Bukobawadau

WAKULIMA WANUIA KULIFANYA ZAO LA VANILLA KUWA MBADALA WA KAHAWA NA CHAI NA KUINUA TENA UCHUMI WA MKOA WA KAGERA

Wananchi wa Mkoa wa Kagera wanuia kulifanya zao la Vanilla kuwa zao mbadala wa mazao ya biashara mkoani hapa ambapo mazao hayo ambayo ni Kahawa na Chai yalikuwa mazao makuu ya kibiasahara yaliyochangia katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Kagera.
Zao la Vanilla huenda likawa zao mkombozi kwa wananchi wa mkoa huu baada ya kupata soko na kuwa na bei nzuri hasa katika soko la dunia jambo linalohamasisha kilimo chake ambapo kwa sasa vanilla mbichi inauzwa Shilingi 70,000/= hadi 100,000/= kwa kilo moja .
Mara baada ya Kuonekana kuwa zao la Vanilla linaweza kuwa mkombozi wa uchumi wa Mkoa wa Kagera uongozi wa mkoa uliamua kuitisha kikao cha wakulima na wadau wa Vanilla ili kuweka mikakati thabiti wa jinsi ya kulifanya zao hilo kuwanufaisha wakulima na kukuza uchumi wa Mkoa wa Kagera.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Deodatus Kinawilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera alisema kutokana na zao la Kahawa na Chai kuanguka bei na kusababisha kuyumba kwa uchaumi wa wananchi sasa zao la vanilla linaweza kuwa mkombozi na kuuinua mkoa wa Kagera kiuchumi tena.
Katika kikao hicho kilichoratibiwa na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Bw. Adam Swai alisema dhumuni kubwa ilikuwa ni kuwaleta pamoja wakulima, wanunuzi na wadau wote wa zao la vanilla ili kuweka mikakati ya pamoja kuhakikisha zao hilo linakuwa na mfumo rasmi hasa katika kautafuta masoko na jinsi ya kuwaendeleza wakulima ili wanufaike.
Wakulima na wadau wa vanilla walikubaliana kuwa sasa zao la vanilla lipewe kipaumble katika mkoa wa Kagera kama zao kuu la biashara. Pili, yaruhusiwe tu makampuni yaliyosajiliwa na kupata reseni za biashara za kununua vanilla. Tatu, bei ya vanilla itangazwe kwa maoteo mapema kulingana na maoteo ya soko la dunia na kama bei ya soko la duni ikiwa ubwa kuliko iliyotangazwa na makampuni hayo awali wakulima walipwe malipo ya pili.
Wanunuzi halali wa vanilla yaani Makampuni yalenge kumuendeleza mkulima na siyo kupatikana wakati tu wa ununuzi wa vanilla ili kuhakikisha wakulima hao wananufaika na kilimo chao kuliko kuwaacha wanahaingaika na kupelekea kuuza vanilla zao kwa bei ndogo kwa kurubuniwa na wajanja wachache.
Aidha, Serikali iwadhibiti wanunuzi kutoka nchi jirani ambao wanawarubuni wakulima na kununua vanilla zao kwa bei ndogo na kukwepa kulipa ushuru na kodi na kupelekea kuikosesha Serikali mapato yake. Serikali ilitakiwa na wadau wa zao la vanilla kudhibiti magendo ya vanilla ili zao hilo lisije kuwa kama mazao ya kahawa yanayotoreshewa nchi jirani.
Katika hatua nyingine mwanzilishi wa kilimo cha vanilla na Meneja Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Wakulima (MAYAWA) katika Mkoa wa Kagera Bw. Charles Kamando alisema zao la vanilla lilianza kulimwa mkoani Kagera kuanzia mwaka 1997 baada ya zao hilo kuletwa na vijana wawili kutoka Nchini Uganda waliokuwa wanafanya kazi katika shamba la Mzungu.
“Kilimo cha zao la Vanilla kilianza mwaka 1932 nchini Uganda lakini mwaka 1997 vijana wawili wa Kitanzania waliiba marando na kuja nayo Mkoani Kagera na ndipo hapo kilimo cha vanilla kilianza kwa shirika letu na tulianza kuwafundisha wakulima 85 na ndiyo mwanzo wa vanilla kuanza kulimwa Mkoani Kagera na nchini Tanzania.” Alitoa historia Bw. Kamando
Kwa sasa MAYAWA ndilo shilrika halali ambalo linajishughulisha na kuwafunza wakulima Mkoani Kagera kulima vanilla, kununua vanilla zinazozalishwa na wakulima, kuzikausha vanilla hizo kwa viwango vinavyohitajika na kutafuta masoko hasa katika soko la dunia. Kikao hicho kiliketi tarehe 28.04.2017 na vikao kama hivyo vitakuwa vinafanyika mara tatu kwa mwaka kila mwaka.
Zao la vanilla linatumika katika matumizi mbalimabli kama vinywaji, madawa ya binadamu, vyakula na vitafunwa pamoja na manukato mablimbali.
Next Post Previous Post
Bukobawadau