Bukobawadau

FIKRA POTOFU ZINACHANGIA UGUMU WA MAISHA


 Na Prudence Karugendo
KUFUATIA  makala niliyoandika hivi karibuni nikilalamikia michango mikubwa ya sherehe,  wamejitokeza wasomaji wengi kuniunga mkono. Karibu wote waliowasiliana na mimi baada ya kuisoma makala hiyo  wameniomba niuendeleze mjadala huo kuzidi kuweka wazi kinachoifanya jamii yetu kuwa na mtazamo huo potofu.
Kinachojionyesha kwamba mambo hayo ya kuchangishana kwa ajili ya sherehe yanafanyika kwa mtindo wa kulazimishana, bila kutilia maanani ugumu wa maisha unaoikabili jamii yetu, ni kwamba sikupata hata mtu mmoja aliyepingana na mtazamo wangu huo wala kuukosoa, wasomaji wote walikuwa wanailaani tabia hiyo ya kuchangishana kwa ajili ya sherehe za masaa machache tu huku yakiachwa mambo yenye maana na yaliyo muhimu. Mpaka nimefikia kujiuliza kama watu wanailaani michango hiyo kwa nini wanalazimika kuichanga?
Mara nyingi nimeuliza kwa nini tunalazimika kuingia kwenye gharama zisizo za lazima kwa kufanya mambo yasiyokuwa na faida endelevu kama haya ya kuchangia sherehe, ziwe za harusi, kumuaga binti anayeenda kuolewa, sendoff, na nyingine nyingi zilizojaa kwenye jamii yetu, tena kwa kuchangia kwa pesa nyingi? Lakini mara nyingi jibu ninalopewa ni la kwamba unapochanga pesa kidogo unategemea utakunywa na kula nini wakati wa sherehe husika? Eti ukubwa wa michango unatokana na kupanda kwa gharama ya maisha!
Jambo hilo linanipa ugumu wa kulitafsiri, sababu kumchangia mtu ili akafanye sherehe yake haina maana kwamba unachangia unachoenda kukila au kukinywa, hapana, unachangia ili kumwezesha jamaa yako afanikishe sherehe yake. Kwa maana hiyo sio kwamba unatakiwa uchangie utakachoenda kukitumia. Suala la  kufanya sherehe ni la mwenye sherehe, kwa maneno mengine ni kwamba alipaswa afanye yeye sherehe na kuwakaribisha walio karibu naye kwa ajili ya kusherehekea, kula na kunywa bure. Kwa ufupi ni kwamba mchango wa mwalikwa ni uwepo wake kwenye sherehe husika, huo ni mchango tosha.
Nasema hivyo kwa sababu mwenye sherehe, hata awe na mapesa mengi kiasi gani, bila kuwa na watu kwenye sherehe bado hawezi kufanikisha lolote, sherehe bila watu haiwezi kuhesabika ni sherehe. Ndiyo maana nasema siyo lazima mtu achangie ndipo aweze kushiriki sherehe.
Yapo mambo ambayo yanahitaji mtu kuyachangia ili aweze  kuyashiriki. Michezo, kama mpira wa miguu, Simba na Yanga kwa mfano, ili uweze kuingia uwanjani kuona mpambano huo wa watani wa jadi ni lazima ulipe kiingilio. Wanaoandaa pambano hilo wanategemea wapate pesa toka kwa watazamaji au washangiliaji. Pambano la aina hiyo ni moja sehemu ya wahusika kujipatia kipato zikiwemo timu zenyewe.
Lakini linapokuja suala la sherehe mambo yanakuwa tofauti. Sherehe sio kwa ajili ya kukusanya kipato, ni kwa ajili ya kutumia tu kukifurahia kilichokusudiwa. Kama ni harusi ni kwa ajili ya kuwapongeza wanaooana, kumpongeza aliyeoa au aliyeolewa.
Na wenye jukumu la kufanya hivyo ni wazazi wa wahusika au wahusika wenyewe. Wageni waalikwa kazi yao ni kuhudhuria ili kuwapongeza na kupatiwa kila kilichoandaliwa katika kusherehesha tukio. Haina maana wala ulazima wa waalikwa kukichangia watakachokitumia kwenye sherehe husika.
Hatahivyo sio vibaya kwa watu wa karibu na wenye sherehe kuwapa michango yao kama sehemu ya kuwaunga mkono, ila izingaiwe kwamba anayekuunga mkono hupaswi kumwekea kiwango anachopaswa kukuunga nacho mkono kana kwamba bila yeye wewe huwezi kufanikisha lolote. Kama ni hivyo bora mtu akaachana na sherehe.
Sioni kwa nini mtu atamani kufanya sherehe kubwa ya kifahari kwa kutegemea mifuko ya watu wengine. Mambo hayo ndiyo yanayowafanya watu waweke kiwango cha chini, kwamba kiwango cha chini ni shilingi laki moja chini ya hapo mtu atapewa tu asante bila ya kadi! La kujiuliza ni kwa nini mtu akupangie kiwango cha kumsaidia kufanya sherehe halafu mwisho wa siku sifa apate yeye kwamba alifanya sherehe ya kifahari wakati mambo yote yalikuwa ya kuombaomba?
