SEARCH -TAFUTA

.

SIR.LOOM INC

KARIBU BUKOBAWADAU BLOG

SADATH BOUTIQUE

PROAKTIV COMMUNICATIONS

15 July 2019

MBUNGE WA JIMBO LA NKENGE AENDELEA NA ZIARA KIJIJI KWA KIJIJI ....

Mh.Balozi Dr.Diodorus Buberwa Kamala Mbunge wa Jimbo la Nkenge ameendelea na ziara yake ya Kijiji kwa kijiji ambapo leo jumapili July 14,2017 amekutana na wananchi wa Kijiji Kabingo Kata Bugorora ili kutoa mrejesho yaliyojiri katika Bunge la Bajeti sambamba na kusikiliza kero na kutatua changamto zinazowakabili na kutolea ufafanuzi suala la miundombinu ya barabara ya Kyabugombe -Karambi iliyopo chini ya Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura) ambapo kiasi cha ambapo kiasi cha Shilingi milioni 924 zimedhibitishwa na Bunge kwa ajili ya Tarura Wilayani Missenyi.
 Wananchi wakazi wa Kijiji cha  Kabingo wakifatilia hoja mbalimbali katika mkutano wa hadhara wa Mbunge Balozi Dk. Kamala
 Wananchi wa Kijiji cha  Kabingo kata Bugorora wakiendelea kumsikiliza kwa makini Mbunge wao Balozi Dk Kamala
 Mh.Mbunge Balozi Dr.Diodorus Buberwa Kamala akitolea ufafanuzi bajeti ya Serikali katika Sekta ya Afya ambapo kuna ongezeko la fedha mara tatu katika mgao wa hospitali za mikoa mbalimbali nchini ikiwemo hospitali kuu ya Mkoa Kagera kutoka Shilingi milioni 700 hadi bilioni 3.1 na kuwaeleza wananchi kwamba Serikali ya Rais Magufuli inazidi kusogeza huduma za Afya karibu na Wananchi
 Mh.Diwani wa Kata ya Bugorora  Projestus Ruzigija akitolea jambo ufafanuzi
 Sehemu ya Wananchi waliohudhuria mkutano huo
Muendelezo wa matukio ya picha

