishi na Endelevu
Ili mjadala wowote ufanikiwe katika mawasiliano shirikishi, washiriki ni lazima wafuate misingi ya KUHESHIMIANA, KUSIKILIZANA, KUSTAHIMILIANA na ADABU zake. Kwamba kila mchangiaji katika mjadala bila kujali itikadi, dini, rangi, jinsia, umri n.k anayo nafasi ya kutoa maoni yake bila woga, akasikilizwa, na hoja yake ikakoselewa kwa hoja na si kwa kumrushia matusi ya nguoni mtoa hoja; au hoja ikaungwa mkono na kupongezwa kwa amani. Mjadala unaofuata misingi hii siku zote huzaa matunda mema kwa washiriki.
Katika kulijadili jambo, ingawa kila mshiriki anakuwa na mtizamo wake, washiriki huanza kwa kuiangalia hoja inayowaunganisha wote -- kwa maana wote wanakubaliana au wana mtizamo sawa katika hoja hiyo. Kuanzia hapo hoja nyingine hujengwa juu ya hoja hiyo tena kwa mchuano mkali na hatimaye washiriki hufikia makubaliano -- kwa maana ya KUKUBALI-KUKUBALIANA, mkasonga mbele na kufikia muafaka-endelevu; au KUKUBALI-KUTOKUKUBALIANA, mkatofautina na mkabaki mlipo au hata kurudi nyuma zaidi kwa kuibua tofauti nyingi na kuwekeana kila aina ya vipingamizi.
Mjadala wa Serikali Moja/Mbili/Tatu/Mkataba
Katika kuijadili Rasimu ya Katiba kuhusu suala la serikali moja au mbili au tatu tuanzie na hoja inayokubalika kwa wote: Kwamba tunaupenda Muungano wetu na tutaudumisha. Kwamba Tanzania ni nchi moja yenye serikali mbili ambazo ni matokeo ya kuungana kwa nchi mbili huru (kwa maana ya dola huru) za Tanganyika na Zanzibar kwa hiari. Kwamba Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar katika nchi ya Tanzania zina mipaka yake inayojulikana. Kwamba sababu walizozitoa waasisi wa Muungano huu za kuwa na muundo wa serikali mbili katika Muungano ili kuepuka kuimeza Zanzibar na pia kupunguza gharama za uendeshaji kuwa kubwa hasa kwa Tanzania Bara (Rejea Hotuba ya Mwalimu Nyerere katika kitabu cha Nyufa), sababu hizi bado zina mashiko na ni mwongozo mwema katika mjadala wetu wa sasa; kwa hiyo ni jambo la busara sababu hizi zikafuatwa. Hapa ndipo pa kuanzia. Kukubali-kukubaliana katika hoja hizi hakumaanishi kwamba wale wanaotetea serikali mbili wameshinda, na wale watetezi wa serikali moja/tatu au muungano wa mkataba wameshindwa. La hasha! Bali ni kukubaliana na hali halisi ilivyo. Kwa mfano, suala la kila sehemu ya Muungano kuwa na mipaka yake inayojulikana si jambo baya ila tatizo linaibuka unaposema, ‘Zanzibar ni nchi yenye dola huru,’ kwa kutumia kigezo cha kuwa na mipaka yake. Zanzibar itakuwaje NCHI YENYE DOLA HURU, KWA MAANA HALISI YA NENO SOVERIGN STATE, ili hali iliishajivua hadhi hiyo na kuwa sehemu ya NCHI YENYE DOLA HURU ya TANZANIA kama Tanganyika ilivyofanya? Mipaka inayojulikana kimataifa ni ya Tanzania na si ya Tanganyika au Zanzibar. Katika hili la mipaka utaiona faida ya Muungano kwa wepesi kwani ni rahisi kwetu kuwa na mpaka mmoja wa kimataifa katika Bahari ya Hindi kuliko nje ya Muungano. Pia jiografia inaufanya Muungano wetu kuwa ni wa asili kwani ni