Bukobawadau

MKUU WA MKOA ASHUTUSHWA NA UHARIBIFU MKUBWA WA MISITU YA HIFADHI YA TAIFA MKOANI KAGERA AHAIDI KUINUSURU MISITU HIYO

MKUU WA MKOA ASHUTUSHWA NA UHARIBIFU MKUBWA WA MISITU YA HIFADHI YA TAIFA MKOANI KAGERA AHAIDI KUINUSURU MISITU HIYO
Na: Sylvester Raphael
Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuinusuru Misitu ya Hifadhi ya Biharamulo, Nyantakala Wilayani Biharamulo na Msitu wa Hifadhi wa Rwiga Wilayani Muleba ambayo imeharibiwa kwa kiwango kikubwa na shughuli za kibinadamu ambazo ni kilimo, ufugaji, ukataji wa mbao na uchomaji wa mkaa katika misitu hiyo.

Meja Jenerali Mstaafu Salum Mstafa Kijuu Mkuu wa Mkoa wa Kagera alitembelea Misitu hiyo ya Hifadhi za Taifa tarehe 30 hadi 31 Januari, 2017 na kujionea uharibifu mkubwa katika misitu hiyo unatokana na shughuli za kibinadamu zinazofanyika kinyume cha sheria.

Mhe. Kijuu alishuhudia eneo la Msitu wa Hifadhi wa Biharamulo katika Kijiji cha Kabale  Kata Rusahunga mita chache kutoka barabara kuu iendayo Dar es Salaam kunaendeshwa kilimo cha mpunga na mahindi katika chanzo cha maji na kupelekea uhaba mkubwa wa maji kutoka katika chanzo hicho kwa sababu ya umwagiliaji unaofanyika kumwagilia mazao hayo.
Katika Misitu hiyo ya Biharamulo na Nyantakala shughuli kuu zinazoendeshwa ni kilimo cha mpunga na mashamba makubwa ya mahindi pia na uchomaji wa mkaa ambapo imepelekea miti mingi kukatwa na kuacha misitu hiyo ikiwa wazi wakati ikiwa ni kinyume cha sheria.

Mkuu wa Mkoa alishuhudia baadhi ya wananchi wakiwa wanaendelea na kilimo ikiwa ni pamoja na kufyeka miti kwa ajili ya kuandaa mashamba katika misitu hiyo. Aidha, imefikia hatua baadhi ya wananchi wameanza kuwakodisha wananchi wenzao ardhi ya kulima katika misitu hiyo ya hifadhi na wanawatoza fedha.
Katika Msitu wa Hifadhi wa Rwiga Wilayani Muleba uharibifu mkubwa unatokana na ukataji miti kwaajili ya uchomaji wa mkaa na ukataji wa mbao ambapo ukiangalia katika maeneo yaliyopo karibu na barabara utaona miti lakini katikati ya msitu uharibifu ni mkubwa sana jambo linalihashiria kuwa kama hatua hazitachukuliwa msitu huo unaweza kuisha ndani ya muda mfupi ujao.

Kutokana na uharibifu huo mkuu wa mkoa wa Kagera alitoa maagizo sita kwa Halmashauri za Wilaya za Biharamulo na Muleba pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kuwa; Kwanza,  kuanzia sasa Halmashauri hizo zishirikianae na Wakala wa Huduma za Misitu katika kufanya doria za mara kwa mara kuhakikisha katika misitu hiyo hakuna shughuli za kibinadamu zinazoendelea.

Pili, kufyeka mazao yote yaliyopandwa katika chanzo cha maji eneo la Kijiji Kabale kata ya Nyakanazi Wilayani Biharamulo ili kukitunza chanzo hicho amabacho kinamwaga maji yake katika Ziwa Victoria pia na maji yake kutumika kuwasaidia wananchi katika matumizi ya kawaida.

