Bukobawadau

MOYO WA MBOWE UNAPASWA UPONGEZWE NA KUIGWA

NA PRUDENCE KARUGENDO
UCHAGUZI unaoendelea ndani ya Chadema ni mfano wa kuigwa katika medani ya kisiasa. Ni wa kuigwa katika mambo kadhaa kama nitakavyoeleza hapa chini.
Kituko ni kwamba wakati uchaguzi huo ndani ya Chadema ukiendelea yameanza kujitokeza malalamiko na manung’uniko toka kwa watu walio nje ya chama hicho, ambao sio wanachama, ya kwamba baadhi ya viongozi, hususan wa ngazi ya kitaifa, wamekaa sana katika nafasi zao walizonazo ndani ya chama!
Wakati nikiwa nimeduwazwa na malalamiko hayo, nikijiuliza watu hao wanawashwaje na pilipili wasiyoila, rafiki yangu aliye kada wa chama tawala, CCM, akaniambaia kwamba atashangaa sana ikiwa Chadema itamchagua tena Freeman Mbowe kuendelea kuwa mwenyekiti wake! Madai yake ni kwamba Mbowe kakaa sana kwenye nafasi hiyo.
Kwa vile madai ya aina hiyo yanatolewa na watu wenye akili timamu, hata kama wako nje ya chama, nimeona kuna hatari maneno yao hayo yakawaingia na kuwapotosha hata walio ndani ya chama wakidhani yana ukweli wa aina fulani,  na hivyo kuwayumbisha kimtazamo. Ndiyo maana leo nikaona suala hilo linafaa kuwa mjadala katika makala haya.
Nilimwambia rafiki yangu huyo, ambaye sina hakika kama anaelewa chama chake CCM kilikoanzia, kwamba Chadema ni chama ambacho bado kinajengwa tofauti na CCM ambacho waliomo ni kama wapangaji tu wanaofurahia muundo wa nyumba wakati wajenzi wake wachache waliobaki wakisimangwa.
Katika CCM mara nyingi tumeshuhudia kebehi za aina mbalimbali kwa wale ambao tunaweza kuwaita wajenzi wa chama hicho, maneno kama wazee hawafai, huu ni wakati wa vijana, hawana lolote hao wanasubiri kufa tu nakadhalika, yanadhihirisha kwamba wapangaji hawana shida tena na wajenzi.
Ni muhimu kuelewa kwamba chama cha siasa kinajengwa na watu wenye moyo uliojaa dhamira ya kweli, watu walio tayari kuterekeza mali na hata vipato pamoja na kila kitu kilicho kwenye miliki zao kwa faida ya chama. Hao hawafanani kabisa na watu wanaotafuta kupanga ndani ya chama kilichojengwa tayari.
Mfano mzuri wa hapa nchini ni wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Aliongoza ujenzi wa TANU na baadaye CCM. Wakati wa kuanzishwa kwa TANU Mwalimu aliamua kuacha kazi yake nzuri na ya heshima sana enzi hizo, aliyoisomea kwa karibu miaka 7, Kampala na Edinburgh, kwa ajili  ya ujenzi wa chama hicho.
Baada ya hapo Nyerere alikaa kwenye usukani kwa karibu miaka 37 bila manung’uniko yoyote toka kwa yeyote. Aliporidhika kwamba chama chake kipo kwenye mwendo salama, kutokana na kuizoea safari, ndipo akamuachia usukani mtu mwingine.
Sasa ni chama gani kingine katika Tanzania ambacho kimeongozwa na mtu mmoja kwa muda kama huo? Wanaosema kwamba Mbowe kakaa sana kwenye ukuu wa chama  wanalijua hilo?
Pamoja na uchanga wake, Chadema kinaye mwenyekiti wa tatu tangia kianzishwe, karibu sawa na CCM chenye mwenyekiti wa nne tangia kianzishwe zaidi ya miaka 60 iliyopita. Chadema kwa miaka 22 kinao wenyeviti 3, CCM kwa miaka 60 kinao wenyeviti 4!