rahisi kwa mkazi wa Pemba kusafiri kwenda Tanga kuliko kwenda Unguja. Vivyo hivyo kwa Unguja na Bagamoyo. Kama busara itatumika, hoja iko wazi kwamba Zanzibar ni sehemu ya Tanzania yenye mamlaka yake ya ndani kwa maana ya NCHI NDANI YA NCHI (AUTONOMOUS REGION) – kwa mujibu wa Katiba ya Muungano na si vinginevyo. Na Muungano upi huo MKATABA? Kwani huu Muungano uliopo si wa mkataba? Kwani Hati ya Muungano si MKATABA (au Hati hii ilitokana na nini)? Mkataba upi mnaoutaka? Mkataba wa Zanzibar kama dola huru? Kama msimamo utashikiriwa wa Zanzibar ni NCHI KAMILI YENYE DOLA HURU kwa sababu na maslahi ya watu binafsi na si kwa maslahi nchi ya Tanzania basi tujue wazi kabisa kwamba Katiba mpya haitapatikana mpaka Tanganyika nayo imekuwa nchi kama Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilivyopendekeza. Na kwa kuirejesha Tanganyika kama nchi yenye dola huru tutakuwa tunarudi kabla ya tarehe 26 Aprili 1964. Na hapo HAKUNA Muungano! Nitafafanua.
SERIKALI TATU NCHI TATU NI JAMBO AMBALO LINAWEZEKANA KISHERIA LAKINI SI JAMBO ENDELEVU KISIASA.
Kwa kuwa jambo hili si endelevu kisiasa basi halitufai. Kisheria utakuwa na Marais watatu wenye mamlaka juu vyombo vya dola. Marais watu wenye majeshi na wakiwa na mamlaka ya kutangaza hali ya hatari. Kisheria jambo la Rais nchi ya Tanganyika au Zanzibar kuwa amri jeshi mkuu wa nchi yake ndani ya Muungano linaonekana kuwa liko sawa lakini kisiasa halifai. Hebu fikiria itakuwa vipi Rais wa Tanganyika akaamua kujitangazia hali ya hatari na yule wa Muungano na wa Zanzibar wakataa? Na hapa ikumbukwe kuwa Marais hawa watatu wanaweza kuwa wanatokea vyama tofauti vya siasa vyenye misimamo tofauti kabisa – hawapikiki chungu kimoja. Au wawili wao wakiwa wanatoka chama kimoja cha siasa na wakajenga genge la kumtenga Rais mwenzao. Iko hatari kubwa sana hapa. Tutajikuta tuko chini ya wababe wa kivita. Serikali ya Muungano katika mfumo huu itakuwa haina vyanzo vya mapato. Na huwezi kutoa suluhisho la tatizo la mapato kwa kuesema kwamba ‘kodi ya bandari inatosha kuendesha serikali ya Muungano.’ Haya ni mapungufu makubwa sana katika utoaji hoja kwani mapato ya bandari yanaweza kuwa pungufu katika mwaka fulani na kuiach serikali ya Muungano ikiwa na naksi. Nani ataipatia pesa ya kujiendesha? Na kama kuna tofauti za kisiasa kati ya marais watatu bila shaka itakuwa vigumu sana kwa serikali ya Muungano kupata mapato ya uhakika. Matokeo yake itashindwa kujiendesha na ofisi za Muungano zitafungwa na Muungano utavunjika. Tuwe makini sana. Tusifuate hisia na haja binafsi bali tuongozwe na uhalisia wa mambo na ukweli wa hoja iliyo wazi kwamba nchi (dola huru) ni Tanzania yenye serikali mbili -- Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Mgogoro wa Kikatiba uliopo sasa kwamba Baraza la Wawakilishi linaweza kuiikataa sheria ya Bunge la Muungano ni mfano mdogo tu wa utata mkubwa wa kisheria na kisiasa utakaoibuka baada ya kuwa serikali tatu na nchi tatu.
