Bukobawadau

TAARIFA YA TANZANIA BLOGGERS NETWORK (TBN) KWA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 02 DESEMBA, 2016 KATIKA UKUMBI WA IDARA YA HABARI (MAELEZO)


Ndugu Mwakilishi kutoka Benki ya NMB,
Waandishi wa habari,

Kwa niaba ya Chama cha Wamiliki/Waendeshaji wa Mitandao ya Kijamii nchini 'Tanzania Bloggers Network' (TBN) napenda kuwashukuru kwa kujitokeza katika mkutano huu muhimu. TBN inajua kuwa mnamajukumu mengi ya kuujuza umma masuala anuai, lakini mmechagua kuja kwetu ili kutusikiliza tulichowaitia na baadae tunaamini mtaujuza umma juu ya tukio letu.

TBN iliosajiliwa rasmi na Serikali mwezi Aprili, 2015 kwa kushirikiana na wataalam wa masuala ya habari na mitandao ya kijamii imeandaa semina kwa wanahabari hawa wa mitandao ya kijamii hasa 'Bloggers' itakayofanyika jijini Dar es Salaam. Semina hii maalumu ambayo itajumuisha mafunzo ya siku mbili yaani tarehe 5 na 6 ya Mwezi Desemba, 2016 kwa washiriki takribani 150 kutoka Tanzania nzima (Bara na Visiwani) itafuatiwa na mkutano mkuu kwa wanachama hai wa TBN kujadili masuala mbalimbali ya chama na tasnia nzima ya mitandao ya jamii.


Ndugu Wanahabari,
Katika mkusanyiko huu wanatasnia watapewa semina juu ya uendeshaji mitandao ya jamii kwa manufaa, upashaji habari kwa kutumia mitandao yao kwa kuziangatia maadili na namna ya kunufaika na mitandao hiyo kwa waendeshaji (kujipatia kipato) hasa ukizingatia kuwa wapo baadhi yetu tunaifanya kama ajira nyingine. Kimsingi lazima tukubali kuwa mitandao hii imekuwa tegemeo kubwa la kusambaza habari mbalimbali tena kwa muda mfupi tangu kutokea kwa tukio fulani, hivyo kuna kila sababu ya kuendelea kuwapiga msasa wanaoiendesha ili kupunguza matumizi mabaya ya mitandao hii.

TBN inaamini njia pekee ya kupambana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ni kuendelea kutoa elimu kwa waendeshaji na watumiaji ili mwisho wa siku wasikubali kutumika vibaya au kuitumia vibaya mitandao hii katika kutoa taarifa. Kwa dunia ya sasa hakuna atakayepinga kuwa mitandao hii imekuwa ikielimisha umma, ikikosoa jamii na kiburudisha juu ya masuala anuai ya kijamii
TBN inapenda kutoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Nne na Tano chini ya Mh. Rais John Pombe Magufuli kwa ushirikiano alioanza kuuonesha hasa kwa kutambua mchango wa mitandao hii ya kijamii na hata kuitumia katika utoaji wa taarifa zao. Kimsingi hii ni hatua nzuri na ya kuigwa hasa katika ulimwengu huu ambapo dunia imekuwa kama kijiji kutokana na hatua ya maendeleo ya habari na mawasiliano.

Ndugu Wanahabari,
Kwa kulitambua hili mnaweza kuona hata taasisi nyeti kama Ikulu nayo ina Blogu maalumu kwa ajili ya kutoa taarifa kwa umma, Idara ya Habari Maelezo nayo ina Blogu kwa ajili ya kutoa taarifa kwa umma juu ya masuala mbalimbali yanayopaswa kutolewa kitaarifa kwa jamii. Jambo la kujivunia zaidi kwa maendeleo ya mitandao hii hata Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Nape M. Nnauye amekuwa mstari wa mbele kuona umuhimu wa mitandao ya kijamii hasa blogu na hata kuzitumia katika kupasha habari umma. Hata katika mkutano wetu wa kesho kutwa ndiye tunayemtarajia kuwa mgeni rasmi atakayetufungulia mkutano huo.
Ndugu Wanahabari,
Kwa namna ya pekee TBN inapenda kutoa shukrani za pekee kwa Benki ya NMB kwa kukubali kuwa wadhamini wa kuu wa mkushanyiko huo wa 'bloggers' kutoka maeneo mbalimbali ya mikoa yetu. Kitendo cha kujitolea kufanikisha jambo hili kinaonesha namna gani NMB inavyowajali wananchi katika masuala mbalimbali ikiwemo hili la upashanaji habari kwa jamii.

Kama hiyo haitoshi tunapenda kuwashukuru wadhamini wengine ambao ni NHIF, SBL, PSPF na Coca Cola ambao wamejitolea kuungana nasi katika kufanikisha tukio hili la kuwaleta pamoja bloggers na kutoa mafunzo kwao. Tunaamini tutakuwa nao siku zote katika masuala mengi ya maendeleo ya tasnia ya mitandao ya kijamii.
Imetolewa na; Mwenyekiti wa Muda wa TBN
Joachim E. Mushi
0756469470
Next Post Previous Post
Bukobawadau