Lakini hata hivyo, mafanikio aliyokipatia Nyerere chama hicho mpaka alipong’atuka ndiyo yanayokifanya CCM kitambe kwa sasa, pamoja na mengine mengi kuachwa au kubomolewa na wanaopanga katika chama hicho kwa wakati huu. Ndipo tuelewe kwamba mpangaji na mjenzi wana thamani tofauti katika jengo lolote liwalo.
Hebu tuigeukie Chadema. Mafanikio ya Mbowe katika chama hicho yanalinganishwa au kufananishwa na yapi yaliyowahi kutokea  tangu kianzishwe? Na kama hayapo, hivyo anayesema kwamba mwenyekiti huyo amekaa sana kwenye nafasi hiyo tunawezaje kusema kwamba anakitakia mema chama hicho wakati chenyewe bado kinayaona hayo mafanikio kama mwanzo wa safari yake?
Hiyo maana yake ni kwamba anayemchoka Mbowe kwa sasa ni kama ameyachoka mafanikio ambayo chama anachokiongoza kinaendelea kuyapata. Inawezekanaje mtu wa aina hiyo tukamuona mwema kwa chama hicho?
Ikumbukwe kwamba Mbowe kaamua kuachia shughuli zake zote na kujikita katika kukijenga chama, tangu mwanzo sijaona dalili zozote kwamba alitaka chama ndicho kimjenge yeye badala yake. Ni watu wachache wenye maamuzi magumu ya kiasi hicho.
Namkumbuka Mzee Mandela alipoamua kuachana na mkewe wa kwanza, Evelyn, kwa ajili ya ANC. Sio wengi wenye ujasiri huo.
Hivyo anayedai kuwa mwenyekiti huyo, Mbowe “Sauti ya Radi”, amekaa sana kwenye uongozi wa Chadema halijui alisemalo kwa vile ni wazi anakuwa ametumwa na maasimu kufanya hivyo.
Hata hivyo wanaokuwa wamemtuma mtu wa aina hiyo wanakijua walichokilenga, sababu wao wanayaelewa mafanikio ya mwenyekiti huyo aliyokipatia chama chake. Ni kwamba hawayataki kwa vile yanawatia kiwewe. Inasemwa kwamba adui muombee njaa.
Mwenyekiti huyo wa Chadema anapaswa atofautishwe na wale wanaoingia kwenye chama wakiwa hawana chochote, hawana umaarufu wala mali, wakitegemea kuvipata ndani ya chama. Wengine baada ya kuvipata wanavitumia kama mtaji wa kukisaliti chama. Ndipo wanayafikiria mapinduzi kwa kutumiwa na maasimu wa chama ili kukiyumbisha.
La kuzingatia ni kwamba Mbowe hakuingia Chadema ili kutafuta umaarufu wala mali. Mimi binafsi nilimjua Mbowe, achilia mbali baba yake mzazi aliyekuwa mmoja wa wafadhili wa harakati za kutafuta uhuru wa nchi yetu, wakati hajawa na mpango wa siasa, umaarufu alikuwa nao tayari. Kwahiyo hatuwezi kusema siasa ndiyo imembeba na kufanya ajulikane ikiwa imempa umaarufu alio nao kwa sasa.
Kwa upande mwingine ipo mifano mingi ya watu wanaohangaika huku na huko wakitafuta umaarufu na pengine mali. Mfano tumewaona vijana waliokuwa wameivamia Chadema, na bila kujua chama hicho kikawapatia umaarufu wa uhakika. Baada ya lengo lao kutimia vijana hao wakautumia umaarufu huo kuanzisha vurugu ndani yake, lakini wakaenguliwa. Kwa vile mtaji wa umaarufu tayari walikuwa nao wakautumia kuanzisha chama kingine cha siasa, ni haki yao.
Ila kwa vyovyote vile chama hicho kipya kitabaki kuwa zao la Chadema kama ilivyo CCM kwa vyama vya TANU na ASP. Hakiwezi kufanya lolote zuri pasipo kupongezwa Chadema kwanza, hata kama kuanzishwa kwake zilikuwa ni njama za kuidhoofisha Chadema.