Katika muundo wa serikali tatu, wenye serikali za Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika, zenye dola huru na mamlaka kamili kama taifa-nchi, hakuna Jamhuri ya Muungano hapo kwa maana ya taifa-nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali kutakuwa na Shirikisho la Jamhuri za Tanzania au Jumuiya ya Jamhuri za Tanzania zenye mkataba wa kushirikiana kisiasa, kiuchumi, kiulinzi na kijamii pale inapobidi. Hatuwezi kuwa taifa-nchi moja ili hali tuna utambulisho tofauti kimatiafa -- kila mmoja akiwa na kiti chake Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na kwingineko. Hatuwezi kuwa taifa-nchi moja ili hali kila mmoja ana mahusiano yake kimataifa na sera zake za nje. Hatuwezi kuwa taifa-nchi moja Tanganyika na Zanzibar zina marais wasiowajibika kwa Rais wa Muungano kwani watakuwa wanaongoza mataifa-nchi yenye dola kamili. Hatuwezi kuwa taifa-nchi moja kwa kuanzisha, kurasimisha na kuhalalisha, tena kwa makusidi kabisa ukabila na ubaguzi katika Katiba. Kwamba “wao watanganyika, sisi wazanzibari.” Kwa kufuata muundo wa serikali tatu tutakuwa temeanzisha rasmi mchakato wa kuiuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ambavyo Rasimu ya Katiba inavyouzika Ujamaa.
Zanzibar na OIC
Inasikitisha kusikia kwamba miongoni mwa hoja za kuwa na muundo wa serikali tatu ni kuipa Zanzibar uhuru wa kujiunga na OIC kwamba itaneemeka. Hoja hii haina mashiko. Hakuna uhusiano wala ushahidi wowote kati ya nchi fulani kuneemeka eti kwa kuwa ni mwanachama wa OIC. Somalia ingekuwa ya kwanza kupatiwa misaada ya kila hali na mali kuondoa vita na umaskini lakini nani katika OIC kaisaidia Somalia? Mpaka leo wanapigana na kuuwana. Nchi wanachama wa OIC nyingi ni tajiri sana na ni pua na mdomo na Somalia lakini hazijawahi kuwa mstari wa mbele kuisaidia Somalia ipate amani. Kumbe kuwa OIC si suluhisho la matatizo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa nchi wananchama. Pia tukumbuke kwamba katika nchi hizi OIC za mashariki ya kati moto unawaka. Kila uchao watu wanachinjana. Je, watakuja kuisaidia ya Zanzibar ili kwao kunabomoka? Na hali hii ya ukosefu wa amani na utulivu katika nchi hizi kwa jinsi mambo yalivyo haishi leo wala kesho. Kwa hiyo suluhisho la umasikini wa watu wa Zanzibar ni watu wenyewe, uongozi bora na siasa safi na kuzitumia raslimali zilizopo kuondoa umasikini na si kutegemea kwamba OIC itakuja kuuondoa. Fikira hizi za kutegemea misaada hazijengi. Ni fikira za kudumaza ustawi na kudumisha utegemezi na ukoloni. Mtegemea cha nduguye hufa ili hali masikini, wahenga walisema. Na hata kama Zanzibar itapata misaada ya OIC na Tanzania Bara je, hakuna waislamu? Wapo. Pili Zanzibar inaweza kupata misaada kutoka nchi za OIC bila kuwa mwanachama. Hili linaweza kufanywa na kufanikiwa ikiwa viongozi watafanya jitihada za kuitafuta misaada hiyo na kuifikisha kwa walengwa.
Muundo Upi wa Muungano Unafaa?
