Bukobawadau

HII NDIYO KAULI YA MNYIKA BAADA BMK KUPITISHA RASIMU YA KATIBA MPYA

MAHARAMIA WAMEPITISHA KATIBA HARAMU; WAMEANZISHA MGOGORO CHANYA NA MWANYA WA MABADILIKO

Dira ni kuwa na katiba bora itakayojenga Tanzania yenye demokrasia ya kweli, uhuru wa kweli na maendeleo endelevu kwa watu wake wote. Lakini uharamia katika mchakato wa katiba mpya umelipasua taifa. Mpasuko huu unaweza kuwa mgogoro hasi wenye madhara kwa wananchi au mgogoro chanya utakaoleta mabadiliko nchini.

Maharamia wanashangilia kilevi katika Bunge Maalum baada ya kukamilisha uharamia dhidi ya rasimu ya katiba ya wananchi kwa kupata theluthi mbili kwa njia za kiharamia. Katiba iliyopendekezwa kiharamia na kudharau maoni ya wananchi ni katiba haramu iliyokosa maridhiano na muafaka wa kitaifa.

Katiba haramu, katiba ya maharamia, katiba ya mafisadi, katiba ya CCM wahafidhiana na mawakala wake inapaswa kupingwa mtaani na mahakamani kwa mbinu mbalimbali.

Iwe ni kwa mikutano, migomo, maandamano, mashtaka au katika sanduku la kura. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba mchakato huu wa mabadiliko ya katiba ni mwanya wa mabadiliko katika taifa letu.

Theluthi mbili ilianza kutafutwa tangu wakati wa kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, tulipinga muundo wa Bunge Maalum na uteuzi wake; madhara yake yamedhihirika sasa.

Rais Kikwete akaongezea udhaifu huo kwa kutumia madaraka vibaya kuteua wanaCCM mahafidhina na mawakala wao kwa wingi katika uteuzi wa wajumbe wa kundi la 201 kuongezea katika hodhi haramu ya wabunge na wawakilishi wa chama chake.

Sitta akakamilisha uharamia huo kwa marekebisho haramu ya kanuni za Bunge Maalum ambayo yaliruhusu kura kupigwa nje ya Bunge hilo na mianya mingine ya wizi wa kura.

Jana Oktoba Mosi Sitta alilalamikia hatua yangu ya kumtaja yeye, Chenge na wenzake kuwa ni ‘maharamia’ dhidi ya rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi. Kwa kuwaita maharamia Sitta amelieleza Bunge Maalum kuwa ni “siasa za kichuo chuo” na kwamba “hatuwezi kushika madaraka kwa mbinu za kitoto”.

Nimkumbushe Sitta na maharamia wenzake kwamba mwaka 1958 Mwalimu Julius Nyerere alishtakiwa kwa kuwaita ‘mashetani na maharamia’ wakuu wa wilaya wa Serikali ya mkoloni. Ninapolitazama Bunge Maalum nakumbuka utetezi wake mahakamani wa kukiri kutamka maneno hayo kwa lengo la kuitaka serikali ya kikoloni itupie macho malalamiko ya watu.

Sitta na maharamia wenzake kama wameshindwa hata kuelewa waraka wa viongozi wa dini na kuuita kuwa “hauna utukufu wa Mungu na wa kipuuzi”, ni wazi wamelewa madaraka wasaidiwe kwa kupumzishwa.

Leo Sitta, Samia Suluhu na maharamia wengine wanasherehekea kama walevi ushindi wa muda mfupi walioupata kwa njia za kiharamia ikiwemo kwa kuwashinikiza na kuwarubuni baadhi ya wajumbe kuhalalisha rasimu haramu. Andrew Chenge aliyetajwa kwenye orodha ya mafisadi (list of shame) ndiye aliyeongoza kazi hiyo kuanzia katika Kamati ya Uandishi.

Uharamia huu dhidi ya rasimu ya tume ya mabadiliko ya katiba na maoni ya wananchi unapaswa kuwa kiunganishi kwa umma kutambua kwamba umoja wa ukweli na uadilifu unapaswa kuvuka mipaka ya vyama, dini, pande mbili za Muungano na tofauti zingine.

Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umeonyesha msimamo wake, Mwenyekiti na Wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wameonyesha msimamo wao, baadhi ya viongozi wa dini wameonyesha msimamo wao, baadhi ya wanaharakati wameonyesha msimamo wao, baadhi ya wajumbe ndani ya Bunge Maalum wameonyesha msimamo wao; wewe je?

Namna pekee ya kuirejesha rasimu ya katiba ya wananchi katika hali iliyofikia ni kuikataa katiba haramu na kuwakataa wote waliofanya uharamia kuwezesha rasimu hiyo kupendekezwa na wote watakao itetea katiba hiyo.

Muasisi wa CCM alikiambia chama hicho mwaka 1995 kwamba “watanzania wanataka mabadiliko wasipoyapata ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM”. CCM imepoteza mwanya wa kuwapa watanzania mabadiliko kutoka ndani ya chama hicho.

Uharamia uliofanywa katika Bunge Maalum una baraka za Katibu Mkuu wa CCM Kinana na Mwenyekiti wa CCM Rais Kikwete. Uharamia huo ulilenga kuwezesha Maoni ya CCM yaliyopitishwa na vikao vya juu vya CCM kinyume na maoni ya wananchi. Hatimaye kwa njia za kiharamia wajumbe wanaojiita walio wengi wa CCM wamepitisha katiba haramu iliyopendekezwa.

Mwalimu Nyerere aliandika katika kitabu cha Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania kwamba Rais wa wakati huo Mwinyi alikuwa mtu mwema na mpole lakini “kiongozi dhaifu”. Akamtakia heri na kuomba asaidiwe amalize kipindi chake salama. Akatabiri kwamba chini ya CCM na uongozi wake mbele ni giza tororo.

Rais Kikwete alithubutu kwa kukubali mchakato wa mabadiliko ya katiba kuanza lakini ameshindwa. Na kwa udhaifu alio uonyesha, kwa vyovyote vile mchakato huu hauwezi kusonga mbele na kukamilika chini yake.

Udhaifu pekee anao weza kuupunguza kwa sasa ni kusimamia marekebisho ya 15 ya Katiba ya mwaka 1977 kuwezesha uchaguzi huru na haki katika uchaguzi mkuu wa udiwani, ubunge na urais mwaka 2015 na kuendelea kwa mchakato wa katiba mpya mwaka 2016 kwa kuzingatia maoni ya wananchi. Tumtakie heri Rais Kikwete amalize kipindi chake salama; matokeo ya kura ya katiba haramu iliyopendezwa yatafutwa kwa kupingwa mahakamani ama kwa njia nyingine.

Mahakama kwa kukosa uhuru wa kikatiba isipotimiza wajibu huo wa kusimamia haki kwa wakati; katiba haramu iliyopendekezwa itafutwa kwa sheria maalum itayotungwa na Bunge litakaloongoza nchi baada ya uchaguzi 2015. Ikiwa watawala wa sasa au wa wakati huo watalazimisha katiba haramu kwenda kupigiwa kura ya maoni, ni wazi itapigiwa kura ya hapana na wananchi iwe ni mwaka 2015 au 2016.

Mabadiliko yatafutwe kwa kuwakataa watetezi wote wa katiba haramu kuanzia kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji mwaka 2014. Mabadiliko yatafutwe kwa kutaka Tume itangaze ratiba ya uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2014 ili kila mwenye umri wa kupiga kura ashiriki kufanya mabadiliko kupitia uchaguzi 2015 na kura ya maoni.

Kwa wajumbe mlioshiriki kuandika katiba haramu, naheshimu na nakubaliana na maneno ya Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji (Mstaafu) Joseph Warioba kwamba tutakutana mtaani. Dhima ni kuwa na katiba mpya itayoleta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na Muungano na Muundo wa Utawala thabiti kwa maendeleo endelevu. Nyinyi mkiwa na katiba haramu sisi tutakuwa na rasimu ya wananchi; sauti ya watu, ni sauti ya Mungu hivyo umma utaamua na historia itatoa hukumu kwa maharamia na walevi wa madaraka.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi.
John Mnyika (Mb)
02/10/2014
Next Post Previous Post
Bukobawadau