Bukobawadau

WAJUMBE TFF WAKATAA TIMU 16

Dar es Salaam. Jaribio la kuzipandisha klabu za Mwadui na African Lyon kinyemela limegonga mwamba baada ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kugoma kuongeza timu za Ligi Kuu hadi 16 msimu ujao wa 2014/2015.
TFF ilitaka kuongeza timu hadi kufikia 16 kwa lengo la kuipoza Mwadui ambayo ilipokwa nafasi ya kucheza Ligi Kuu baada ya Stand United kupewa pointi za mezani siku ya mwisho ya Ligi Daraja la Kwanza, wakati uongozi wa African Lyon unahusishwa kuwa na uhusiano wa karibu na ‘bosi’ mmoja wa TFF.
Habari ambazo gazeti hili limezipata zinasema wajumbe hao walikataa mapendekezo ya Kamati ya Mashindano ya TFF, ambayo ilitaka msimu ujao Ligi Kuu iwe na timu 16, kwa kuziongeza timu hizo mbili zilizoshika nafasi za juu kwenye makundi yao.
Kamati hiyo pia ilikuwa ikiendesha kampeni ya kuhakikisha Ashanti United inabakizwa Ligi Kuu pamoja na Rhino Rangers na JKT Oljoro.
Hata hivyo, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF walikataa mapendekezo hayo na badala yake wakapitisha msimu wa 2015/2016 ndio ligi iwe na timu 16 badala ya 14.
“Hatuwezi kubadili kanuni baada ya msimu kumalizika, hivyo Ligi Kuu inayoanza mwezi wa nane tumeamua itabaki na timu 14 kama kawaida. Lakini msimu wa 2015/206 itakuwa na timu 16,” alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF.
“Pia tumeipa jukumu Kamati ya Mashindano ya TFF iandae marekebisho kisha watuletee na sisi tutapanga kanuni za ligi kwa ajili ya msimu ujao.
“Kuna mapendekezo kuwa msimu ujao zishuke timu mbili kisha zipande nne, na mapendekezo mengine ni kushusha timu tatu na zipande tano,” alisema mjumbe huyo.
Taarifa iliyotumwa na ofisa habari wa TFF, Boniface Wambura inasema kuwa uamuzi wa kuongeza timu msimu wa 2015/16 umefanywa kwa lengo la kuongeza ushindani katika ligi hiyo na kuwawezesha wachezaji kupata mechi nyingi zaidi.
“Kwa mabadiliko hayo maana yake ni kuwa Ligi Kuu msimu wa 2015/16 utakuwa na mechi 240, wakati kwa sasa una mechi 182,” alisema Wambura.
Katika hatua nyingine, habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kamati hiyo ya utendaji itapitisha adhabu kwa mtu au klabu itakayopatikana na hatia ya kupanga matokeo.
“Kumekuwa na upangaji wa matokeo sana katika ligi, msimu ujao atakayebainika anaweza kufungiwa miaka 10 hadi 20 au maisha,” alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
Wakati huohuo, Wambura alisema Kamati ya Utendaji itafanyia uamuzi mapendekezo ya idadi ya wachezaji wa kigeni.
katika eneo hilo baada ya kupata maoni ya klabu za VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ambazo Mei 11 mwaka huu zitakutana na Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
“Mapendekezo ya Kamati ya Mashindano ni kuwa idadi ya wachezaji wa kigeni iendelee kuwa watano kama ilivyo katika kanuni za sasa za VPL,” aliongeza Wambura.
Next Post Previous Post
Bukobawadau