Rejea Historia
Busara itumike sana katika kuangalia muundo wa Muungano. Ni muundo upi unatufaa kama Tanzania? Tukirejea katika historia tunazikuta sababu nzuri ya kuwa serikali mbili ambazo zinamashiko mpaka leo hii (kama nilivyosema hapo juu). Mojawapo ni kutokumezwa kwa Zanzibar. Naamini hali ingekuwa ngumu sana sasa kama Muungano wetu ungekuwa serikali moja. Wale wanaosema Zanzibar ni koloni kwa hakika hoja yao ingekuwa moto wa kuotea mbali. Serikali tatu jibu lake ni hakuna Muungano bali Jumuiya tu. Katika kuimarisha Muungano tulikuwa na Rais wa Muungano akisimamia shughuli zote za Muungano na Tanzania Bara (Tanganyika). Pia tulikuwa na Makamu wa Rais wawili -- Rais wa Tanzania Zanzibar na Waziri Mkuu katika serikali ya Muungano na Tanzania Bara. Ulikuwa ni muundo mzuri kabisa. Rais wa Muungano alikuwa na mamlaka juu ya Rais wa Zanzibar kwani huyu alikuwa ni Makamu wake wa Kwanza au wa Pili. Pili Rais wa Zanzibar alikuwa na hadhi yake kamili katika Muungano. Tatu Waziri Mkuu alikuwa na hadhi yake kama Makamu wa Rais Muungano huko Tanzania Zanzibar. Ni kweli kuna wakati fulani Rais wa Zanzibar ndiye alikuwa Makamu Rais pekee yake lakini hili halikumuondolea hadhi Waziri Mkuu huko Zanzibar (Rejea wakati Aboud Jumbe akiwa Makamu wa Rais).  Muungano ulikuwa imara. Ni kutokana na uimara huu ndio maana Muungano hakuvunjika mwaka 1984. Pia ulikuwepo wakati Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wote walitokea Zanzibar (Rejea wakati Alli Hassan Mwinyi akiwa Rais wa Zanzibar na Dr. Salim Ahmed Salim akiwa Waziri Mkuu). Utaifa huu umeishia wapi?
            Madhara ya G55 kwa Muundo wa Uongozi wa Muungano
Katika muundo wa sasa wa uongozi wa serikali ya Muungano uliojitokeza baada ya vuguvugu la G55 la kuidai Tanganyika, Zanzibar kutaka kujiunga na OIC na kuelekea kwenye uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi wa 1995, Rais wa Zanzibar si Makamu wa Rais katika serikali ya Muungano, hivyo basi hana sauti katika serikali ya Muungano. Pia Waziri Mkuu wa Tanzania hana sauti yeyote Zanzibar. Matokeo yake hadhi ya viongozi hao ipo tu kwa sababu ni watu wanaotoka chama kimoja na si vinginevyo. Matokeo yake Rais wa Zanzibar hawajibiki kwa Rais wa Muungano. Atawajibika kwake kama nani? Siyo Makamu wake. Ndiyo maana hata utaratibu wa kuteuliwa wakuu mikoa ya Zanzibar kwa Rais wa Zanzibar kushauriana na Rais wa Muungano unafutwa na Katiba ya Katiba ya Zanzibar ingawa hii ni kinyume na Katiba ya Muungano. Kumbe ikitokea ‘Kuchafuka kwa Hali ya Hewa Zanzibar’ kama ilivyokuwa mwaka 1984 hakuna mwenye mamlaka ya kumzuia Rais wa Zanzibar kuuvunjwa Muungano. Hayupo. Labda kupitia vikao vya vyama vya siasa ambavyo haivitakuwa na nguvu tena hali hiyo ikijitokeza. Pia kwa Makamu wa Rais wa Muungano na Waziri Mkuu wa Muungano ukiuliza wana mamlaka gani kule Zanzibar ni vigumu kupata jibu. Hawana sauti. Wanaheshimika tu kiungwana. Kumbe katika kumdhibiti Rais wa Zanzibar mwaka 1994, G55 ilituachia muundo wa kiuongozi wa serikali ya Muungano unaoendeshwa kiungwana tu. Jambo hili ni kikwazo kikubwa sana kwa uhai wa Muungano wa serikali mbili nchi moja. Huu ndiyo ukweli na tulisahihishe. 
