Bukobawadau

RAIS KIKWETE NA RAIS NKURUNZIZA WAZINDUA UIMARISHWAJI WA MPAKA WA KIMATAIFA KATI YA TANZANIA NA BURUNDI MUGIKOMERO MKOANI KAGERA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Jamhuri ya Burundi Pierre Nkurunziza kwa pamoja walizindua uimarishwaji wa mpaka wa kimataifa kati ya nchi mbili za Tanzania na Burundi kijijini Mugikomero  Wilayani Ngara tarehe 27/08/2014
Uzinduzi wa uimarishwaji wa mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Burundi ulifanyika  kwa ushirikiano na makubaliano kati ya Watanzania na Warundi baada ya miaka 90 toka mipaka iliyowekwa na wakoloni tarehe 12/08/1924 na iliyokuwa “Anglo Beligian Boundary Commission”.

 Rais Kikwete akiwahutubia wananchi toka nchi za Burundi na Tanzania waliofurika katika mpaka wa  Mugikomero alisema mpaka umeimarishwa siyo kwasababu kuna mgogoro bali ni kutokana na ushirikiano na mahusiano mazuri kati ya wananchi wa Tanzania na Burundi.
“Ni vyema kuimarisha mipaka yetu kusudi wananchi waelewe wapo upande gani wa nchi hizi mbili ili kuweka mahusiano mazuri na kuondoa mkanganyiko ni wapi baadhi ya wananchi wanatoka, baada ya kuimarisha mipaka wao wenyewe wataona na kujua ni raia wan chi gani. Alisema Rais Kikwete.
Rais kikwete alisema kuwa uimarishwaji wa mpaka kati ya Tanzania na Burundi ni agizo la Umoja wa Nchi za Afrika (AU) ambapo Umoja wa nchi za Afrika uliagiza nchi wanachama ifikapo mwaka 2017 nchi zote ziwe zimeimarisha mipaka yao kwa makubaliano ili kuondoa migogoro kati ya nchi moja na nyingine isiyokuwa ya lazima.
Mara baada ya mpaka wote wa Tanzania na Burundi kuwa umeimarishwa utasainiwa mkataba wa makubaliano kati ya Tanzania na Burundi na kuufuta mkataba wa mipaka uliowekwa na wakoloni na mkataba huo utakuwa wa Watanzania na Warundi na siyo Waingereza na Wajerumani.
Rais Kikwete alisistiza kuwa kwa kizazi cha sasa kilichoshuhudia kazi za kurudisha mawe ya mipaka kitakuwa mlinzi wa mpaka na anaamini kuwa mawe ya mipaka hayawezi kuhujumiwa wala kung’olewa kwani sasa wananchi wameelewa nini maana ya mawe hayo na wataendelea kuyalinda na kudumisha udugu kati ya nchi mbili.
“Marafiki huchora mipaka kwa kalamu kukiwa na amani na utulivu lakini maadui huchora mipaka kwa nguvu na wino wa damu sisi ni ndugu na mipaka yetu tumeimarisha kwa makubaliano makubwa na ushirikiano na tutaendelea kudumisha amani na utulivu daima” Alisistiza Rais Kikwete.

Waziri wa Ardhi na Mendendeleo ya Makazi wa Tanzania Profesa Anna Tibaijuka akizungumzia uimarishwaji wa mipaka kati ya Tanzania na nchi jirani alisema kuwa tayari kwa upande majini mipaka kati ya Tanzania na nchi jirani tayari imeimarishwa na awamu ya kwanza kati ya Tanzania na Burundi imekamilika  kwa kilometa 170. (Ngara Kagera)
Awamu ya pili itakuwa ni mpaka uliopo upande wa mkoa wa Kigoma kilometa 120 na awamu ya tatu itakuwa kilometa 160 katika mpaka wa Tanzania na Burundi ulipo mkoani Kigoma. Profesa Tibaijuka alisema kuwa zoezi la kuimarisha mipaka linahitaji fedha nyingi na ndiyo maana wanafanya uimarshaji wa mipaka kwa awamu.
Profesa Tibaijuka alisema uimarishaji wa mipaka unafanywa kwa makubaliano kati ya nchi husika na makubaliano hayo ni pamoja na kila nchi kukubali kuacha eneo la wazi la meta 12.5 (Buffer Zone) kila upande  kutoka kwenye jiwe la mpaka na kuliacha eneo hilo bila kulifanyia shughuli yoyote ile ya kibinadamu ili mpaka uonekane vizuri.
Profesa Tibaijuka  alisema kwa sasa zinahitajika zadi ya billion 2.7 ili kukamilsha uimarishwaji wa mpaka kati ya Tanzania na Burundi kwa awamu mbili zilizobaki. Rais Kikwete alihaidi mbele ya wananchi kutafuta fedha hizo ili wizara ikamilishe kazi hiyo kabla ya mwaka 2017 na kuagiza yafuatayo;
Kwanza wananchi wote wanaoishi katika maeneo ya mipaka wayalinde mawe yaliyojengwa kuonyesha mipaka bila kuyahujumu, Pili Mikoa na Halmashauri zote zinazopakana na nchi jirani itenge bujeti ya kilinda mipaka iliyoimarishwa, na mwisho ni Kamati zinazohusika na uimarishaji wa mipaka kukamilisha kazi kwa wakati kabla ya mwaka 2017
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza akihutubia umati uliofurika Mugikomero Wilayani Ngara  aliishukuru Tanzania kwa kushirikana na  nchi yake katika kushirikishwa, kuunda kamati ya pamoja ya wataalam hatimaye kufanya kazi kwa pamoja ya  kuimarisha mipaka kati ya nchi hizo mbili
Rais Nkurunziza alisema wakati Burundi inatafuta uhuru Rwagasole alishikwa mkono na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kumsaidia sana mpaka Burundi ikapata uhuru. Aidha alisema kuwa Tanzania imekuwa ikisaidia sana Warundi wanapopata matatizo na kuyatatua matatizo yao.
 “Wakati wa machafuko huko Burundi zaidi ya warundi milioni moja walikimbilia Tanzania na walifanya uharibifu mkubwa wa mazingira lakini bado ndugu zetu watanzania walendelea kutusaidia na kutuvumilia bila kutuchoka ambapo inaonyesha kuwa Tanzania ni zaidi ya undugu.” Alishukuru Rais Nkurunziza.
Rais Nkurunziza aliihakikishia Tanzania kuwa Burundi watendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania aidha, nchi ya Burundi itaendelea kuchangia na kutoa ushirikiano katika kuimarisha mipaka kati yake na Tanzania.
Tanzania inapakana na nchi nane na zifuatazo ni kilometa za mipaka kati ya Tanzania na nchi hizo; Rwanda 217 km, Zambia 338 km,  Uganda 396 km, Burundi 451 km, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) 473 km, Malawi 475 km, Msumbiji 756 km, na  Kenya 769 km.
Next Post Previous Post
Bukobawadau