Tatu, Wananchi wote waliolima katika Misitu ya Hifadhi ya Taifa watambuliwe mara moja na kuandkiwa barua ya kuacha mara moja kuendesha shughuli za kilimo katika misitu hiyo. Aidha Mkuu wa Mkoa aliwaruhursu wananchi hao kuvuna mazao yao ambayo wamelima katika misitu hiyo  na mara baada ya kuvuna wasiruhuswe tena kulima isipokuwa wapande miti ya asili kuirejesha ile waliyoikata.

Nne, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania waandike vibao vikubwa vinavyoonyesha kuwa hairusiwi kufanya shughuli zozote za kibinadamu katika Hifadhi za Misitu za Taifa. Pia watoe eimu kwa wananchi wanaozunguka katika hifadhi hizo kueleza umuhimu wa kuitunza misitu hiyo.

Tano, zifanyike operesheni za mara kwa mara  katika misitu hiyo ili kuliinda na uharibifu wa shughuli za kibinadamu jambo amabalo linapelekea hali ya hewa kubadika na kuleta majanga kama ukame kwasababu ya kukata miti hovyo.

Sita, Halmashauri za Wilaya za Biharamulo na Muleba  ziliagizwa kuweka vizuizi vya barabarani vya kustukiza mara kwa mara ili kukamata mkaa unaobebwa na Baiskeli na pikipiki mara baada ya magari kuwa yanakamatwa mara kwa mara na ikaanza kutumika mbinu ya kutumia pikipiki, pia kuwakamata wafanyabiashara wa mkaa wote ambao hawana leseni za biashara hiyo.

Angalizo; Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu alitoa angalizo kwa viongozi wa ngazi zote katika maeneo hayo na watumishi wananohusika na utunzaji wa Misitu ya Hifadhi ya Taifa kuwa hatasita kuchukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria na kuwafukuza kazi kwa yeyeyote ambaye atalichukulia suala hilo kimzaa bila kutimiza wajibu wake.

Bi Hafsa Galitano Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo alimshukuru sana Mkuu wa Mkoa kwa kuingilia kati suala hilo la uharibifu wa Misitu ya Biharamulo na Nyantakara na alisema Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ndiyo waliopelekea misitu hiyo kufikia kiwango hicho cha uharibifu kutokana na migongano wao na Halmashuri.

“Mkuu wa Mkoa nakushukuru sana Wakala wa Huduma za Misitu ndiyo waliotufikisha hapa, lakini kwa maagizo yako Mkuu sisi tupo tayari kushirikiana kikamilifu nao na kuanzia sasa hatutakubali misitu yetu iharibiwe tena. Alimalizia Bi Hafsa Galiatano.
Naye Kaimu Meneja Wakala wa Huduma za Misitu Kanda ya Ziwa Bw. Hamza Omari alisema kuwa ofisi yake itashirikiana na Halmashaurikikamilifu katika  kuilinda Misitu ya Hifadhi. Aidha, alisema kuwa baada ya Ofisi yake kusaini randama ya makubaliano na Ofisi ya Rais TAMISEMI hakuna tena mkanganyikokati ya ofisi yake  na Halmashauri.
Wito, kutokana na tabia nchi kubadilika duniani kote na hasa katika mkoa wetu wa Kagera ambako tumekuwa tukipata mvua karibu kwa mwaka mzima lakini mwaka 2016 hali ya ukame imeukumba mkoa wetu wa Kagera pia na nchi nzima, wananchi tunao wajibu mkubwa wa kuhakikisha tunalinda misitu yetu ya hifadhi ili kulinda mazingira.

Kwa upande wa mifugo Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu alisema utaratibu unaandaliwa wa kuondoa mifugo yote katika Misitu na Mapaori ya Hifadhi za Taifa na ukikamilika Serikali itatangaza jinsi ya zoezi la kuondoa mifugo hiyo litakavyofanyika .
Next Post Previous Post
Bukobawadau