Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kuhuzunishwa sana na tukio la kushambuliwa na kuuawa kwa vijana saba hodari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania waliokuwa wanalinda amani katika eneo la Darfur, Sudan.
Kwa hakika, Rais amesikitishwa sana na kitendo hicho ambako wanajeshi wengine 14 wa Tanzania wamejeruhiwa na waasi wa Sudan na ametuma salamu za rambirambi za moyoni mwake kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na kwa familia za wafiwa wote.
Aidha, Rais Kikwete anaungana na Watanzania wote na hasa maofisa na wapiganaji wa JWTZ na familia za wafiwa kuomboleza vifo vya vijana hao hodari wa Tanzania. Rais pia anaungana na Watanzania wote kuwaombea wale walioumia katika tukio hilo waweze kupona haraka na kuendelea na majukumu yao ya
Katika salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Adolf Mwamunynge na familia za wafiwa, Rais Kikwete na Amiri Jeshi Mkuu amesema:
“Sina maneno ya kutosha ya kuelezea mshtuko, huzuni na masikitiko yangu makubwa kufuatia vifo vya vijana wetu hao ambao wamepoteza maisha yao katika shughuli muhimu sana ya utekelezaji wa majukumu ya Umoja wa Mataifa ya kulinda na kuleta amani katika eneo la dunia ambako maelfu kwa maelfu ya watu wamepoteza maisha yao kwa kushambuliwa na waassi.”
Rais Kikwete ameongeza kumwambia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na familia za wafiwa ”Napenda kwa niaba ya Watanzania wenzangu niwahakikishieni kwamba hakuna shaka kuwa vijana wetu hao tokea walipokwenda Darfur Februari mwaka huu, na kwa hakika tokea Tanzania ilipoanza kuchangia walinzi katika eneo hilo mwaka 2007, wamefanya kazi nzuri sana, kazi iliyoongozwa na weledi wa hali ya juu na kazi ambayo imeiletea nchi yetu heshima kubwa. Tutaendelea kuwaenzi kwa kujivunia kazi yao.”
Amesisitiza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza vijana wetu hawa. Kupitia kwao, natuma salamu za rambirambi kwa maofisa wakuu na maofisa wadogo pamoja na wapigaji wote wa Jeshi letu kwa kupotelewa na wenzao. “
“Aidha, kupitia kwako, natuma salamu zangu kwa wanafamilia za waliopotelewa na wapenzi wao na ndugu zao katika tukio hilo. Wajulishe kuwa naungana nao katika kuomboleza.
Kwa walioumia, Rais Kikwete amemwambia Jenerali Mwamunyange: “Naungana pia na Watanzania wenzangu katika kuwapa pole nyingi walioumia katika tukio hilo tukiwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na kuendelea na shughuli zao za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa.”
Vijana hao waliopoteza maisha yao na walioumia, walikuwa sehemu ya askari 37 na ofisa mmoja ambao walikuwa wanasindikiza msafara wa waangalizi wa kijeshi katika Darfur kutoka eneo la Khorabeche kwenda Nyara waliposhambuliwa na waasi kiasi cha kilomita 20 kutoka Khorabeche saa tatu asubuhi jana, Jumamosi, Julai 13, 2013.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
Mkurugenzi aigomea bodi ya CCM kujiuzulu
Mkurugenzi Mtendaji wa Kamapuni ya Peoples Media Communication iliyo chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mikidadi Mamhomud amekataa kujiuzuu wadhifa wake mbele ya wajumbe wa Bodi ya Uhuru FM katika kikao kichoongozwa na kigogo wa CCM imefahamika.
Habari za uhakika toka miongoni mwa wajumbe wa kikao hicho zilipatikana mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho zimeeleza kuwa wajumbe kwa pamoja hawakuridhishwa na utendaji wa Mkurugenzi huyo na kuifanya Uhuru FM inayomilikiwa na CCM kuzorota.
Kutokana na kusuasua kwa utendaji wa Radio hiyo na kumalizika kwa mkataba wa Mkurugenzi huyo toka mwaka 2010, wajumbe walipendekeza ajiuzulu ili kutoa nafasi kwa watu wengine kuomba nafasi hiyo.