            Mabadiliko ya Katiba Zanzibar 2010
Mabadiliko ya Katiba Zanzibar ya 2010 ambayo yanasema Zanzibar ni nchi (dola huru), ingawa yanaonekana ni ukombozi wa kuipa Zanzibar hadhi ya nchi, lakini yako kinyume kabisa na Katiba ya Muungano. Ni kinyume na tamko kwamba nchi za Tanganyika na Zanzibar ziliungana kuunda nchi moja iitwayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kimsingi kwa mabadiliko haya Katiba ya Zanzibar iko juu ya Katiba ya Muungano. Kwamba sheria zikitungwa na Bunge la Muungano ambalo lina wabunge kutoka Zanzibar lazima ziidhinishwe na Baraza la Wawakilishi ili ziweze kutumika Zanzibar. Iko wapi nchi moja hapo ya Tanzania? Au Baraza la Wawakilishi ni Bunge la Seneti la Muungano? La kusikitisha wakati mabadiliko haya yanafanyika hakuna aliyeyakemea. Matokeo yake sasa ni hiki kizungumkuti kilichopo.
Kwa kuwa yalifanyika makosa haya basi tusiyatumie pamoja na kero zilizopo kuhusu Muungano kujenga hoja za kuleta muundo wa serikali tatu ambao kimsingi utakuwa mbovu zaidi ya ubovu uliopo katika muundo huu wa sasa. Kazi iliyoko mbele yetu ni kusahihisha makosa yote haya kwa maridhiano ya kukubali kukubaliana.
            Dhana Potofu Kuhusu Muungano
Katika kujadili muundo wa Muungano tusisahau kwamba katika miaka 50 ya Muungano yamekuwepo makosa mengi yaliyofanywa  ambayo yamesababisha chuki dhidi ya Muungano. Yamefanyika mabadiliko mbalimbali ya Katiba na sheria ili kukidhi haja binafsi za baadhi ya viongozi. Makosa haya yasitumike kupandikiza mbegu ya kuuvunja Muungano kwa kuchochea muundo wa serikali tatu. Pia Muungano umezushiwa dhana nyingi potofu zinazolenga kuuvunja. Ipo dhana kwamba Muungano ni matokeo ya kazi za kijasusi za wamarekani kwa kumtumia Mwalimu kuimeza Zanzibar; kwamba mchakato wa kuanzishwa Muungano ulikwenda haraka mno tena bila ya ushauri na hivyo basi Muungano si halali. Ufe. Uzikwe. Usahaulike. Dhana nyingine inasema kama Nyerere angelikuwa kweli anaupenda Muungano wa Afrika basi angemshauri rafiki yake Kenneth Kahunda ili Zambia nayo iingie kwenye Muungano wetu. Dhana hii nayo inahitimisha kwa kushadidia kwamba hatima ya Muungano wa Tanzania ni kuvunjika kama ulivyovunjika muungano wa Ghana na Guinea, au ule Senegal na Gambia. Hata Muungano wa Uingereza nao uko kwenye hati hati ya kuvujika kwani Uskoti (Scotland) inataka kujietenga. Pia ipo dhana kwamba madhumuni ya waasisi wa Muungano yalikuwa ni serikali tatu. Kwa hiyo serikali tatu zinarudi kwenye mzizi wa madhumuni ya Muungano. Dhana hizi zote msingi wake mkubwa ni kupandikiza chuki dhidi ya Muungano. Na hoja zake hazilengi kuijenga Tanzania imara bali zinalenga kuiangamiza kwa kuuvunja Muungano wetu.
            Kero za Muungano
Kero za Muungano zimekuwa zikitajwa kama mapungufu katika Muungano. ‘Kero za Muungano’ zisiwe chachu ya kukimbilia muundo wa serikali ya mkataba au tatu kwa kuanzisha serikali na nchi ya Tanganyika bali ziwe ni nyenzo za kutusaidia kutafuta dawa mujarabu ya kero hizo. Tusahihishe. Tuboreshe. Tusivunje. Kero zote zinazungumzika na zina dawa mujarabu kama nia ya dhati ya kuulinda Muungano ipo. Kiimsingi kuundwa kwa serikali tatu, kutokana na utata unaozunguka mapendekezo hayo tena kwa mujibu wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, kutauvunja Muungano. Na matokeo yake ni kero kubwa zaidi ya “sisi na wao.”
