Bukobawadau

HII NDIYO HOTUBA YA ZITTO KABWE

KUTOKA KWA Z ITTO KABWE:
Hotuba Niliyotaka Kuitoa Bungeni Jana
Posted by TeamZitto
Mheshimiwa Spika, nilijiunga na Bunge lako tukufu mwaka 2005 nikiwa kijana mdogo mwenye malengo ya kupaza sauti ya vijana kwenye masuala yanayohusu nchi yetu na pia kutetea maslahi ya wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Mkoa wa Kigoma.

Katika kudumu kwangu kama mbunge nililelewa na kukuzwa na chama cha siasa cha CHADEMA ambacho kupitia chama hiki niliingia Bungeni. Chama hiki kilinilea na kunikuza tangu nikiwa na umri wa miaka 16 na kupitia chama hiki nimejifunza mambo mengi sana. Nimeijua nchi yangu, nimejua siasa na nimejulikana ndani na nje ya nchi. Nitakuwa mwizi wa fadhila nisipotoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa CHADEMA na viongozi ambao nimefanya nao kazi muda wote nikiwa mwanachama na kiongozi.

Mheshimiwa Spika, Chama kilinikuza kama mwanasiasa lakini watu wa Kigoma Kaskazini ndio walionipa kiti hiki ninachokalia kama Mbunge. Juzi nilipokuwa nyumbani nilipata fursa ya kuwashukuru rasmi wananchi kwa imani waliyonipa kuwatumikia kwa vipindi viwili mfululizo. Wengi wenu ndugu zangu wabunge mnafahamu, mihula miwili sio jambo la mchezo, sio lelemama. Mola atawalipa wananchi wa Kigoma kwa imani kubwa walioionyesha kwangu na kuniwezesha kulitumikia Taifa langu kwa namna nilivyolitumikia.

Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii leo kuzungumzia suala la muda mrefu sasa la kutoelewana kati yangu na chama changu na hivyo kuleta msuguano kati ya wananchi walionichagua kuwawakilisha na chama nilichopitia na kupeperusha bendera yake wakati wa uchaguzi mkuu. Licha ya msimamo wangu wa siku zote kwamba wananchi pekee waliomchagua mwakilishi wao ndio wawe na mamlaka ya kumwondoa kwenye uwakilishi mchaguliwa huyo, mfumo wetu wa kikatiba na mfumo wetu wa kisiasa haupo hivyo na umeamua vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, kwamba chama cha siasa kinaweza kumvua uanachama mwanachama wake na hivyo kupoteza kiti chake cha uwakilishi wa wananchi wake ni moja ya makosa makubwa ya kikatiba ambayo tumeendelea kuyakumbatia, nimekuwa nikipinga na nitaendelea kupinga udikteta wa vyama dhidi ya utashi wa wananchi.

Mheshimiwa Spika, licha ya upinzani wangu mkali wa vifungu kandamizi vya kikatiba, kama mzalendo ninaiheshimu Katiba yetu na mfumo wetu wa sasa na ninaheshimu uamuzi wa mahakama dhidi ya kesi yangu na sitakata rufaa. Hatua itakayofuata ni uamuzi wa chama changu na baadhi ya viongozi wameshatangaza kwa umma kupitia vyombo vya habari kunivua uanachama ingawa sijapewa taarifa rasmi.

Mheshimiwa Spika, ningeweza kukata rufaa kuhusu maamuzi ya mahakama kwani kuna sababu lukuki ya kushinda rufaa hiyo. Lakini ninadhani nimepigania haki zangu kwa muda mrefu sasa. Nimepigania kupanua wigo wa demokrasia ndani ya chama changu kwa muda mrefu sasa. Lakini ugomvi huu hauna manufaa kwa pande zote husika, kwa hakika unatuumiza wote. Mimi ni mwanademokrasia. Naamini katika siasa za ushindani ndani ya chama na katika mfumo mzima wa siasa kitaifa. Lakini sitakuwa tayari kudhoofisha harakati na kazi kubwa walizofanya wanamageuzi waliotutangulia kwa kuendeleza ugomvi unaotuumiza. Hivyo niko tayari kukubali kukaa pembeni. Ninaamini kuwa mapambano ya kuleta mabadiliko ya kweli na demokrasia katika nchi yetu Tanzania ni makubwa kuliko mimi, kuliko kiongozi yoyote wa Chadema na kuliko wanachama wa Chadema. Mapambano haya ya mabadiliko si kwa ajili ya kizazi hiki tu bali kwa vizazi vijavyo. Ndiyo maana siku zote nimesema Nchi kwanza, vyama baadae. Kuona makundi yanajitokeza ndani ya harakati hizi, na kuwa na uhasama mkubwa uliopindukia, unawakatisha tamaa wananchi wanaotutumaini kuleta siasa iliyo tofauti na siasa za sasa. Muda umefika wa kupiga mstari na kuanza upya. Hivyo nimeamua kuwa nitatii maamuzi ya chama ya kunivua uanachama na kung’atuka ubunge.

Mheshimiwa Spika, naomba niweke wazi kuwa nimefikia uamuzi huu kwa utashi wangu mwenyewe na nimepewa Baraka zote na wananchi wangu na wazee wa Jimbo la Kigoma Kaskazini. Najua Watanzania wengi ambao nimewatumikia kwa moyo wangu wote katika kipindi cha miaka hii 10 wanaweza wasikubaliane na uamuzi huu. Hata hivyo Watanzania wajue kuwa mfumo wetu wa siasa na katiba unatoa nguvu kwa vyama vya siasa kudhibiti wabunge wake. Naamua hivi kwa sababu wenzangu ndani ya chama ambao nimehangaika nao usiku na mchana kujenga chama na kukifisha hapa kilipo hawapo tayari kufanya kazi tena na mimi. Nimesoma na kusikia kauli nyingi zinazoweka wazi kuwa hawanitaki ndani ya chama. Nimejitahidi kwa njia zangu zote kuona kama tunaweza kuendelea kufanya kazi pamoja ya kujenga mfumo madhubuti wa vyama vingi nchini lakini imekuwa ngumu kama mwanachama mwenzao. Ninaheshimu uamuzi wao huo.

