Bukobawadau

Bunge utata mtupu watatu watimuliwa tena,mwongozo wa spika waleta shida

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP) Said Mwema, jana alikuwa miongoni mwa watu walioshuhudia patashika iliyosababisha Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwatimua kikaoni wabunge watatu wa Chadema. Wabunge hao waliofukuzwa bungeni jana asubuhi ni Godbless Lema (Arusha Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Tundu Lissu (Singida Mashariki).

Walifukuzwa kutokana na kile Naibu Spika Ndugai alichoeleza kuwa ni kukiuka Kanuni za Bunge zinazowataka kutozungumza chochote ndani ya bunge bila idhini ya kiti cha spika.

Tukio la kufukuzwa kwa wabunge hao limekuja siku moja baada ya mmoja wa wenyeviti wa Bunge, Sylivester Mabumba, kumfukuza bungeni Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (Chadema), baada ya kukaidi amri iliyomtaka akae chini wakati akiomba mwongozo.

Wakati tukio hilo la juzi likiwa limeonyesha taswira mbaya kwa mhimili huo wa dola wa kutunga sheria na kuisimamia Serikali, jana Lissu, Lema na Msigwa kwa pamoja walipewa adhabu hiyo baada ya kubishana na Ndugai bila utaratibu.

Katika tukio hilo, wabunge hao walipinga kile walichokiita muda mrefu aliokuwa amepewa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kueleza kukiukwa kwa kanuni za Bunge.

Lukuvi aliomba kupewa mwongozo wa Naibu Spika mara baada ya Lema ambaye ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kusoma hotuba ya maoni ya kambi ya upinzani kuhusu wizara hiyo ambayo ilikuwa na shutuma nyingi dhidi ya Serikali, hasa Jeshi la Polisi


"Mwongozo wa Spika, mwongozo wa Spika........Mheshimiwa Naibu Spika sasa......," alisikika sauti ya Lissu wakati Lukuvi akiendelea kuzungumza, hali iliyosababisha Naibu Spika kusimama na kumuonya.

"Nimesema hairuhusiwi kuwasha mic (kinasa sauti) yako bila ruhusa yangu...waziri endelea...." alisema Ndugai
Baada ya kauli hiyo, ndipo vipaza sauti ambavyo haikuwa rahisi kufahamu idadi yake viliwashwa na sauti kuanza kusikika zikimkosoa Ndugai kwamba anapendelea, kwani Lukuvi alipewa muda mrefu wa kuomba utaratibu tofauti na msimamo wa awali aliokuwa ameutoa Naibu Spika huyo


"Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani ..." ilisikika sauti ya Msigwa huku sauti nyingine kadha wa kadha zikisikika bila mpangilio hali iliyosababisha taharuki na kuathiri shughuli za Bunge. Sauti hizo zilisababisha mzozo na kukosekana kwa utulivu na usikivu bungeni hivyo Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM) akaamua kutumia rungu lake kuwafukuza wabunge hao watatu kutoka ndani ya Ukumbi wa Bunge.

"Nilishasema tangu asubuhi na nimewakumbusha kwamba hakuna mbunge anayeruhusiwa kuwasha microphone (kinasa sauti) na kuzungumza bila idhini ya kiti, sasa naanza kutumia kanuni, nimewaona wabunge watatu, Mheshimiwa Lissu, Mheshimiwa Mchungaji Msigwa na Mheshimiwa Lema, tokeni nje," aliamuru Ndugai na kuongeza:
"Tena nitafuatilia kuhakikisha kwamba mnaondolewa kabisa nje ya geti (lango kuu) la kuingilia bungeni, muondoke kabisa katika eneo hili."

Kufuatia kauli hiyo, wabunge hao walitoka nje huku wakisindikizwa na askari (wapambe) wa Bunge hadi nje ya ukumbi na baadaye kuondolewa kabisa katika eneo hilo, hivyo kutokuwa na fursa hata ya kuzungumza na waandishi wa habari


Tafrani hiyo ilishuhudiwa na IGP Mwema pamoja na wakuu wa taasisi nyingine zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo jana iliwasilisha hotuba yake kwa mwaka 2011/2012.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, wabunge hao jana hawakuruhusiwa kurejea tena bungeni siku hiyo, badala yake watarejea leo kwani adhabu yao ni kukosa kikao kwa siku moja tu.

