Bukobawadau

WAHAMIAJI HARAMU 23 KUTOKA NCHINI BURUNDI WAKAMATWA MKOANI GEITA

Wahamiaji haramu 23 kutoka nchini Burundi wamekamatwa na idara ya uhamiaji mkoa wa Geita wakiwa safarini kuelekea katika mikoa ya Shinyanga na Tabora kujitafutia hifadhi kutokana na hali tete ya usalama inayoendelea nchini mwao.

Akizungumza na ITV afisa uhamiaji mkoa wa Geita Charles washima amesema kati ya wahamiaji hao 23 mmoja ameshashitakiwa mahakamani na kuhukumiwa kwenda jela miezi tisa kutokana na kupatikana na hatia ya kuingia nchini kinyume cha sheria, aidha kati ya wahamiaji haramu waliokamatwa wengi wao ni watoto wadogo chini ya umri wa miaka kumi na nane ambapo  idara hiyo inaandaa utaratibu wa kuwafikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Baadhi ya wahamiaji haramu hao kutoka burundi wamesema wamelazimika kukimbia nchini mwao kutokana maisha magumu na hali ya vurugu zinazoendelea kwa wananchi kupinga rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunzinza kuingia katika awamu ya tatu ya kuwania kugombea kiti cha urais.

 Aidha mkuu wa kitengo cha udhibiti wa mipaka mkoa wa Geita Vitalis Komanya amewataka wananchi kutoa ushirikiano wa ulinzi wa mipaka ya nchi kutokana na kuwa wahamiaji wengi wao huingia nchini kwa kupitia njia za panya na kuhifadhiwa na wananchi hivyo kuhatarisha usalama.
ITV
Next Post Previous Post
Bukobawadau