Mjadala Bungeni Ulenge Kujenga na Si Kubomoa
Katika kuamua ni muundo upi Muungano tuufuate, Bunge la Katiba, lifikirie kwa busara na mapana sana, tena kwa maslahi ya nchi yetu Tanzania na si kwa maslahi ya vyama vya siasa au kundi la watu fulani. Kama maamuzi yatachuliwa ya kulinda maslahi binafsi baadala ya maslahi ya Tanzania tutajikuta tunauvunja Muungano. Kwa hiyo, umefika wa wakati sasa wananchi, vyama vya siasa na asasi za makundi mbalimbali na wabunge wa bunge la Katiba kukubali kukubaliana kwamba muundo muafaka utakaodumisha Muungano ni muundo wa serikali mbili. Nje ya serikali mbili au ndani ya serikali tatu kuna “sisi ni watanganyika wao ni wazanzibari.” Tutakapoanza kuitana “sisi na wao” hakuna Muungano hapo. Kikatiba na kisheria mtajiita Watanganyika na Wazanzibari lakini kisiasa mtakuwa mmevunja UTANZANIA NA UDUGU UTOKANAO NA UTANZANIA HUO. Ubaguzi huu hautaishia hapo, utaitafuna Tanganyika na Zanzibar milele. Hatutasalimika. Utaifa utakufa na ukabila utatawala – “Wazanzibari na Wazanzibara”. (Rejea Hotuba ya Mwalimu Nyerere ya Nyufa).
Sasa nini kifanyike ili kuleta makubaliano ya kukubali-kukubaliana katika mjadala wa Bunge la Katiba kuhusu muundo Muungano wa serikali mbili ?
1.     Heshima na kuthamini utu ni vitu adhimu sana hivyo basi uwepo wa nidhamu, hekima, busara na umakini katika kujadili Rasimu ya Katiba katika Bunge utaliwezesha Bunge kufikia makubaliano. Uzalendo na nia ya dhati ya kupata Katiba nzuri viwe muongozo mkuu. Kwamba wabunge wajiepushe na kutumia lugha chafu ya matusi, kejeli na vitisho kwani kwa kufanya hivyo mtakuwa mnaubomoa upendo, umoja na udugu wetu na mnajenga hasira, chuki na uhasama. Katiba bora haitapatika kupitia hali ya uhasama na kutokuaminiana iliyopo kwa sasa katika Bunge. Wabunge wawe na ustarabu wa kusikiliza, kushauriana, kusahihishana, kukosoana na hata kurekebishana kwa kusikilizana na si kwa kupayukiana na kutukanana na hata kutunishiana misuli kama tunavyoendelea kuona. Jazba au kupayuka si ishara ya uzalendo.
2.     Mjadala wa Rasimu ya Katiba usigeuzwe kuwa mjadala wa kujadili watu. Mtakuwa mnapoteza mwelekeo, muda na pesa za wananchi kwa kuwajadili watu. Katika kuwajadili mnaweza kujikuta mnateleza ulimi au hata kwa makusidi na kuwatukana mnaowajadili kutokana na jazba na hatimaye mkaonekana ni wachache wa adabu. Pia yako mambo mengi muhimu sana ya kujadiliwa, likiwemo suala la ITIKADI YA UJAMAA, na si muundo wa Muungano peke yake ingawa Muungano ndiyo nchi yenyewe -- Tanzania.
3.     Tanzania Zanzibar ikubali kubadilisha Katiba yake ili isipingane na Katiba ya Muungano. Tukumbuke kwamba waasisi wa Muungano waliweka MUUNDO WA NCHI MOJA, TANZANIA, YENYE SERIKALI MBILI.
4.     Kiongezewe kifungu katika Rasimu ya Katiba kwamba Tanzania iwe na Makamu wa Rais watatu. Cheo cha Makamu wa Rais anayetokana na nafasi ya Mgombea Mweza kiendelee kuwepo ili kuondoa utata wa nani atakuwa Rais endapo nafasi ya Rais itakuwa wazi kwa mujibu wa Katiba na hasa pale Makamu wa pili na watatu wa Rais wakiwa wanatokea vyama vya siasa tofauti na Rais (hili linaweza kutokea). Makamu wa Rais atokanaye na mgombea mwenza atajulikana kama Makamu wa Kwanza wa Rais.
