Bukobawadau

AWEKEZA KATIKA KILIMO CHA KISASA MKOANI KAGERA SASA APATA SOKO KULIKO ANAVYOZALISHA NJOO UWEKEZE KAGERA PENYE SOKO LA BIDHAA ZAKO

Na: Sylvester Raphael
Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti aendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji Kagera na kuendelea kuweka msukumo na kuhamasisha wawekezaji ambao tayari wamewekeza mkoani humo kuchapa kazi kwa bidii sana na kuendelea kuzalisha bidhaa mbalimbali ili kukuza uchumi na kuifanya Kagera kuwa kitovu cha biashara na uchumi wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Ni baada ya kutembelea mashamaba ya mwekezaji mzawa wa Kagera Bw. Fidelis Christian Bashasha anayewekeza katika kilimo cha mpunga mweupe, mahindi na alizeti Bugorora Wilayani Missenyi na anamiliki kampuni ya Global Agency Limited ambayo ilipata mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwaajili ya kilimo cha kisasa.
Mkuu wa Mkoa Gaguti baada ya kutembelea na kuona mashamba na mitambo ya mwekezaji huyo alimpongeza Bw. Bashasha na Kampuni yake kwa kushirikiana vizuri na wananchi ambao wamezunguka eneo lake la uwekezaji kwa kuwapatia mbegu bora na soko la kuuza mazao yao.
“Huyu ni mwekezaji ni mzawa na amekuja kuwekeza nyumbani kwahiyo sisi sote tutanufaika, wito wangu ni kwa wawekezaji wengine kuja kuchangamkia fursa kama tulivyoziainisha kwenye kitabu cha mwongozo wa uwekezaji ambao ulizinduliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa katika Wiki ya Uwekezaji Kagera Agosti 14, 2019.” Alisisitiza Mhe. Gaguti
Bw. Fidelis Christian Bashasha alianza uwekezaji katika kilimo cha kisasa miaka sita iliyopita na amekuwa akipata ushirikiano wa kutosha katika uongozi wa Serikali ya Mkoa na Wilaya na hajawahi kupata changamoto yoyote wakati akiandaa mashamba yake na sehemu ya kujenga kiwanda Omukajunguti.
“Tayari tumefanya majaribio ya mazao matatu ambayo ni mpunga mweupe, alizeti na mahindi, mazao hayo yanakubali kwa eneo la shamba letu na kazi ya kuondoa maji na kufanya ulinganisho wa shamba umekalilika mwaka huu tumelima ekari 3000 kwa msimu huu wa vuli na tunatarajia kuvuna zaidi ya tani 120 na tumepata soko nchini Rwanda wanahitaji tani 30,000.” Alieleza Bw. Bashasha
Bw. Bashasha anajenga kituo cha kukusanya mazao yakiwemo ya wananchi na kituo hicho kitakuwa na kiwanda cha kukausha na kusindika mazao hayo kabla ya kusafirishwa na kupelekwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Next Post Previous Post
Bukobawadau