Bukobawadau

KINACHOFICHWA NA UKAWA NI HIKI HAPA

Na Mchakachuaji
Kama kuna chama cha siasa kisichoeleweka malengo yake hapa nchini basi chama hicho ni CUF. Nashawishika kukifananisha chama hicho na mwanamke ambaye hajatulia, mwanamke  ambaye leo anaolewa na mwanamume huyu na kesho yake kumtamani mwanamume Yule, na akishaolewa kule kesho yake anadai talaka!  Kwa tabia ya aina hiyo ni vigumu kujenga imani kwa mwanamke huyo au kukiamini anachokikusudia katika ndoa zake hizo za pata potea.
Tunakumbuka kwamba baada ya mikwaruzano ya muda mrefu kati ya chama cha CUF na chama tawala, CCM, kwa upande wa Zanzibar, baadaye vyama hivyo vilifikia makubaliano ya kusitisha mikwaruzano kwa kitu kilichojulikana kama muafaka, na hivyo chama tawala kukubali kupunguza madaraka yake na kuigawa nusu ya madaraka hayo kwa CUF. Vyote viwili vikawa vyama tawala kwa upande huo wa muungano.
Vyama hivyo vilikubaliana kuunda kwa pamoja Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kwa maana hiyo CUF nayo ikawa chama tawala kwa upande wa Zanzibar. Kitendo cha CUF kukubali kuungana na CCM,  nacho kuhesabika kama chama tawala kina maana ya kwamba chama hicho kilikuwa kimekubaliana na sera za chama hicho tawala.
Kwahiyo kwa vile sera ya CCM ilikuwa ni kuendesha nchi ya Tanzania kwa muundo wa Muungano wa serikali mbili, Zanzibar na Tanzania, basi CUF kukubali kuungana na CCM na kuendesha nchi kwa pamoja kwa upande wa Zanzibar, tayari chama hicho cha wananchi kilikuwa kinaamini katika muundo huo wa muungano. Muungano wa serikali mbili.
Sasa katika mchakato wa kuandika katiba mpya ya nchi hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikaja na kitu kipya ilichodai ni maoni ya wananchi, Muungano wa Serikali tatu. Kwa vile Rasimu hiyo moja kwa moja inakinzana na msimamo wa utawala wa CCM ilikuwa ni lazima chama hicho tawala  kikionyeshe kitu hicho kilicho kinyume na mfumo wa uendeshaji wake wa serikali bila uficho wowote. Bila hivyo CCM ingekuwa inakubali kuwa imeiongoza nchi hii muda wote kinyume na matakwa ya wananchi.
Katika hilo nilitegemea Chama Cha Wananchi kiwe mshirika namba moja wa CCM katika kuipinga Rasimu hiyo inayopendekeza kwamba Katiba mpya itamke kwamba Serikali ya Tanzania ni muungano wa serikali tatu. Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba baada ya makubaliano ya muafaka wa kuendesha nchi kwa pamoja tayari CUF ilikuwa imekubaliana na muundo huo wa serikali mbili unaotambuliwa na CCM.
Lakini kwa mshangao wa kila mmoja, ghafla CUF ikaruka mara moja na kujiunga na vyama vingine vya upinzani vikiongozwa na Chadema,  kuunda kitu kinachoitwa UKAWA, Umoja wa Katiba ya Wananchi. Umoja huo unaunga mkono Rasimu iliyoletwa katika Bunge maalumu kwa ajili ya kujadiliwa ili baadaye  irekebishwe, kama hapanabudi,  au kupitishwa jinsi ilivyo na kuwa Katiba mpya.
Mbali na kuishangaa CUF kwa ukinyonga wake huo, bado naishangaa UKAWA kwa msimamo wake kwamba Rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapaswa iheshimiwe. Swali ni kwamba kama Rasimu hiyo inapaswa iheshimiwe kazi ya Bunge Maalumu ni nini? Si Rasimu hiyo, baada ya kuwasilishwa kwa rais, moja kwa moja ingepelekwa na kutengenezwa katiba mpya bila usumbufu wa kuitisha Bunge Maalumu.
