Bukobawadau

WAFUGAJI MKOANI KAGERA WATAFUTIWA UFUMBUZI WA MALISHO YA MIFUGO YAO.

Mkuu wa Mkoa ametoa taarifa kwa vyombo vya Habari juu ya suala hilo kama ifuatavyo:

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI  TAREHE 13 SEPTEMBA, 2O17
Ndugu Waandishi wa Habari, Nimewaiteni hapa ili kutoa maagizo na Maamuzi ya Serikali juu ya ubainishaji na uendelezaji wa nyanda za malisho katika eneo la Mwisa II katika Wilaya za Muleba na Karagwe. Uendelezaji wa eneo la Mwisa II kwa ajili ya ufugaji ni mpango ulioanza miaka ya nyuma na ulianza kwa mradi wa kuzuia ndorobo ulioendeshwa na Wizara yenye dhamana ya Mifugo kwa wakati huo kwa lengo la kuufanya uwanda wa Mwisa II kuwa na ufugaji wenye tija na endelevu. Eneo la Mwisa II ni eneo linaloanzia katika mipaka ya Ranchi ya Kagoma, kupitia Bonde la Ziwa Burigi hadi Pori la Akiba la Burigi.
Ndugu Waandishi wa Habari, Lengo la uendelezaji wa eneo la Mwisa II ni kuviendeleza vijiji vinavyogusa eneo la Mwisa II na kuongeza kipato kwa kupunguza umasikini kwa wananchi katika ngazi za Vijiji, Halmashauri husika, Mkoa na Taifa kwa ujumla. Mpango huu ni fursa kwa Mkoa wa Kagera kujikwamua kiuchumi na kutoka nafasi unaoshika kwa sasa ambayo ni ya tatu toka chini kwa kipato Kitaifa.
Mpango huu utaondoa ufugaji holela na ukataji wa miti ovyo na kuwezesha uzalishaji mifugo kisasa na kibiashara bila kuharibu mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. Pia, mpango huu unatarajiwa kuwezesha upatikanaji wa maeneo ya malisho kwa ajili ya wafugaji wa Kitanzania walioondolewa kwenye Misitu ya Hifadhi na Mapori ya Akiba na hivyo kutatua migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Ndugu Waandishi wa Habari, Mpango huu wa uendelezaji wa Mwisa II ni utekelezaji wa Maagizo na Maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Serikali ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Rais wakati wa ziara yake Mkoani Kagera mwezi Julai, 2017 ambaye alisisitiza hifadhi endelevu ya Misitu ya Hifadhi na Mapori ya Akiba na wananchi kupunguza mifugo yao na kufuga kisasa na kibiashara kufuatana na ardhi waliyonayo.
Aidha, utekelezaji wa mpango huu unaenda sambamba na Maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Makamu wa Rais mwaka 2016 kwa Mikoa kutenga maeneo ya wafugaji pindi agizo litakapotolewa la kuondoa mifugo toka kwenye maeneo ya Hifadhi ambapo Mkoa uliainisha eneo la Mwisa II kuwa ni nyanda za malisho. Aidha, Mwezi Juni 2017, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokutana na Maafisa Mifugo wa Mikoa na Halmashauri zote Tanzania Mkoanii Dodoma aliagiza maeneo ya wafugaji yatengwe, yapimwe na yamilikishwe kwa wafugaji.
Ndugu Waandishi wa Habari, Mpango huu wa uendelezaji wa Mwisa II utawezesha upatikanaji endelevu wa mali ghafi za viwanda vya nyama, maziwa na bidhaa zake, ngozi na bidhaa zake na kadhalika. Pia mpango huu ni utekelezaji wa Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya uwekezaji wa viwanda ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na kuongeza ajira kwa Watanzania.
Ndugu Waandishi wa Habari, (angalizo) Ili kutekeleza azima ya uendelezaji wa eneo la Mwisa II hatua mbalimbali zitatekelezwa bila kuathiri mipaka ya Vijiji, kunyang‘anya ardhi ya Vijiji au kuathiri miradi iliyopo ikiwa ni pamoja na mradi wa umwagiliaji wa IKAKI unaogusa vijiji vya Itunzi, Kashalala na Kiteme. Hatua hizo ni kama zilivyoainishwa hapa chini:-
Ndugu Waandishi wa Habari, Hatua ambazo tayari zimechukuliwa au zitakazochukuliwa ni kama ifuatavyo: Kwanza Timu ya Wataalam ngazi ya Wizara, Mkoa, na Halmashauri husika tayari imekutana na wajumbe wa Halmashauri za Vijiji na Madiwani kwa ajili ya kuwaelimisha juu ya zoezi la ubainishaji wa eneo la Mwisa II katika maeneo yao na elimu inaendelea kutolewa. Pili, Wataalamu kwa kushirikiana na Watendaji wa Vijiji na viongozi wa Vijiji wanaendelea kubaini eneo la Mwisa II na kuliwekea alama kwenye mipaka ya nje.
Tatu, Baada ya Timu kukamilisha hatua mbili za mwanzo eneo la Mwisa II litagawiwa katika Vitalu kwa kuweka alama kulingana na jiografia ya eneo husika, upatikanaji wa nyanda za malisho, maeneo ya maji, maeneo ya makazi, huduma za kijamii na miundombinu mbalimbali inayopatikana katika eneo hilo.
Ndugu Waandishi wa Habari, Hatua ya Nne itakuwa ni kukamilisha kazi ya Upimaji kwa kutumia (GPS set). Tano, ni kusajili vitalu na kuvipa namba za usajili utakaofanywa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Hatua ya Sita na ya mwisho itakuwa ni ushirikishwaji kuanzia ngazi za Vijiji, Wilaya na Mkoa kwa kuwatambua wananchi watakaopendekezwa kumilikishwa vitalu aidha, kipaumbele kitakuwa kwa Wanavijiji watakaojiunga katika ushirika wa wafugaji.
Ndugu Waandishi wa Habari, (Maagizo) Ili kufanikisha mpango huu ambao upo kwa ajili ya faida ya wananchi, Vijiji husika, Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla naagiza yafuatayo yatekelezwe;
Moja, Viongozi, Watendaji na Wataalam wa ngazi zote washirikiane wakiwa na msimamo na Dira moja.
Pili, Waheshimiwa Mawaziri wa Sekta zinazohusika naomba watoe ushirikiano na uwezeshaji unaohitajika ikiwemo Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Kagera, na Wawakilishi wengine wa Wananchi.
Ndugu Waandishi wa Habari, Mwisho napenda kuwakumbusha wananchi wote kuwa ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwajibika ipasavyo katika kulinda, kuhifadhi na kutunza maliasili za misitu, Mapori ya Akiba, Maeneo ya Hifadhi na vyanzo vya maji ili kuepusha Mkoa wetu kugeuka jangwa na kuendeleza ufugaji wenye Tija na Kibiashara.
Ilitolewa na; Mhe. Meja Jenerali (Mst) Salum M. Kijuu
Mkuu wa Mkoa
KAGERA
13 Septemba, 2017
Next Post Previous Post
Bukobawadau