Bukobawadau

SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA LAWAWEZESHA VIJANA MKOANI KAGERA KUJIAJILI KUPITA MASHINE ZA KUFYATUA TOFALI ZA GHARAMA NAFUU

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lawawezesha vijana Mkoani Kagera kujiajili kwa kuwapatia mashine 32 za kisasa za kufyatua matofali yenye gharama nafuu zenye jumla ya gharama ya shilingi 14,400,000/=
Mashine hizo zilikabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe ofisini kwake kwenye hafla fupi na mwakilishi wa shirika la Nyumba la Taifa  Bw.Adrian Dominick tarehe 1, 2014.
 Mashine za tofali nafuu.
Katika hafla hiyo Mkuu wa mkoa alizikabidhi mashine hizo kwa Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri nane za Mkoa wa Kagera kwajili ya kuzikabidhi mashine hizo kwenye vikundi vya vijana katika halmashauri zao.

Akikabidhi Mashine hizo Bw. Adrian kwa Mkuu wa Mkoa alisema dhumuni kubwa la shirika ni kuwawezesha vijana kujiajili na kutoka vijiweni ili kujiunga katika vikundi na kufanya kazi kwa kujituma na kujiingizia kipato halali.

Aidha Bw. Adrian alisema mashine hizo zitawasaidia wananchi wa Mkoa wa Kagera kujenga nyumba za gharama nafuu kwa kutumia matofali yanayoingiliana bila kutumia udongo yatakayofyatuliwa kwa kutumia mashine hizo za kisasa.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera akikabidhi mashine hizo kwa Halmashauri za Wilaya alisema ili kuhakikisha vijana wanajiajili sasa ni wakati taasisi za serikali na wananchi binafsi kuanza kutumia matofali yatakayozalishwa kwenye vikundi hivyo vya vijana ili kuwapa vijana ajira.

Aidha alilishukuru Shirika la Nyumba la Taifa kuukumbuka Mkoa wa Kagera katika kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, pia aliwaasa vijana kujituma na kuchapa kazi kwa bidii ili kupata maisha bora.

Kila Halmashauri ya Wilaya ilipewa mashine nne aidha kikundi kitakachonufaika na mashine hizo pia kitawezeshwa shilingi 500,000/= na shirika la Nyumba la Taifa  kama mtaji wa kuanzia uzalishaji wa tofali zenye gharama nafuu.
Next Post Previous Post
Bukobawadau