Mambo kadhaa yameelezwa na wajumbe yakimuelemea Mikidadi ambaye ni mtangazaji wa siku nyingi wa Radio Tanzania Dar es Salaam, Radio One na ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilala Mkoani Dar es Salaam kwa kipindi kimoja na alishindwa kuchaguliwa tena katika nafasi hiyo ya uenyekiti wa CCM wilaya ya Ilala kutokana na ubadhilifu wa fedha na mali za chama alioufanya kipindi alichopata uenyekiti huo, na tabia hii ya ubadhilifu ameiendeleza hata alipopewa ukurugenzi wa Radio Uhuru.
Mjadala mkubwa ndani ya kikao hicho ulitokana na kufanyika kwa tathmini ya utendaji na ufanisi wa Radio hiyo, hali iliyothibitika kuwa imepoteza kundi la wasikilizaji na kukosekana kwa mvuto kwa wasikilizaji na pia kukosekana kwa ari ya wafanyakazi ambao hutayarisha vipindi na kupiga debe ili kukisaidia Chama Cha Mapinduzi kushinda kwenye chaguzi zake kuu.
Hata hivyo kwa upande mwingine malalamiko ya msingi toka kwa wafanyakazi wa kituo hicho ni juu ya makato ya fedha ya Hifadhi ya Jamii (NSSF) kudaiwa kutowasilishwa kunakohusikili hali fedha ya wafanyakazi inakatwa kila mwezi na pia baadahi ya wafanyakazi kudai kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha za taaasi na mali zake. Pia kuna tuhuma za tasisi hiyo kutolipa kodi (PAYEE) TRA ili hali wafanyakazi wanakatwa kodi hiyo kila mwezi.
Pia kuna madeni makubwa sana yanayoikumba tasisi hiyo ambayo nayo yametokana na ubadhilifu huo wa fedha za tasisi. Baadhi ya madeni yanayoikabili tasisi hiyo mbali na NSSF, TRA, ni deni kubwa la pango la minara ya kurushia matangazo huko Kisarawe, Mbeya, Dodoma , Tabora, Tanga na Arusha na Mwanza, kituo kinapata matangazo ya biashara, fedha za malipo hazionekani, hili limetukera kama wajumbe wa bodi tunataka hatua zichukuliwe ” alisema mmoja wa wajumbe wa Bodi hiyo.
Aidha, mjumbe mwingine alisema kikao hicho cha wajumbe wa bodi kimepata taarifa za kutosha toka kwa wadau mbali mbali kuwa Mkurugenzi huyo amekuwa akiajiri ovyo ovyo wafanyakazi wasio na sifa wala uwezo kwa njia za kujuana, undugu na upendeleo badala ya kubaki na timu ndogo itakayolipwa mishahara mizuri. Mfano, amemuajili mwanae wa kumzaa (ABDUL MIKIDADI) katika Redio hiyo bila hata ya kufuata taratibu za ajira zinazostahili, hana sifa wala elimu yoyote wakati wapo vijana wasomi wengi tu wapo mitaani wanahainga kutafuta kazi.ameajili vijana ambao ni watoto wa majirani zake huko anakoishi bila ya kuzingatia taratibu za ajira.hawana sifa yoyote. Hii yote ni ajira za kujuana tu!
Jambo jingine lililoelezwa na baadhi ya wajumbe wa bodi hiyo ya Radio ya CCM ni kutosikika kwa matangazo katika masafa yake kwenye Mikoa ya Arusha, Tanga na Tabora kwa muda mrefu huku uongozi chini ya Mikidadi ukikataa kuchukua hatua.
Kwa upande mwingine, taarifa zinaeleza kuwa tayari bodi hiyo ilishampeleka mshauri mwelekezi katika kituo hicho na kutaka yafanyike maboresho pamoja na kupunguzwa kwa baadhi ya wafanyakazi ambao hawana tija na sifa ya kiutendaji.
Taarifa za uhakika zimebainisha kuwa lawama kubwa anatupiwa mkurugenzi aliyepo kwa kushindwa kuhimili ushindani na vyombo binafsi licha ya Uhuru FM kuanzishwa mwaka 2000 lakini hadi sasa ikikosa hadhi na kushuka chati.