5.     Waziri Mkuu wa Muungano na Rais wa Zanzibar wawe ni Makamu wa Rais kwa nafasi zao – Makamu wa Pili na Makamu wa Tatu. Tukifanya hivi tutakuwa tumewapa viongozi hawa hadhi yao katika serikali ya Muungano. Ukosefu wa hadhi ya viongozi hawa katika Muungano ni kikwazo kikubwa kwa Muungano imara. Pili Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa na mamlaka kwa Rais wa Zanzibar kwani atakuwa ni miongoni mwa Makamu wake.
6.     Kwa kuwa hofu kuu inaweza kuwa juu ya utata iwapo nafasi ya Rais na nafasi ya Makamu wa Rais ziinaweza kuwa wazi kwa pamoja kwa wakati mmoja kwa mujibu wa Katiba (jambo ambalo ni nadra sana kutokea ingawa linaweza kutokea) basi Katiba iweke wazi kwamba Jaji Mkuu au Spika wa Bunge atashika madaraka ya Rais katika kipindi hicho cha mpito na si Makamu pili au Makamu tatu ambao huenda wakawa wanatoka vyama tofauti na chama cha Rais na Makamu wa Kwanza wa Rais walioacha nafasi zao wazi ili kuondoa utata huo. Hii ni kwa sababu ridhaa ya wapiga kura ni kwa hao watakaokuwa wameacha nafasi.
Mapendekezo namba 4-6 yatatupa wepesi sana ikiwa tutaka kuunda serikali ya umoja wa kitaifa iliyo imara kwa maslahi ya Tanzania pale serikali zetu mbili zikuwa zikiongozwa na marais kutoka vyama tofauti vya siasa.
 
Hitimisho
Nitumie fursa hii kutoa angalizo kwamba ukipima uzito wa sababu za kuwa na nchi tatu na serikali moja/tatu na faida zake na hasara zake au muungano wa mkataba ukalinganisha muundo wa nchi moja na serikali mbili na faida zake na hasara zake unaona kwamba Muungano wa nchi moja serikali mbili unafaa na ni endelevu kisheria na kisiasa.
 
Nimalizie kwa kulikumbusha tena Bunge la Katiba umuhimu wa kufuata misingi ya kuheshimiana, kusikilizana, kustahimiliana na adabu na kuepuka matusi na kutunishiana misuli katika kuijadili Rasimu ya Katiba. Kinyume chake mtapitisha Katiba mbovu inayotoa leseni ya kuuwa Muungano. Na wananchi wataikataa. Endelezeni umakini wenu wa kujadili kila kipengele kwa kina na msikubali kushinikizwa na yeyote yule. Fanyeni kazi hii kwa maslahi ya Tanzania na watanzania.
 
Panapo uhai na uzima nitaandika kuhusu Rasimu ya Katiba kuuzika Ujamaa na athari zake kwa Tanzania, Uraia wa Nchi mbili na athari zake, na upotoshaji kuhusu maendeleo ya Tanzania ikilinganishwa na Malaysia au Korea.
 
Nakutakieni kila lenye kheri katika kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wetu.
 
Mungu Ibariki Tanzania
Dumisha Uhuru na Umoja
Dumisha Muungano wa Tanzania
 
Ndugu yenu
 
Dkt Amani Millanga
 
06/04/2014
London
 "No Choice, No Sacrifice; No Sacrifice, No Access; No Access, No Success.The Choice Should be Guided by the 6Cs of a Good Character: Conscience, Compassion, Consideration, Courage, Control & Confidence."by Amani Millanga
NAAMINI KUWA NAFSI IKITAWALIWA NA TAMAA HATA KAMA INA ELIMU KUBWA NA UTAJIRI KIASI GANI, ELIMU NA UTAJIRI HUO HAVIFANYI KAZI KWA MANUFAA YA WATU.
Next Post Previous Post
Bukobawadau