SEARCH -TAFUTA

.

SIR.LOOM INC

11 January 2018

ANAANDIKA MH.JIMMY NAIBU MEYA MANISPAA BUKOBA

Kupitia akaunti yake ya faceboo Mh. Jimmy Karugenzi anasema;"TUWEKE MAMBO SAWA"
Nimekutana na mwananchi mmoja akaniuliza swali 
"Mh. Naibu Meya, eti ni kweli madiwani wa manispaa ya Bukoba mmemkataa mwekezaji anayetaka kuwekeza $ milioni moja katika manispaa yetu ya Bukoba"
Kwa sababu swali hili nimekuwa nikiulizwa na watu wengi napenda kuliweka jambo hili wazi na wana Bukoba manispaa mnaweza jua ukweli kuhusu jambo hili na mnaweza tupa ushauri maana mji huu ni mali yenu ili tufanye maamuzi yaliyo bora kama tutaona inafaa.
Ni kweli kwamba hata kabla ya kipindi chetu yupo mzungu mmoja mmarekani ambaye ni Profesa wa mambo ya kale amekuwa akiomba apewe eneo la wazi ambalo linajulikana sana kwa jina la Bukoba Club au Gymkana ili ajenge jumba kubwa litakalohusisha kutunza na kufanya maonyesho ya mambo ya kale ya mkoa wetu wa Kagera. Jumba hili litakuwa na kumbi na hotel ndani. Profesa huyu amekuwa kwa miaka mingi akifanya tafiti kuhusu mambo ya kale ya mkoa huu na ameandika pia vitabu kuhusiana na jambo hili. Hivyo aliona ni vema pia akafanya project ya ujenzi wa makumbusho na kwa kushirikiana na idara ya maendeleo jamii ya ofisi ya RAS Kagera walileta maombi ofisi ya mkurugenzi wa manispaa ili wapewe eneo hilo la wazi nililolitaja maana upangaji na ugawaji wa maeneo katika matumizi ni kazi ya ofisi ya mkurugenzi kupitia halmashauri yake.
Ni ukweli kuwa jambo hili ili lipate baraka lililetwa katika vikao vya kamati mbali mbali husika na hata katika baraza la madiwani kwa majadiliano na vibali.

MKWAMO ULIPO
Kamati husika na hata baraza la madiwani halikuridhia utoaji wa eneo hilo na badala yake walitoa ushauri kwamba ni vizuri eneo hilo libaki kwa matumizi yake ya awali yaliyokusudiwa ambayo ni kuwa eneo la burudani na michezo na mwekezaji atafutiwe eneo jingine aweze kuweka mradi wake ambao hata halmashauri inaupenda lakini inaonekana kama mwekezaji anapenda apewe eneo hilo hilo tu na si vinginevyo.
Ndugu zangu wana Bukoba, nyie ni mashahidi kwamba mji wa Bukoba hauna eneo lolote jingine la wazi lililobaki kwa ajili ya shughuli za kijamii kama mikusanyiko, michezo na burudani na mapumziko zaidi ya eneo hili.
zamani tulitumia uwanja wa Kaitaba na uwanja wa Uhuru platform populary known as uwanja wa Mayunga. Viwanja hivi sasa havitumiki baada ya kuzuiwa tokana na matumizi mengineyo. Kiwanja cha kaitaba baada ya kuwekewa nyasi bandia kimebaki kama kiwanja cha michezo mikubwa. Lakini viwanja vinavyoombwa ndivyo pekee vilivyo wazi kwa watu kwenda kufanya shughuli za burudani za michezo. Vijana wetu wanahitaji viwanja vya michezo. Shule zetu nyingi zina maeneo finyu kiasi cha kukosa maeneo ya kuweka viwanja vya michezo na eneo hili bado linaweza tumiwa na vijana hawa kujifurahisha katika michezo. Eneo jingine katika eneo hilo lina ukumbi wa Bukoba club ambayo pia bado inadai kulimiliki. Kwa sababu hiyo ushauri wetu kwa mwekezaji wetu mpendwa ilikuwa ni kumpa eneo jingine kwenye maeneo yetu katika mradi wa viwanja 5000 lakini ameendelea kushikilia kupewa eneo hilo hilo. Sisi madiwani hatuwezi kuwa wajinga kiasi hicho cha kukataa pesa nzuri kama hiyo kuwekezwa katika manispaa. Lakini tunaogopa sana pia kuwekeza eneo hilo na kuacha wananchi wakikosa eneo la kutumia katika shughuli zao za kijamii. Wote mnakumbuka katika siku za karibuni eneo hili ndio linatumika hata katika mikutano mbalimbali maana hakuna eneo jingine linaloweza beba wana Bukoba.
Tunaupenda uwekezaji ambao hautaleta pia usumbufu mwingine ambao hatutaweza kuujibu. Tusingependa kuhesabiwa dhambi ya kusababisha wana Bukoba kutokuwa na maeneo ya wazi. Lakini tuko tayari kabisa kukaa chini na mwekezaji huyu na wengine wote watakaokuja na mawazo mazuri ya namna bora ya kufanya uwekezaji bila ya kuathiri eneo lile. 
KWA MANENO HAYA MACHACHE NITAKUWA NIMEJIBU WENGI WALIOKUWA WAKITEGEMEA KUNIULIZA.
ASANTENI
Nakaribisha maoni na mawazo mengine.

2 comment:

Prudence Karugendo said...

Kama sikosei huyo atakuwa mwalimu wangu katika kitengo cha Akiolojia UDSM ambaye pia aliwahi kuishi miaka 2o Bukoba akifanya utafiti. Hapa tunapaswa kutofautisha mambo mawili, umuhimu wa jambo analotaka kufanya kwetu na umuhimu wa maendeleo yetu kama manispaa. Sioni kama ni suala la kujenga jumba la makumbusho, sababu yoyote ya yeye kulazimisha eneo analolitaka yeye. Sababu hata akipewa eneo kule Kabuhara Beach bado analolenga kulifanya litafanyika tu. Kuubadilisha mandhari mji wetu ni kitu kisichokubalika, hata kwao anakoto mambo yako hivyo.

Wazo ni zuri, ila liwe na halisia ya kweli, tutakuwa watu wa ajabu kumkubalia mtu afanye anavyojitakia eti kisa anatuletea maendeleo. Hatupaswi kukuballi tu kienyeji kisa mtu wa nje anatuletea maendeleo.

Maendeleo yaliyo bora yanatakiwa yawe na mchango wetu.

daniel mutta said...

Mh. Jimmy, mimi ni mzawa wa bukoba na ninapenda kushauri ifuatavyo. Moja ya njia mwafaka kupata maeneo kwa maendeleo ya bkb ni kulihamisha geteza kuu la bkb. Magereza hayajengwi katikati ya miji. Angalia ilipo segerea dsm au butimba mza nk. Kwa mji wa eneo dogo kama bkb iliyozungukwa na milima hapa lilipo gereza siyo mahali pake. Na ndiyo maana hata uwanja wa ndege iliamriwa ujengwe omukajunguti. Eneo hilo likiachwa na prison mnaweza kuamua litumiwe vipi lkn hilo gereza likibaki pale upanuzi wa bkb ni ndoto. Ni vzr mkoa ukaanza maxungumzo na serikali kuu ili kupata ufumbuzi kwa maslahi ya maendeleo ya wana bkb. Daniel Paul

 

WASILIANA NASI KUPITIA 0715505043 / 0784505045 0768397241 / 0754505043

.

SIR.LOOM INC & MC BARAKA

.

IDADI YA WATU