14 July 2019

IJUE MITAZAMO YA VIONGOZI WETU KUELEKEA WIKI YA UWEKEZAJI KAGERA AGOSTI 12 HADI 17, 2019 GYMKHANA MANISPAA YA BUKOBA

Tunapoelekea katika Wiki ya Uwekezaji Mkoani Kagera sasa tunakuletea makala fupi fupi ili ujue malengo ya wiki hiyo na mtazamo wa viongozi wa Mkoa wa Kagera kuelekea Wiki hiyo Agosti 12 hadi 17, 2019 wiki ambayo ni fursa kubwa kwa Wanakagera na wadau mbalimbali wa maendeleo kuzijua fursa zinazopatka Kagera na kuzichangamkia.
Kaulimbiu ya Wiki ya Uwekezaji Kagera ni “Kagera Eneo la Kimkakati kwa Uchumi Wetu na Afrika Mashariki” kaulimbiu hii inamaanisha kuwa Mkoa wa Kagera unapakana na nchi tano za Kenya, Uganda, Burundi, Sudani Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi hizo ni fursa ya biashara kutokea Kagera.
Katika kuelekea Wiki ya Uwekezaji Kagera Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti tayari amefanya mawasilianao na Balozi wa Nchi ya Kongo ambaye tayari amethibitisha kushiriki wiki hiyo jambo ambalo kwa wadau wa biashara wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo ya kufanya biashara na nchi ya Kongo (DRC) mfano biashara ya Samaki, Dagaa, mbogamboga, mahindi na ndizi.
Pili, Mhe. Gaguti tayari Julai 7, 2019 amekutana na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda Mhe. Ernest Mangu ili kuweka mazingira sawa kati ya wafanyabiashara wa Rwanda na Tanzania na Wanankagera kutumia fursa ya mpaka wa Rusumo kufanya biashara nchini Rwanda kwa kutumia fursa ya ukaribu na kuwa na mpaka mrefu katika wa Kagera.
Balozi wa Tanzania nchini Rwanda Mhe. Ernest Mangu katika kikao hicho cha Julai 7, 2019 kilichofanyika Wilayani Ngara alihaidi kuwaleta wafanyabiashara wa Rwanda kuja kushiriki katika Wiki ya Kagera kuona fursa za uwekezaji pamoja na biashara mbalimbali wanazoweza kufanya kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa Mkoa wa Kagera au Watanzania, hiyo ni fursa inakuja.
Naye katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Profesa Faustin Kamuzora akiwa Mwenyekiti wa kikao cha kupitia andiko la uwekezaji Mkoani Kagera kilichofanyika Julai 11, 2019 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa alisema kuwa ni bahati kubwa ambayo haijawahi kutokea tangu uhuru mkoa kuwa na andiko la uwekezaji ambalo litazinduliwa rasmi Agosti 14, 2019 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ambaye atakuwa mgeni Rasmi katika Wiki ya Uwekezaji Kagera.
Naye Sheikh Haruna kichwabuta Sheikh wa Mkoa wa Kagera akitoa neno katika uzinduzi wa mpango mkakati wa miaka mitano wa maendeleo wa Baraza la Waislamu Tanzania Mkoa wa Kagera Juni 22, 2019 katika Shule ya Nyanshenye Manispaa ya Bukoba alitoa wito kwa Waislamu wenzake kuiona Wiki ya Kagera kama fursa na wasibaki nyuma bali washiriki kikamilifu mkoa wa kagera usonge mbele kwa kuzitumia fursa uliobarikiwa nazo
Askofu Dk. Abednego Keshomshahara wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Magharibi akitoa neno katika mkutano wa SINODE wa mwaka Kiizi Halmashauri ya Bukoba aliwakumbusha wachungaji Maaskofu na viongozi wote waliokuwepo katika mkutano huo kuwa Mkuu wa Mkoa Kagera anataka Kagera ifunguke na anatakiwa kuungwa mkono kwa dhati katika Wiki ya Uwekezaji Kagera.
Katika Wiki ya Uwekezaji Kagera pamoja na fursa nyingi zitakazokuwepo lakini fursa ya utamaduni katika mkoa wa Kagera pia itaangaliwa kwa karibu hasa utamaduni wa watu wanaoishi katika mkoa huu ambapo tamaduni hizo zinaweza kuwa kivutio kikubwa na kuleta watalii na kuacha fedha za kigeni ili kukuza zaidi uchumi wa mkoa.
Jipange kushiriki Wiki ya Uwekezaji Kagera na kuzitumia fursa za Kagera kujenga uchumi wako binafsi, uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla “Kagera Eneo la Kimkakati kwa Uchumi Wetu na Afrika Mashariki” Kagera Kazi, Amani na Maendeleo.

BMC MABINGWA FAINALI ZA RWEGASIRA CUP

Mgeni Rasmi Profesa Faustin Kamuzora Katibu tawala mkoa Kagera  akikabidhi Kombe kwa  nahodha wa timu ya Bukoba Munispaa Council (BMC) ambao ndio Mabingwa wa michuano ya Rwegasira Cup 2019  inayodhaminiwa na Ndugu Edward Rwegasira pichani kushoto. 
Wananchi wakiwa wamehudhuriwa mpambano huo
Baada ya kutoka 2-2 katika dakika 120 sasa tunashuhudia matuta.
Timu ya BMC inapata ushindi kwa penati  4-3 

Mpaka mwisho wa Mchezo Busimbe Fc 3-4 Bukoba Municipal Council (BMC)
Kwa hisani kubwa ya Ndugu Edward Rwegasira

12 July 2019

KAMISHNA GENERALI WA MAGEREZA NCHINI AMPONGEZA RC GAGUTI KUDUMISHA ULINZI NA USALAMA WA KAGERA PIA AGUSWA NA USHIRIKIANO NA JESHI LA MAGEREZA

Kamishna Generali wa Magereza nchini Tanzania Phaustine Kasike afurahishwa na ushirikiano wa Serikali ya Mkoa wa Kagera chini ya Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti na Jeshi la Magereza mkoani humo namna wanavyoshirikiana kutatua changamoto mbalimbali za Jeshi hilo katika kuweka mazingira bora ya utendaji kazi.

Akiwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa Kamishna Generali Kasike Julai 10, 2019 alipofika kumsalimia Mkuu wa Mkoa Gaguti alimpongeza yeye binafsi pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kwa kudumisha ulinzi na usalama hasa kwa kipindi hiki ambacho sasa mkoa wa Kagera umetulia kwa matukio mbalimbali makubwa ya utekaji barabarani
Kamishna Generali Kasike alisema kuwa yupo Mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi hasa kufuatilia maelekezo mahususi yaliyotolewa na kwa Jeshi hilo ya kuhakikisha Jeshi la Magereza linazalisha chakula cha kutosha kuwalisha wafungwa lakini pia ikiwezekana kuzalisha ziada ya chakula kwani nguvu kazi ya kuzalisha chakula hicho ipo ambao ni wafungwa katika Magereza.
“Sisi Jeshi la Magereza Tumeweka mkakati maalumu wa kuzalisha chakula cha kutosha kulisha Magereza yote nchini na katika mkakati huo tulibainisha Magereza kumi nchi nzima ambapo na Gereza la Kitengure la hapa mkoani Kagera lipo kati ya hayo kumi kwani Gereza hilo linazalisha chakula kwa misimu miwili ya vuli na masika.” Alifafanua Jenerali Kasike.
 Pia Kamishna Jenerali Kasike alisema katika kuboresha makazi ya Maafisa wa Jeshi la Magereza wanao mpango mkakati wa Kila Gereza kuzalisha tofali hasa zile za kuchoma ili kujenga makazi mapya ya Maafisa na kukarabati miundombinu ambayo tayari imechoka.
Kwaniaba ya wananchi wa Mkoa wa Kagera Mkuu wa Mkoa Gaguti alimshukuru Kamishna Generali Kasike kwa kuamua kufanya ziara Mkoani Kagera kuja kuona changamoto mbalimbali hasa kwa upande wa chakula cha wafungwa na makazi ya Maafisa wa Jeshi hilo la Magereza.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alimhakikishia Jenerali Kasike kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha hasa katika ujenzi wa makazi bora ya Maafisa wa Magereza ili kuboresha zaidi utendaji kazi wa Maafisa hao katika kutekeleza majukumu yao.
Aidha, uongozi wa mkoa utaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Jeshi la Magereza Mkoani Kagera Kagera katika kuzalisha chakula cha kujitosheleza kwa Wafungwa lakini pia kuzalisha chakula cha ziada kwa Magereza ya nje ya Mkoa kwa kuwa Mkoa wa Kagera unayo fursa nzuri ya kilimo na kupelekea uzalishaji wa chakula kuwezekana kwa mimisimu miwili taofauti.
Mwisho Kamishna Jenerali Kasike alisema kuwa ziara yake ni ya mafanikio makubwa mkoani Kagera kwa jinsi alivyopokelewa na uongozi wa mkoa pia alivyohakikishiwa ushirikiano na Mkuu wa Mkoa Gaguti katika kutatua changamoto mbalimbali za Jeshi la Magereza.

Na: Sylvester Raphael 

RWEGASIRA FC WASHINDA 1-0 DHIDI YA KIBETA

 Wenyeji wa michuana ya Rwegasira Cup timu yaRwegasira Fc ya Kitendaguro wametoka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Kibeta mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa chuo cha Afya Cha Kagemu.
Taswira kutoka Viwanja vya Chuo cha Afya Kagemu kilichopo Kata Kitendaguro Manispaa Bukoba
Ndugu  Edward Emmanuel Rwegasira  pichani kushoto mdhamini na mwandaaji wa michuano hiyo akifuatilia Mechi ya kumtafuta mshindi wa tatu kati ya timu yake wenyeji Rwegasira Fc na Kebeta Fc
Wapenzi wa Soka wakifuatilia mchezo wa Mashindano ya Rwegasira Cup yaliyoandaliwa na Mmoja wa Watoto wa Marehemu mzee Emmanuel Rwegasira aliyewahi kuwa Mbunge wa Bukoba Vijijini na Mwenyekiti wa CCM Wilaya Bukoba ni katika Uwanja wa Chuo cha Afya Kagemu Manispaa Bukoba.
 Viongozi wa timu Rwegasira Fc walioibuka kidedea kwa kuichapa bao 1-0  timu ya Kibeta Fc.
Mtanange ukiendelea Uwanjani
 Benchi la Wachezaji wa Timu ya Rwegasira Fc.

