Bukobawadau

BALOZI WA VATICAN NA MWAKILISHI WA PAPA NCHINI TANZANIA AWASILI MKOANI KAGERA KUFANYA ZIARA YA SIKU SITA


Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini Tanzania, Francisco Montecillo Padilla atembelea mkoa wa Kagera katika ziara ya kujione shughuli mbalimbali za Kanisa Katoliki mkoani zinavyotekelezwa pia na kutoa Baraka za pamoja kwa wakristo wa kanisa hilo.
Balozi Padilla akiwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa Kagera alipowasili kumsalimia aliishukuru serikali ya mkoa wa Kagera kwa kuwaunganisha wananchi wa Kagera  bila kujali imani zao ambapo wanafanya shughuli zao kila mmoja kwa imani yake  bila usumbufu wowote.
Pia Balozi Padilla alisema kuwa serikali inafanya kazi moja ya kuwaudumia wananchi pia na dini zinafanya kazi ya kuwahudumia wananchi hao hao kiroho kwa hiyo hakuna haja ya serikali na dini kugombana wala kukwaruzana kwasababu wote wanafanya kazi moja kwa wananchi.
“Ni bora kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya serikali na dini na nashukuru jambo hilo linatekelezwa mkoani Kagera, nimekuja kukagua shughuli mbalimbali hapa na kupata baraka za pamoja na wakristo wa mkoa wa Kagera ili kujenga jamii moja yenye familia moja katika kumtukuza Mungu.” Alimalizia Balozi Padilla.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera John Mongella akimkaribisha Balozi Padilla alimshukuru kwa kufanya ziara mkoani Kagera na alimweleza kuwa serikali inatambua juhudi za kanisa Katoliki katika kuleta maendeleo kwa wananchi hasa ujenzi wa shule na hospitali kama huduma za jamii kwa wananch,i pia kutoa huduma za kiroho zinazosaidia kukuza maadili katika jamii.
Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa chini Tanzania, Francisco Montecillo Padilla ziara yake imeanza leo Septemba 3, 2015 na anatarajia kuwepo mkoani hapa kwa takribani siku sita, aidha Balozi Padilla anatarajiwa kuongoza ibada takatifu ya maombezi ya Bikra Maria katika hija huko Nyakijooga Parokiani Mugana Wilayani Missenyi  tarehe 6.09.2015 siku ya Jumapili.

Na Sylvester Raphael
Next Post Previous Post
Bukobawadau