Bukobawadau

WADAU WAPONGEZA GOING BONGO

Rais wa Shirikisho la Filamu Simon Mwakifamba akiongea na vyombo vya habari wakati wa uzinduzi filamu ya ‘Going Bongo’ uliofanyika jana Ijumaa 

WADAU mbalimbali waliofika kwenye  onyesho la kwanza la filamu  ya mtanzania anayeishi nchini Marekani  wametoa sifa kemkema kuhusu filamu hiyo  inayokwenda kwa jina la ‘Going Bongo’ kwamba wamewataka wasanii wa hapa nchini waige mfano wake.
Wakizungumza baada ya kutoka kuaitazama ndani ya ukumbi wa cimema wa Cinemax Ijumaa usiku mkongwe katika filamu  Ibrahimu  Banane almaarufu kwa jina la  ‘Mzee Katembo’ alisema kwamba mtunzi wa filamu hiyo  amewashtua  wasanii wa hapa nyumbani na Afrika Mashariki kwa ujumla.
“Ametushtua  sisi kwamba  tutunge filamu na kuzicheza katika kiwango cha kimataifa na tuchukue muda mrefu ili kuweza kutunga na kurekodi filamu zetu kama tunataka kulikamata soko hilo na kujitangaza kwa ujumla endapo tu tutafuata nyayo za mtunzi wake Ernest Napoleon.” alisema Katembo.
Alisema m ameiangalia  filamu hiyo  inayokwenda kwa jina la  ‘Going Bongo’ ni nzuri  kila muigizaji amesimama  katika nafasi yake na kuuvaa uhusika vilivyo na endapo wasanii wa hapa nyumbani watataka kutengeneza filamu nzuri  wasiogope kuingia gharama  kama jinsi filamu hiyo inavyoonesha muandaaji alivyoingia gharama kwamba aimerekodiwa katika nchi mbili tofauti.
“Hapa nyumbani sisi tumezoea kuona kwamba msanii anafyatua  filamu mbili ndani ya mwezi mmoja jambo ambalo hupunguza ubunifu kwani ni vigumu kichwa kimoja kuweza kutoa kitu kizuri ndani ya mwezi mmoja” alisema Katembo.
Msemaji wa  Waigizaji  nchini Massoud Kaftani  aliimwagia sifa filamu hiyo na kusema kwamba wamepata somo kutoka kwa Ernest hivyo wanashukuru pia kwa kupata nafasi ya kuishuhudia filamu hiyo na kuahidi wkamba watafanyia kazi changamoto mbalimbali zilizo ndani ya tasnia ya filamu na maigizo nchini.
Wakati huohuo Rais wa Shirikisho la Filamu Simon Mwakifamba aliongeza kwa kusema kuwa yeye binafsi amevutiwa na filamu hiyo kutokana na kuzingatiwa kwa vina na  mpangilio mzuri, “hili ni jambo la kujivunia kama watanzania pia tunatoa wito kwa watanzania wengine wanao ishi nje ya nchi kujipanga na kuibua vipaji vyao kimataifa kama jinsi alivyotuonesha Ernest hivyo huko waliko nina imani na wao wameifuatilia  filamu hii ya Going Bongo ilete chachu kwa watanzania wanaoishi ughaibuni na wa hapa nyumbani wote tujipange kwa pamoja katika  kuikuza na kuiendeleza tasnia hii” alisema Mwakifamba.
Filamu hiyo ilishuhudiwa na wadau mbalimbali akiwamo Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’  huku akiitoa maneno ya kuisifa gfilamu hiyo na kusema kuwa muandaaji ametoa somo kwa wasanii wahapa nchini.
Filamu hiyo inayokwenda kwa jina la ‘Going Bongo’ ilioneshwa kwa mara ya kwanza kwenye ukumbi wa sinema wa Century Cinemax uliopo Mlimani City, Jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na mashabiki wengi ambao wengi wao walikiri kuvutiwa nayo.
Filamu hiyo ambayo mpaka sasa imetwaa tunzo kadhaa, pamoja na tunzo ya Ziff  ina maudhui ambayo yanonyesha maisha ya Daktari aliyejitolea kwenda kufanya huduma  nchini Tanzania kwa muda wa  mwezi mmoja huku mtunzi na muandishi  pia aliyeisimamia  katika kuitengeneza na kuigiza filamu hiyo ni  Ernest Napoleon .
Filamu hii imerekodiwa   majiji makubwa mawili ambayo ni Dar es Salaam na California  Marekani, inaelezea sehemu ya maisha ya kweli aliyonayo Daktari  mwenye asili ya nchini Ufaransa  aliyeondoka Ulaya na kwenda kufanya kazi  barani Afrika.
Kati ya tuzo ambazo filamu hii imeshinda ni pamoja na, Filamu Bora Afrika Mashiriki katika tamasha la Zanzibar International Film Festival (Ziff)  na Filamu Bora ya Kimataifa katika tamasha la ‘Black Entertainment Fashion’,  ‘Film and Television Awards’  (BEFTA)
Next Post Previous Post
Bukobawadau