 Wachezaji wa timu ya Rwegasira Cup wakishangilia bao lao la Ushindi
Mchezo wa  fainali hizi unatalajiwa kufanyika Jioni ya leo Ijumaa kwa kuzikutanisha timu ya Bukoba Municipal Council (BMC) na Buhembe Fc
 Mchezaji wa Kibeta Fc akitibiwa ili arudi uwanjani
Wadau wa kamati ya maandalizi ya Michuano ya Rwegasira Cup
 Muendelezo wa matukio ya picha Uwanjani Rwegasira Fc 1-0 Kibeta Fc.
Mpambano wa kutafuta mshindi wa tatu,Michuano ya Rwegasira CUP 
 Wakati Mgeni Rasmi ambaye ni mdhamini wa Michuano hii Ndugu  Edward Emmanuel Rwegasira akisalimiana na Wachezaji na Viongozi wa timu ya Rwegasira Fc.
 Katika picha ya Pamoja na Wachezaji wa Kibeta Fc.
Mchezo wa  fainali za  Rwegasira Cup unatalajiwa kufanyika  leo Ijumaa July 12,2019 saa 10:00 Jioni kwa kuzikutanisha timu ya Bukoba Municipal Council (BMC) na Buhembe Fc


09 July 2019

MKUU WA MKOA WA KAGERA KUWATIA HASIRA WAFANYABIASHARA WA MIPAKANI KUCHANGAMKIA FURSA ZA NCHI JIRANI

• Soko la Tanzania lipo Rwanda ardhi yao haiongezeki watu wanaongezeka – Balozi Mangu
Na: Sylvester Raphael
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti aweka mkakati kabambe wa kuwatia hasira wafanyabiashara wa mkoa wake kutambua na kuzitumia fursa za kufanya biashara na nchi jirani za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambazo bado hatumiki ipasavyo katika kuinua uchumi wa wa Mkoa na Tanzania kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alionesha nia na matamanio yake hayo baada ya kufanya kikao cha wadau wa Biashara Mkoani Kagera pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda Mhe. Ernest Mangu ili kujadili fursa zinazopatikana nchini Rwanda na Wafanyabiashara wa Tanzania hasa wa Mkoa wa Kagera wanaweza kuzitumiaje fursa hizo kufanya baiashara.
Katika kikao hicho cha wadau wa biashara kilichofanyika Wilayani Ngara Julai 7, 2019 Mkuu wa Mkoa Gaguti baada ya kusikiliza kwa umakini wasilisho la Balozi Mangu kuhusu fursa za biashara zinazopatikana nchini Rwanda pia na maoni ya wafanyabiashara wa mpakani hasa Rusumo na Kabanga alisema kuwa haoni mwamko au hasira za wafanyabiashara wa upande wa Tanzania hasa Kagera kunuia kufanya biashara ya kweli na jirani zetu Wanyarwanda.
“Nakaribia kumaliza mwaka katika nafasi yangu ya ukuu wa Mkoa lakini sijawahi kuona wafanyabiashara wameleta kero kwangu inayohusu namna wao wanavyofanya biashara au vikwazo vinavowakwaza bali napokea kero za migogoro tu ofisini kwangu sioni kabisa hasira ya wafanyabiashara wetu kutaka kutumia fursa za mkoa huu kupakana na nchi hizi sana sana nimesikiliza maoni yao hapa walio wengi si wafanyabiashara bali madalali tu.” Alisisitiza Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Balozi wa Tanzania nchini Rwanda Ernest Mangu akitaja fursa za biashara ambazo hazijawahi kutumika ipasavyo na Watanzania alisema kuwa alipoteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda jambo la kwanza kulifanya lilikuwa ni kutembelea mipaka yote ya Rwanda kuona biashara zinafanyikaje lakini katika mipaka yote mpaka wa Rusumo ndiyo umedorora sana na haufanyi biashara kama mipaka mingine ilivyo.
Balozi Mangu alisema katika nchi ya Rwanda kuna soko kubwa la Dagaa, Samaki, Ndizi, Mchele, mahindi, Mbogamboga, Saruji pamoja na bidhaa nyinginezo za viwandani. Ukiondoa saruji bidhaa zilizotajwa zinapatikana mkoa wa Kagera na mikoa ya jirani jambo ambalo lingewafanya wafanyabiashara wa Kagera na mikoa jirani kutumia fursa ya uhuhitaji huo kufanya biashara na Wanyarwanda pia na nchi ya Congo kwani kutoka Kagera kwenda Congo ni Kilometa 350 hadi 400 tu.
“Nchi ya Rwanda ina milima na mabonde na kwasasa ina wingi wa watu kuliko ardhi iliyopo kwahiyo wanahitaji chakula hasa ndizi na ndizi hizo zinalimwa hapa Kagera lakini bado sijaona wafanyabiashara wanaojishughulisha na biashara ya ndizi kwenda Rwanda. Pili, Mchele wa Tanzania unapendwa sana na Wanyarwanda lakini pia kuna soko Congo bado Watanzania hatujalichangamkia soko hilo bali Wanyarwanda wenyewe ndiyo wanafanyabiashara.” Alifafanua Balozi Mangu
Balozi Mangu alishauri Halmashauri za Wilaya za mipakani kwa kushirikiana na Wafanyabiashara kujenga maghara ya bidhaa mbalimbali ili bidhaa zinazotakiwa na nchi jirani zipatikane karibu na mipaka kuliko kuzifuata mbali ndani ya nchi mfano Saruji Mtwara, Mchele mpaka Kahama Shinyanga au Mwanza na bidhaa nyinginezo mpaka Kariakoo Dar es Salaam.
Aidha, Balozi Mangu alishauri kuanzishwa kwa magulio au masoko makubwa karibu na mipaka ambapo katika masoko au magulio hayo kila bidhaa ipatikane ili majirani waweza kuwa wanavuka na kununua bidhaa hizo bila kuzifuata mbali na mpaka. “Kwasasa tangu Rwanada ifunge mpaka wake na Uganda Serikali ilielekeza wazi wananchi wake kuwa bidhaa zote wanazozitaka wazipate Tanzania, hilo ni soko kwetu sasa. Alisisitiza Balozi Mangu.
Ili kuhakikisha fursa za biashara zilizopo nchini Rwanda zinachangamkiwa na Watanzania hasa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Kagera Kikao hicho cha wadau wa Biashara kiliweka mkakati wa muda mfupi wa maazimio makubwa sita kuhakikisha fursa hizo zinachangamkiwa kisawasawa kama ifuatavyo:
Kwanza ndani ya wiki mbili toka siku ya kikao Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoani Kagera (TRA) kwa kushirikiana na Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) pamoja na Maafisa Biashara wa Wilaya na Mkoa wafanye usajiri wa wafanyabiashara za mipakani wote na si madalari ili kujua ni biashara gani wanafanya ili kusaidiwa.
Pili, ndani ya mwezi mmoja TRA Kagera waandae kikao kikubwa cha wafanyabiashara wote ili kutoa elimu ya biashara ya mipakani ikiwa ni pamoja na Ubalozi wa Tanzania Nchini Rwanda kualikwa kushiriki kutoa elimu juu ya fursa za Kibiashara zinazopatika nchini Rwanda.
Tatu, ndani ya Mwezi mmoja kiandaliwe kikao cha ujirani mwema kati ya Mkoa wa Kagera na Mkoa wa Jirani wa Rwanda ili kuzungumza na kuweka mikakati ya pamoja ya namna bora wafanyabiashara wa mikoa hiyo wanavyoweza kushirikaiana katika biashara.
Nne, Maafisa Biashara wakishirikiana na Wakuu wa Wilaya wafanye utambuzi wa maeneo ya kufanyia biashara mfano kama mfanyabiashara anataka dagaa azipate wapi na sikwenda moja kwa moaj kwa mvuvi au kama ni ndizi asiende moja kwa moja kwa mkulima bali pawepo na soko au eneo anapoweza kupata bidhaa hizo.
Mwisho Halmashauri za Wilaya pamoja na Mkoa kuwa na mpango Mkakati wa kuboresha masoko ya mipakani ambayo tayari yalikuwa yameanza kujengwa mfano soko la Nkwenda na Murongo Wilayani Kyerwa pamoja na soko la Kabanga Wilayani Ngara.
Mara baada ya kikao hicho wafanyabiashara waliohudhuria walimshukuru Mkuu wa Mkoa Gaguti kwa kuwakutanisha na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda Ernest Mangu na kuwafungua macho ya kufanya biashara pia na kuwajengea uwezo wa namna gani wanawezaje kulifikia soko la Rwanda wakiwa wafanyabiashara wa Tanzania.

 

WASILIANA NASI KUPITIA 0715505043 / 0784505045 0768397241 / 0754505043

.

SIR.LOOM INC & MC BARAKA

.

IDADI YA WATU