Mimi naona sio vibaya kama mtu ana pesa yake, hata akipanga kufanya sherehe ya kifahari namna gani ni juu yake,  kusudi kama ni sifa ziende kwake kwa maana halisi, kwamba kafanya sherehe ya kifahari kwa kuwaita watu washerehekee bila kuwatoza kiingilio. Lakini kwa kuwapangia kiwango wanachopaswa kutoa sifa inastahili iwaendee walioshiriki kwa kukubali bila sababu za msingi kulipa kiingilio kikuwa kuhudhuria sherehe ya ndugu, jamaa, rafiki au jirani yao.
Nasema kwamba sio sababu ya msingi kuhudhuria sherehe ambayo unaambiwa sahani ya chakula ni shilingi 35,000 – 40, 000 wakati chakula chenyewe ni cha kawaida, wali vijiko 3, nusu ndizi, kipaja cha kuku na madoido mengine ambavyo kwa pamoja havifikii thamani ya shilingi 6, 000/=! Papo hapo eti vinywaji, mfano bia inayouzwa kwa sh. 2,200 eti kwenye sherehe inauzwa kwa sh. 5000/, soda ambayo kawaida ni sh. 600/ eti kwenye sherehe ni sh. 2000/ nakadhalika!
Mambo mengine yanayonifanya mpaka nikasikia kizunguzungu ni huu mtindo wa sasa ambao baadhi ya wafanyabiashara wanajenga maholi yeye viyoyozi kiasi cha kuwazubaisha watu na kuwafanya wayatamani pamoja na gharama kubwa zinazowekwa ili kuyatumia. Maholi hayo kwa sasa yanakwenda mpaka shilingi 10, 000, 000/ wakati muda unaotumika kukaa mle hauzidi masaa manne! Sababu kawaida kuingia kwenye holi, kama ni sherehe ya harusi au “sendoff” kumuaga mwali anayeenda kuolewa,  ni saa 2 mpaka saa 6 usiku. Bila kingine cha ziada tayari kiasi cha kati ya shilingi milioni 3 mpaka 10 kinakuwa kimeteketea!
Jambo lingine ambalo nashangaa kwa nini watu hawalipigii kelele ni ule mtindo wa wenye maholi ya sherehe kutaka kuhodhi kila mapato yanayotokana na wenye sherehe. Mbali na kutoza pesa iliyo kama kufuru kwa ajili ya holi tu, bado wenye kumbi hizo wanataka mapambo, vyakula, vinywaji nakadhalika, vyote vitoke kwao.
Unaweza kukuta wenye ukumbi wanataka mpaka shilingi milioni 20 kwa ajili ya chakula tu, wakati chakula kitakachotumika hakizidi cha sh. 7,000,000/, kwahiyo kinachobaki hakitupwi. Pamoja na kuwa kimenunuliwa chote kikibaki kinahifadhiwa na kuuzwa tena kwenye shughuli nyingine! Matokeo yake wenye bahati mbaya wanaambulia kuuziwa kwa bei mbaya chakula kilichooza!
Wakati mambo yakiwa hivyo bado kumbi za kawaida ambazo zinatoza viwango nya wastani zipo, ila kwa fikra za ajabu watu hawazipendi kumbi hizo kwa madai ya kwamba zimepitwa na wakati! Lakini ukija kuangalia wanaosema hivyo wana kitu gani kinachowafanya wayaone mambo mengine yamepitwa na wakati, kwa maana ya kuwa na kipato kikubwa kinachowafanya wawe na jeuri hiyo, kipato kinachokwenda na wakati,  unakuta hakuna!
Kipato cha miaka 20 iliyopita karibu ni kilekile kinachotumika mpaka leo! Ila watu wanakubaliana na kupanda kwa gharama za maisha wakijiminya kwa kila namna ili kwenda nazo sambamba gharama hizo! Wanakubali kwamba mambo fulanifulani, kimatumizi, yamepitwa na wakati ila hakuna anayeona kuwa kipato kilichopo kwa sasa nacho kimepitwa na wakati!
Hayo ndiyo mawazo ya Watanzania walio wengi. Kufanya mambo pasipo  kutafakari kwanza huku madai ya kwamba gharama za maisha zinapanda yakiendelea kila kukicha! Lakini ukija kuangalia utakuta gharama hazipandi zenyewe, zinapandishwa na wananchi walewale wanaolalamika kutokana na kufanya mambo wakiwa wameegemea kwenye ufahari usio na mpangilio, ufahari usiojali kiwango cha kipato.
Kwa maana hiyo nimalizie kwa kusema kwamba upandaji wa gharama za maisha unatokana na fikra za wananchi zilivyo, wananchi wakisema gharama zisipande haziwezi kupanda hata kidogo, ila wakiziachia zipande zitapanda mpaka mbinguni, na hakuna anayepaswa kulalamika. Sababu anayejipiga mwenyewe hapaswi kulia na mtu.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau