Bukobawadau

VIONGOZI WA SERIKALI ZA MITAA WAONYWA KUTOCHAKACHUA ZOEZI LA UGWAJI WA VYANDARUA VYA BURE MKOANI KAGERA

Viongozi wa Serikali za Mitaa waonywa kutochakachua zoezi la ugawaji wa vyandarua vyenye viatilifu vinavyoua mbu waenezao malaria vinavyogawiwa na serikali kwa wananchi  bure katika nchi nzima ukiwemo mkoa wa Kagera  ili kutokomeza  maambukizi na ugonjwa wa malaria.
Viongozi hao walionywa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella wakati wa uzinduzi wa zoezi la kugawa vyandarua kwa wananchi  Mkoani Kagera katika Kata ya Kemondo Wilayani Bukoba Jumatano 12 Agosti, 2015.
Mhe. Mongella  aliwasistiza viongozi hao kusimamia zoezi la ugawaji bila kufanya ujanja  wa kutowatoza wananchi fedha  kiwango chochote kwani serikali imetoa vyandarua hivyo bure kwa kila mwananchi aliyejiandikisha hapo kabla na kupewa kadi ya kuchukulia chandarua.
Pia Mhe. Mongella aliwaeleza wananchi kuwa kila mmoja anastahili kupata chandarua hata ambaye hakupata fursa ya kujiandikisha hapo awali au alipoteza kadi yake atajiandikisha wakati wa zoezi  na kuhakikiwa na viongozi wake na atapewa chandarua .

Wananchi nao walionywa kutotumia zoezi hilo kufanya udanganyifu wa kujiandikisha zaidi ya mara moja kwa nia ya kuchukua vyandarua zaidi na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya vyandarua hivyo kama kufugia kuku, kuvua na kutengenezea vitalu vya miti.
Katika sensa iliyofanyika hapo awali ilibainika kuwa mkoa wa Kagera una jumla ya kaya 509,710 ambazo zitagawiwa jumla ya vyandarua 1,810,250 ambapo kaya moja inaweza kupata zaidi ya chandarua moja kwa kutegemea wanankaya waliopo na walioandikishwa wakati wa sensa.
Mratibu wa Malaria Mkoani Kagera Dk. Julian Mugengi akisoma taarifa katika uzinduzi huo alisema kuwa Mkoa wa Kagera umekuwa na historia ya milipuko ya malaria hasa katika Wilaya ya Muleba kwa miaka ya 1997, 1998, 2007, na mwaka 2013.
Dk. Juliani alisema kuwa katika  taarifa ya utafiti wa viashiria vya UKIMWI na Malaria ya mwaka 2007 ilionyesha kuwa mkoa  wa Kagera ulikuwa na maambukizi ya malaria  kwa asilimia 42% hadi 50% na mwaka 2010 kiwango hicho kilishuka hadi asilimia 10% hiyo ilitokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kwa mwaka 2015 wagonjwa waliopima katika vituo vya kutolea huduma maambukizi ya malaria yalikuwa juu kwa miezi ya Januari na Februari kwa watoto juu ya miaka 5, na watoto chini ya miaka 5 maambukizi yalikuwa asilimia 59.1%.
Aidha maambukizi ya vimelea vya malaria yalipungua kwa mwezi Marchi hadi Juni 2015 kutokana na unyunyiziaji wadawa ya ukoko majumbani uliofanyika katika Wilaya za Biharamulo Ngara na Muleba na kupunguza mambukizi hadi Julai 2015 watoto chini ya miaka 5 yalikuwa asilimia 25.7% na wakubwa asilimia 4.6% kwa wagonjwa waliopima katika vituo vya kutolea huduma.
Kauli mbiu ya mwaka huu 2015 inasema “Wekeza kwa Maisha ya Baadae, Tokomeza Malaria”  
Next Post Previous Post
Bukobawadau