"Wafanyakazi wa Radio yetu si wakoofi ila ni jasiri, hawataki kuonewa na kuburuzwa, hutumia akili na maarifa katika kujituma lakini wanakatishwa tamaa hasa katika malipo ya posho, mishahara ya upendeleo kwa wengine kulipwa mishahara kiduchu bila ya kuangalia utendajikazi wa mtu au elimu yake.
Kitendo cha mkurugenzi huyo (Mikidadi) kukataa kujiuzuru nafasi hiyo na hasa kutokana na tuhuma zinazomkabili, tuhuma za Ubadhilifu wa fedha na mali za tasisi hiyo, tuhuma ya ngono kwa wasichana wanaotaka ajira katika redio hiyo, ajira za upendeleo na undugu, mishahara ya upendeleo nk, kitendo hicho kinatafusiliwa kuwa huenda labda urafiki wake na katibu mkuu wa CCM ndio unampa kiburi na jeuri hiyo ya kutojiuzuru.
Mwisho kama kweli ile sera ya kuvua gamba ipo active, basi hili ni gamba lingine linalopaswa kuvuliwa haraka kabla mambo makubwa na ya hatari hayatokea katika tasisi hii zaidi ya kesi iliyopo mahakamani kwa sasa ya ubadhilifu wa fedha za wafanyakazi za NSSF inayomkabili mkurugenzi huyu .
CREDIT;JF
Rais wa Sudan Omar al-Bashir, ameondoka nchini Nigeria baada ya makundi ya kutetea haki za kibinadam kwenda mahakamani, kushinikiza serikali kumkamata kuhusiana na tuhuma za uhalifu wa kivita.
Afisa mmoja wa kibalozi, katika ubalozi wa Sudan nchini Nigeria, amesema rais Bashir, alirejea nyumbani Jumatatu jioni kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Muungano wa Afrika ambao alikuwa akihudhuria.
Afisa huyo amesema, rais huyo alikuwa na majukumu mengine ambayo yalikuwa yakimsubiri nyumbani na amekanusha madai kuwa aliondoka kwa sababu ya kuongezeka kwa shinikizo za kukamatwa kwake.
Mahakama ya kimataifa ya Jinai ICC, inamtuhumu Rais Bashir kwa kuhusika na mauaji ya halaiki katika eneo la Darfur nchini Sudan.
Muungano wa Afrika umetoa wito kwa wanachama wake kutotekeleza agizo la mahakama ya ICC ya kumkamata rais huyo wa Sudan.
Viongozi hao wa AU wanasema mahakama hiyo ya ICC imekuwa ikiwalenga viongozi wa nchi za Kiafrika pekee.
Bwana Bashir alikuwa Nigeria kwa mkutano ulioandaliwa na muungano wa Afrika kuhusu afya unaokamailika baadaye leo.
Ubalozi wa Sudan umesema kuwa aliondoka kwa sababu ya majukumu mengine.
Mahakama ya kimataifa ya ICC ilitoa kibali cha kumkamata Bashir mwaka 2009, baada ya kumtuhumu kwa kufanya mauaji ya halaiki wakati wa vita vilivyodumu mwongo mmoja katika jimbo la Darfur.
Sudan haitambui mahakama ya ICC na inaituhumu kwa kuwa chombo cha nchi za kimataifa kutumiwa kukandamiza nchi za Afrika huku Muungano wa Ulaya ukitoa wito kwa nchi za Afrika kutomkamata Bashir.
Aidha Bashir alitarajiwa kutoa hotuba kwenye mkutano huo mjini Abuja, Jumatatu kulingana na vyombo vya habari nchini humo.
Lakini alipoitwa kutoa hotuba yake hakuwepo kwenye ukumbi.
Bashir alipokelewa na gwaride la jeshi Nigeria, alipowasili mjini Abuja Jumamosi. Mkutano huo unatafuta mbinu za kupambana zaidi na magonjwa ya Kifua kikuu, Ukimwi na Malaria.
Viongozi kutoka nchi nane za Afrika wanahudhuria mkutano huo.
Msemaji wa rais wa Nigeria,Reuben Abati, aliambia shirika la habari la AP kuwa Bashir alikuwa mjini Abuja kwa mwaliko wa muungano wa AU wala sio Nigeria.
CHANZO;BBC