Bukobawadau

KUHUSU KUGAWANA MAJIMBO



CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO
(CHADEMA)
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UKAWA KUGAWANA MAJIMBO

Tangu jana kumekuwa na taarifa kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari kuhusu msimamo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya ubunge kwenye majimbo ya uchaguzi nchini.
Habari hizo ambazo zingine zimeripotiwa kwenye vyombo vya habari hususan magazeti ya jana (Alhamis) na leo (Ijumaa), zimesema kuwa UKAWA ‘wameshagawana’ majimbo kadha wa kadha na kwamba bado kuna ubishano katika baadhi ya majimbo kutafuta mwafaka wa kufikia lengo la kuwa na mgombea mmoja badala ya kila chama kuweka mgombea wake.
Tunapenda kutoa ufafanuzi juu ya habari hizo ambazo kwa namna moja ama nyingine zimesababisha usumbufu usio wa lazima kwa wafuasi, wapenzi, wanachama na viongozi wa CHADEMA na wanachama wa vyama vingine vinavyounda UKAWA.
CHADEMA kama walivyo washirika wenza wa UKAWA, kiko kwenye mazungumzo vyama vingine katika umoja huo ili kuhakikisha lengo la kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakaohusisha nafasi za udiwani, uwakilishi, ubunge na urais, linafikiwa.
Mazungumzo bado yanaendelea vizuri. Hayajafikia tamati. Hivyo taarifa hizo ambazo zimeendelea kusambaa kwamba UKAWA ‘wameachiana au kugawana majimbo’ na kwamba kuna maeneo tayari yamepewa chama fulani na maeneo mengine mwafaka haujafikiwa, si rasmi wala si sahihi.
Kwa uzito wa hatua hiyo, mazungumzo yakikamilika na makubaliano kufikiwa, viongozi wakuu wa vyama vinavyounda UKAWA, kikiwemo CHADEMA, watatoa taarifa rasmi na sahihi kwa umma wa Watanzania ili Watanzania waelewe kwa ukamilifu uamuzi huo.
Wafuasi, wapenzi, wanachama na viongozi wa CHADEMA wanaendelea kufanya kazi za ujenzi na uimarishaji wa chama katika kila eneo kadri ya maagizo ya vikao vya chama, hususan kupitia program endelevu ya CHADEMA ni Msingi, operesheni mbalimbali mf; kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu mwezi Oktoba, n.k.
Katika shughuli za uenezi na uimarishaji wa CHADEMA, kwa kadri ya maagizo ya chama, viongozi waendelee kusimamia misingi ya ushirikiano wa UKAWA kwa ajili ya matumaini na haki za Watanzania ambao wanajiandaa kutimiza kiu yao ya kufanya mabadiliko kwa kuiondoa CCM madarakani kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Imetolewa leo Ijumaa, Machi 20, 2014 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
Next Post Previous Post
Bukobawadau