Mheshimiwa Spika, kwa miaka kumi hii si yote niliyafanya sahihi, yapo ambayo niliyakosea kama mwanadamu katika kufanya kazi kwangu, kwa namna yeyote ile naomba radhi Watanzania wote kwa yote ambayo sikuyafanya kwa usahihi. Mimi ni binadamu, kiumbe dhaifu, sijakamilika. Ni Mola peke yake amekamilika.

Mheshimiwa Spika, siwezi kuanza maisha yangu mapya bila ya kulishukuru Bunge lako tukufu, Bunge la Tisa chini ya Mzee Samwel Sitta na Bunge la Kumi chini yako Mama Anna Simamba Makinda. Bunge limekuwa ni nyumbani kwangu kwa takribani muongo mmoja. Nimekuzwa, nimejifunza, nimepambana, nimefurahi na nimelia ndani ya Bunge hili. Kwa pamoja tumepigania maslahi ya wananchi wetu na kupingana na kufanya mambo kwa mazoea na hivyo kuleta mabadiliko kadhaa. Ni kipindi hiki ambapo wabunge tumekuwa na sauti, Bunge la Tisa lilijenga ‘Bunge lenye Meno’ katika kupambana na ufisadi. Bunge la Kumi limejenga ‘Bunge lenye nguvu’ katika mfumo wa Bajeti ya nchi yetu. Kupitia Bunge hili tumeweka misingi ya kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, wakati Bunge la Tisa litakumbukwa kwa hoja ya Buzwagi iliyopelekea nchi yetu kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa sekta ya madini (Sera mpya ya Madini na Sheria mpya ya Madini ) na hivyo mapato ya sekta ya madini kuongezeka kutoka Tshs 32 bilioni kwa mwaka mpaka Tshs 450 bilioni kwa mwaka hivi sasa; Bunge la Kumi litakumbukwa kwa hoja maalumu ya Tegeta Escrow iliyopelekea mfumo wetu wa maadili ya Viongozi kupitia Baraza la Maadili kuanza kufanya kazi kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa katika miaka iliyopita. Mimi kuwa sehemu ya mabunge yaliyotekeleza hatua hizo za mabadiliko ni jambo la kujivunia sana.

Mheshimiwa Spika, kwa familia yangu, wajumbe wa PAC, tumekuwa nguzo kubwa ya kujenga uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge na wananchi. Napenda kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa kuniunga mkono na kwa kunipa ushirikiano kama Mwenyekiti wao. Changamoto na malezi mliyonipa kwa miaka yote hii yamejenga Mtanzania mmoja mwenye dhati ya kuitumikia nchi yake, muda wowote, wakati wowote na kwa namna yeyote ile bila woga wala upendeleo. Nawashukuru kwa kujitoa kwenu kwa nchi yetu na dhamira isiyo na mawaa ya kujenga Taifa imara zaidi.

Nitaendelea kuwatumikia wananchi wa Kigoma Kaskazini na Taifa langu hata kama nimelazimika kuachia nafasi yangu ya ubunge kwa kipindi hiki kilichosalia kwa kusimamia ukweli, kutetea demokrasia ya kweli na kupigania maendeleo ya kweli kwa mwananchi wa kawaida bila ubaguzi wowote.

Mheshimiwa Spika, Kwa CHADEMA, licha ya tofauti zetu ambazo zimekua kiwango cha kutosameheka, najivunia kwa fursa mliyonipa kuwa sehemu ya Baraza hili la Taifa ambalo leo ninalihutubia kwa mara ya mwisho kama mbunge wa Kigoma Kaskazini. Fursa iliyonifanya niweze kuitumikia nchi yangu na mkoa wangu wa Kigoma. Inawezekana tusiweze kuelewana katika masuala ya uongozi, misingi na itikadi, lakini ninaamini tunapaswa kuelewana na kukubaliana katika kubwa ya kuijenga nchi yetu kuwa Taifa linalojitegemea na lisilo na aina yeyote ya ubaguzi. Taifa lenye uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira na kuondoa umasikini, ujinga na maradhi, Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ni matumaini yangu kuwa tutakuwa bega kwa bega katika harakati hizi katika siku zijazo. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo, nafasi hii ya kihistoria tuliyopewa haihitaji siasa za ubinafsi na unafsi! Uzalendo wetu utapimwa kwa uwezo wetu wa kuweka tofauti zetu binafsi pembeni kwa lengo lililo kubwa zaidi yetu.

Mheshimiwa Spika, Mwisho kwa wananchi wa Jimbo langu, wana Kigoma na raia wote wa Tanzania ambao kwa ridhaa yao nimekaa katika viti hivi kwa miaka takribani kumi, nawahakikishia kuwa dhamira yangu kuwatumikia, nia yangu na sababu za kutoa utumishi wangu kwenu vimekuwa na nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule. Huu ni mwanzo mpya. Ngugi aliandika ‘a grain of wheat’ kwa maana ya kwamba ‘Ili Mbegu iweze kumea lazima ife kwanza’.
Asanteni sana.
Next Post Previous Post
Bukobawadau