Bunge maalumu maana yake ni kwamba Rasimu ikajadiliwe na Bunge hilo ili kama kuna mapungufu yaondolewe katika kuiboresha kabla haijawa Katiba kamili. Moja ya mapungufu yaliyojionyesha katika Rasimu hiyo ni hilo la muundo wa serikali tatu, muundo ambao vyama tawala, CCM na CUF, vilikuwa makini kabisa kuliepuka kutokana na madhara yanayotishia kutokea kufuatia serikali kuukumbatia muundo wa muungano aina hiyo.
Kwa mantiki hiyo tutaona kwamba kinachoongelewa na Ukawa kwamba Rasimu iheshimiwe hakina mashiko yoyote.
Kitendo cha CUF kutoulinda msimamo wake, kama ilivyo CCM inayoulinda wa kwake, ndicho kinachonipa wasiwasi na kunifanya nishindwe kukiamini chama hicho. Chama ambacho kwa zaidi ya miaka mitano kimeongoza nchi, kupitia kwenye maridhiano na muafaka,  bila matatizo yoyote katika muundo wa serikali mbili,  leo hii kinasema lazima katiba mpya iandikwe kwa mfumo wa serikali tatu!
Kwa msimamo huo wa kuyumbayumba wa chama hicho tunaweza kukiamini kile ambacho kimekuwa kikisemwa muda wote kuwa chama hicho kina ajenda ya siri. Si ajabu, katika usiri huo, yakajitokeza yale ya kwamba kinataka Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uvunjike ili kiweze kuirudisha hali iliyokuwepo Zanzibar kabla ya Mapinduzi Matukufu ya 1964, kwa maana ya kuurudisha utawala wa kisultani.
Muungano wa serikali tatu ni hoja iliyokuwa inashikiliwa na wapinzani. Maana ya upinzani ni kuupinga utawala uliopo madarakani hata kama upinzani huo hauna hoja zinazojitosheleza. Lakini hatutegemei chama kinachoongoza dola kijipinge chenyewe. Kwa hapa CUF ni chama tawala sio chama cha upinzani. Kitakuwaje chama cha upinzani wakati Katibu wake Mkuu, Maalimu Seifu, akiwa ni makamu wa rais wa serikali iliyoko madarakani, hata kama ni kwa upande mmoja wa muungano?
Ina maana mtu anaweza akawa madarakani halafu akawa mpinzani? Anampinga nani kama hajipingi yeye mwenyewe?
Kilichomfanya Maalimu Seif akawa makamu wa kwanza wa rais kwa upande wa Zanzibar, wakati chama tawala ni CCM, ndicho kinachonifanya niamini kwamba CCM na CUF kwa sasa ni kitu kimoja.
Sioni ajabu yoyote kwa vyama vya upinzani, mfano, Chadema, NCCR Mageuzi, DP na vinginevyo,  kutaka kuwepo na muundo wa serikali mbili, maana hayo ndiyo malengo ya upinzani. Lakini inapotokea hata chama kilicho madarakani kikajiunga na upinzani kwa madai ya kuyakataa yanayoendeshwa na utawala au kuupinga mfumo wa utawala pamoja na muundo wa serikali iliyoko madarakani,  ni lazima tuhisi kuwa kuna kinachoendelea chini ya uvungu. Hali hiyo ni lazima ilete mashaka kabla ya kuiunga mkono.
Kwahiyo tunaposema Ukawa hatunabudi kuuelewa vizuri umoja huo una lengo gani. Hatuwezi kujiridhisha tu kwamba huo ni Umoja wa katiba ya Wananchi kama wenyewe unavyojinadi, sababu katiba inayoandaliwa ni ya wananchi. Sasa kunapojitokeza kinachojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi tuelewe nini? Kuna siri gani katika kitu hicho, hasa pale umoja huo unapoonekana kushinikizwa pamoja na kuongozwa na chama kilicho Ikulu?
Watanzania tunapaswa kuongozwa na umakini katika mchakato huu unaoendelea wa kuandika Katiba mpya ya nchi yetu, vingenevyo tukiuachia upofu ndio utuongoze si ajabu hawa wanaojiita Ukawa tukashtukia wanatufanyia mazingaombwe. Tuwe macho na kikundi hiki cha UKAWA kama kweli tunaitakia nchi yaliyo mema.
Next Post Previous Post
Bukobawadau