Bukobawadau

BREAKING NEWS:Mahakama yawavua nyadhifa madiwani sita Bukoba

Hizi ni taarifa za hivi punde.Ni kutokana na sakata linaloendelea bukoba kuhusiana na mgogoro katika manispaa hiyo.

Madiwani hao kutoka vyama tofauti walifunguliwa kesi mahakamani na Diwani wa Kata ya Kahororo, Chifu Kalumuna (CCM) kuwa hawana sifa za kuendelea kuwa madiwani.

Kalumuna, ambaye pia ni Mwenyekiti wa UVCCM Manispaa ya Bukoba na Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Uchumi alifungua shauri dhidi ya madiwani hao kuwa wamepoteza sifa za kuendelea kuwa madiwani kwa kushindwa kuhudhuria vikao vya kisheria bila taarifa.

Madiwani walalamikiwa katika kesi hiyo walikuwa ni Diwani Yusuph Ngaiza (Kashai CCM), Dauda Kalumuna (Ijuganyondo CCM), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo CCM) na Deusdedith Mutakyahwa wa Kata ya Nyanga CCM.

Wengine ni Richard Gaspar (Miembeni CCM), Mulungi Kichwabuta (Viti Maalumu CCM), Israel Mulaki (Kibeta CHADEMA) na Rabia Badru (Viti Maalumu CUF).

Baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kusoma taarifa ya ukaguzi kwenye manispaa hiyo, madiwani walitakiwa kuanza vikao mara moja.
Hata hivyo, Kalumuna aliweka pingamizi dhidi ya madiwani hao kutohudhuria vikao mpaka itakaposikilizwa kesi ya msingi aliyofungua dhidi yao.

Baada ya mahakama kupitia hoja za mlalamikaji na walalamikiwa kupitia kwa mawakili wao, Hakimu wa mahakama hiyo, Charles Uisso alisema mahakama hiyo ina uwezo kisheria kusikiliza shauri lao na kutaka upande wa walalamikiwa kupeleka hoja nyingine za msingi kama zitakuwapo.

Upande wa walalamikiwa walianza kuwasilisha hoja mpya za utetezi Machi 3, kwa uamuzi huo vikao vya Baraza la madiwani viliendelea kusimama kusubiri uamuzi wa mahakama.

Walalamikiwa walikuwa wanatetewa na Wakili Mathias Rweyemamu, huku mlalamikaji ukiwakilishwa na Wakili Aaron Kabunga.

Chanzo cha kesi hiyo ni mgogoro ambao umechukua muda mrefu na kusimama kwa maendeleo kati ya Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki na Meya wa Manispaa hiyo, Dk Anatoly Amani.

Haijulikani kama uamuzi huu wa mahakama utatuliza hali ya hewa katika manispaa ya Bukoba.
Next Post Previous Post
Bukobawadau