Bukobawadau

Maofisa ugani watakiwa kuwa na mavazi ya shamba

Na Ashura Jumapili.
MKUU wa Wilaya ya Muleba, Lembris Kipuyo, amewaagiza maofisa ugani wa halmashauri hiyo kuwa na mavazi ya shambani yaliyowekewa nembo ili watambulike kwa wakulima.
Kipuyo alitoa agizo hilo katika kongamano la mtandao wa vikundi vya wakulima wadogowadogo (Mviwata) mkoani Kagera la kuibua changamoto za kilimo lililofanyika wilayani hapa.
Mkuu huyo wa wilaya (DC), alisema lengo la kutaka kuwepo na vazi maalum la kuwatambua maofisa ugani linatokana na maafisa ugani walio vijijini kufanana na wakulima, hivyo kuwapa wakati mgumu baadhi ya wakulima kuwatambua pindi wanapowahitaji.
Alisema wataalam hao wa kilimo ni wachache katika halmashauri hiyo yenye vijiji 161 ambao hawatoshelezi mahitaji ya wakulima kwa wakati kutokana na ukosefu wa miundombinu ya usafiri.
Alisema wilaya hiyo iko kwenye mkakati wa kuwawezesha maofisa ugani wachache ambapo mmoja ataweza kuhudumia vijiji vitatu na kuwafikia wakulima kwa ukaribu zaidi kwa kuwapatia pikipiki.
Alisema mpango huo utasaidia ukusanyaji wa takwimu za kilimo kupitia maafisa ugani kwa kuwezeshwa usafiri na vitendea kazi vya kutosha.
Mbali na hilo, aliwatahadharisha wakulima kuhusu kuhifadhi mazingira na kuwataka kuacha tabia ya kulima kwenye vyanzo vya maji.
Next Post Previous Post
Bukobawadau