Vilevile tulimshuhudia mwanasiasa mmoja, mkongwe, aliyeanzia chama tawala kama mpangaji lakini, sababu chama chake kilipomwelekeza afuate utaratibu fulani kikiamini ni mzalendo ndani yake, yeye akaamua kuuvua kabisa uanachama na kujaribu “ubangaizaji” katika upinzani. Lakini kutokana na kukosa uzalendo mtu huyo akalazimika kuvizunguka karibu vyama vyote vya upinzani akitafuta pa kujibanza kupata maslahi binafsi.
Ndipo baadaye, baada ya kuhakikisha ametaabika vya kutosha, chama tawala kikamshika mkono na kumrudisha kwake. Sasa mtu huyo anaapa kuubomoa upinzani bila kujali hifadhi uliyompatia kutokana na tabia yake ya kukosa uzalendo.
Nani anaweza kusema mtu huyo ana nia thabiti ya ujenzi na uimarishaji wa mahali alipo kwa sasa hata kama yeye anafanya kila hila ili umma uamini hivyo? Sababu anayoyasema kwa upinzani kwa sasa ndiyo yaleyale, au zaidi, aliyoyasema kwa CCM pale alipohamia kwenye upinzani akiiona CCM haifai.
Lazima yeye atabaki ni mpangaji tu mwenye kuhamia kwingine kila anapoona nyumba aliyomo imeanza kuyumba. Hana dalili zozote za ujenzi wala ukarabati wa mahali alipo.
Kwa upande wa Chadema wapo watu, hasa vijana, wenye dhamira ya kweli ya ujenzi na uimarishaji wa chama hicho. Uzalendo wao ndani ya chama hicho siutilii shaka hata kidogo kulingana na unavyojionyesha, hauna madoa.
Kwa hapa nitoe mfano wa kijana mmoja, Kamanda Baraka Leonard Mfilinge, mwenyeji wa Ilula, Iringa. Kijana huyo ana moyo wa aina yake kiitikadi na katika ujenzi wa Chadema. Ni mzalendo wa kweli kiitikadi.
Tulipofahamiana ndipo alipokuwa amemaliza kidato cha 6. Mapenzi yake kwa Chadema yamemfanya aachane na elimu ya Chuo Kikuu kwanza, alikatisha masomo chuoni na kurudi kufanya kazi za kujitolea akipita maeneo mbalimbali, hasa ya vijijini kule kwao Iringa, akiinadi Chadema kwa vijana na wazee. Hiyo ni kazi aliyoanza kuifanya akiwa hajulikani kwa ngazi yoyote kichama.
Mara nyingi amefanya hivyo akitembea kwa miguu na mara nyingine akishinda njaa kutokana na kutokuwa na kipato chochote.
Kusema ukweli anayoyafanya Baraka Mfilinge kwa Chadema nashindwa kuyatofautisha na aliyoyafanya Mwalimu Nyerere kwa TANU baada ya kuacha kazi ya uwalimu St. Francis College (Pugu).
Harakati za Baraka kuitumikia Chadema zimemfikisha mpaka ngazi ya kitaifa ambako ameshiriki katika chaguzi mbalimbali kama uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, Sombetini – Arusha, Kiborolonyi – Moshi, Kiomoni – Tanga, Bagamoyo, Ng’ang’ange, Ukumbi, Ibumu, Kalenga na Chalinze.
Kwa sasa Baraka kachaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA), mkoa wa Iringa. Na sasa kagombea nafasi ya Uratibu na Uhamasishaji wa Vijana kitaifa.
Kama kweli tumedhamiria upinzani wa kweli katika siasa za Tanzania ningewaomba wana Chadema wawafikirie watu wa aina ya Baraka Leonard Mfilinge katika ujenzi na uimarishaji wa chama hicho.
Nimalizie kwa kusema kwamba isitokee hata mara moja chama cha siasa kikakubali kusikiliza ushauri na ushawishi toka nje ya chama kinapofanya mambo yake ya ndani, kama uchaguzi. Hata Msajili wa Vyama vya Siasa nchini hapaswi kufanya hivyo. Yeye anachotakiwa kukifanya ni kuangalia kama taratibu na kanuni vimefuatwa kulingana na katiba ya chama iliyopelekwa kwake. Vinginevyo atakuwa anatumiwa kukiua alichowekwa kukisimamia na kukilinda.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau