Bukobawadau

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI YATOA MAFUNZO YA UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA KWA MFUMO WA BVR MKOANI KAGERA

Tume ya Taifa ya Uchuguzi (NEC) leo tarehe 14 Mei, 2015 imeanza semina ya mafunzo ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura  kwa mfumo mpya wa uandikishaji uitwao “Biometric Voters Registraion (BVR)  kwa Maafisa Waandikishaji, Waandikishaji Wasaidizi na Maafisa Uchaguzi wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa ya Bukoba katika mkoa wa Kagera.
Katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mkuu wa Mkoa Kagera Mhe. John Mongella aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Jackson Msome aliwaasa Maafisa waliotarajiwa kupata mafunzo ya uandikishaji kwa mfumo mpya wa (BVR) kuzingatia mafunzo ili wakati ukifika wananchi wanaostahili kuandikishwa waweze kuandikishwa bila matatizo.
 Aidha Mkuu wa Mkoa wa Kagera aliwataka wanasiasa na viongozi wa vyama vya siasa kuwaacha watendaji kufanya kufanya kazi yao ya uandikishaji bila kuingiliwa wala kubughiwa ili zoezi liweze kufanikiwa kama inavyotarajiwa na kuwapa wananchi haki yao ya msingi muda ukifika ili waweze kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Pia Mhe. Mongella alivitaka vyama vya siasa kuhakikisha vinaweka wawakilishi wao katika vituo vya uandikishaji ili kuangalia zoezi zima linavyoendeshwa ili kama kutakuwepo nakasoro vyama hivyo vya siasa viweze kutoa ushauri ni wapi pa kurekebisha wakati zoezi linaendelea ili kusiwepo na malalamiko mara baada ya zoezi kuisha.
Viongozi wa siasa na Wakurugezi Watendaji wa Halmashauri na Manispaa ya Bukoba wamesistizwa pia kuhamasisha wananchi kwa njiaq mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wenye vigezo wanaandikishwa mara zoezi litakapoanza katika Halmashauri za wilaya ili kuyafikia malengo yaliyokusudiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Bw. Albert Macha Afisa kutoka kitengo cha uboreshaji wa Daftari la kudumu la Wapiga Kura akitoa ufafanuzi juu ya mfumo wa uandikishaji utakavyoendeshwa alisema kuwa kila Halmashauri tayari imebainisha jumla ya vituo vitakavyotumika kuandikisha wananchi na kila kata itatumia  siku saba za katika kuandikisha wananchi na vifaa vitahamishiwa katika kata nyingine.
“Tayari vifaa mbambali vya uandikishaji wa wananchi kwa mfumo mpya wa kielektroniki wa (BVR) vimewasili mkoani Kagera zikiwemo BVR zenyewe na fomu mbalimbali zitakazotumika katika uandikishaji wa wananchi na vimesambazwa katika Halmashauri zote za mkoa wa Kagera, aidha uandikishaji unatarajia kuanza tarehe 21.05.2015 katika mkoa wa Kagera”  Alisema Bw. Macha.
Next Post Previous Post
Bukobawadau