MKUU WA WILAYA YA KARAGWE AITAKA KDCU IJIPANGE KUKABILI NGUVU YA SOKO HURIA
Mwenyekiti wa KDCU Prospery Mulungi akifungua Mkutano Mkuu wa chama hicho siku ya Jumanne.
Mrajisi Msaidizi wa vyama vya Ushirika Mkoani Kagera Rwenkiko Shorosi akijadili jambo na Mwenzake baada ya kupitia taarifa mbalimbali zilizowasilishwa kwa ajili ya kujadiliwa na wanachama.
Mjumbe kutoka Chama cha Msingi cha Kayanga Adventina Costantine akionyesha uwezo wake wa kujenga hoja ya kutetea masirahi ya wakulima wa kahawa.
MC mwendesha kikao akiwa tayari kupokea maelekezo kwa ajili ya shughuli ya leo
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera Darry Rwegasira
amekishauri chama cha Ushirika cha Wilaya hiyo(KDCU)kuacha kufanya biashara ya
kahawa kwa mazoea ili kiweze kukabiliana na nguvu ya ushindani katika soko
huria.
Akifungua Mkutano Mkuu wa 26 wa chama hicho mjini
Kayanga,alisema umefika wakati wa viongozi wa chama hicho kuwa na fikra chanya
katika ulimwengu wa ushindani wa biashara ya kahawa,na kusema kuwa vyama vya
ushirika vinakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa wanunuzi wengine.
Pia alisema Serikali itaendelea kuvilinda vyama vya ushirika
kisheria na kushauri Serikali za vijiji kutunga sheria ndogo ndogo
katika maeneo yao ili kulinda ubora wa kahawa,tofauti na ilivyo sasa ambapo
wakulima huvuna kahawa mbichi na nyingine kupelekwa kwenye vyama vya msingi
zikiwa na uchafu.
Katika hotuba yake pia pia aliishauri KDCU kuweka na
kutekeleza mikakati ya kuongeza wanachama na kutaka wakulima wanaouza kahawa
katika ushirika huo wapewe motisha mbalimbali ikiwemo kuwawezesha kueleka
watoto wao kupata elimu katika ngazi mbalimbali.
Naye Mwenyekiti wa KDCU Prospery Mulungi alisema chama hicho
kimechukua hatua mbalimbali ili kudhibiti watumishi wanaohusishwa na ubadhilifu
ikiwemo kuwafikisha katika vyombo vya sharia.Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo
baadhi ya watumishi wa KDCU wanadaiwa kukiingizia hasara chama hicho kwa
kuhusishwa na wizi wa fedha,maguni na kahawa.
Aidha Mwenyekiti huyo aliwaeleza wajumbe wa Mkutano huo kuwa
kwa msimu uliopita KDCU imekabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuyumba
kwa bei ya kahawa,na kushindwa kufikia lengo lake la kukusanya tani elfu kumi
na mbili za kahawa na badala yake kukusanya tani elfu tisa.
Ofisa kutoka Ofisi ya Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoani Kagera Mokili Juma akiwa makini kufuatilia majadiliano wakati wa Mkutano wa KDCU.