Hotuba ya Lema
Katika hotuba ya kambi yake,Lema aliikosoa Serikali kwamba imekuwa ikiwatumia polisi kuwakandamiza wananchi, huku akihoji sababu za kutochunguzwa kwa mauaji yaliyofanywa na polisi katika maeneo mbalimbali nchini.
Lema alifafanua kwamba, hali ya usalama wa raia na mali zao nchini ni mbaya tofauti na dira ya wizara ambayo inaweka wazi kuwa jukumu lake la msingi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, kuhifadhi wanaotuhumiwa kwa uhalifu na kuwarekebisha wafungwa.

"Vile mfumo mzima wa Magereza umekuwa wa kutesa na kudhalilisha zaidi wafungwa na watuhumiwa wa uhalifu kuliko kuwahifadhi na kuwarekebisha," alisema Lema na kuongeza:
"Mfumo wa uhamiaji umekuwa dhaifu kuruhusu wageni haramu badala ya kuwadhibiti na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, kimekuwa cha kushuhudia matukio ya moto badala ya kuyazuia na kuyadhibiti."

Waziri kivuli huyo alienda mbali kwa kutoa tuhuma nzito akisema, Serikali imekuwa ikitumia Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kuua raia wasiokuwa na hatia wanapodai haki zao, hali ambayo inakinzana na kauli za viongozi ambao wamekuwa wakihubiri amani.

Mbunge huyo alinukuu Ripoti ya Utafiti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambayo inaeleza kuhusu vifo vya watu 52 wakiwa mikononi mwa polisi mwaka 2010 katika eneo la Mgodi wa Dhahabu wa North Mara na kwamba, 10 kati yao waliuwawa na polisi.

"Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika kipindi cha miezi mitano ya mwanzo ya mwaka 2011, tayari Watanzania 21 wameuawa kwa kupigwa risasi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu na wengine wengi kuumizwa. Kati ya hao, watu 9 wameripotiwa kuuawa na Jeshi la Polisi katika maeneo yanayozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara peke yake," alisema Lema na kuongeza:
"Vile vile watu watatu waliuawa katika Jiji la Arusha polisi walipovamia maandamano ya amani kupinga uchaguzi batili wa meya wa jiji hilo".

Alisema vitendo hivyo vinakiuka Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 ambayo inatoa haki ya kuishi kwa kila mtu na kwamba vifungu vya 195 na 196 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania vinakataza vitendo vya mauaji vilivyo kinyume na sheria

"Kwa mujibu wa ibara ya 30(2)(c) ya Katiba, mauaji yanaweza kuwa halali endapo yamefanywa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa kwa ajili ya kuhakikisha utekelezaji wa hukumu au amri ya mahakama iliyotolewa katika shauri lolote la jinai.”

Alisema mauaji ambayo yamekuwa yakifanywa na Polisi yalipaswa kuchunguzwa kwani hayatokani na adhabu yoyote ya kifo iliyotolewa na mahakama za Tanzania.

Lema aliliambia Bunge kuwa; "Kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo, Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania, kifo chochote ambacho kimetokea katika mazingira ya mashaka kinatakiwa kuchunguzwa kwa mujibu wa sheria hiyo. Hatua ya kwanza ya uchunguzi wa kifo cha aina hiyo, kwa mujibu wa sheria hiyo, ni uchunguzi wa kidaktari ili kubainisha sababu halisi ya kifo hicho".

Ajali za barabarani
Kuhusu ajali za barabarani, Lema alisema Watanzania wengi wamekuwa wakipoteza maisha na kupata ulemavu wa kudumu kwa sababu ya kukithiri kwa ajali za barabarani.

"Taarifa tulizonazo zinaonyesha kuwa ajali za barabarani ziliongezeka kutoka 22,019 mwaka 2009 hadi 24,926 mwaka 2010....Katika ajali hizo watu 3,689 walifariki na wengine 22,064 walijeruhiwa.

Kiasi hiki ni kikubwa sana kwani ni sawa na ajali 68 kwa kila siku," alisema Lema na kuongeza:
"Hii ni sawa na kusema Watanzania 10 hufariki kila siku kutokana na ajali za barabarani ambazo nyingi zinasababishwa na uzembe na rushwa..."

Hoja ya Lukuvi
Hotuba hiyo ya Lema ilimfanya Lukuvi aombe utaratibu kwa Ndugai na aliporuhusiwa alikosoa hotuba hiyo ya waziri kivuli kwamba, ilikuwa imejaa uchochezi ambao haukupaswa kupewa nafasi ya kusikilizwa na Watanzania.
"Kama masikio ya Watanzania nayo yanaweza kuwa na uvumilivu kiasi hiki sijui, lakini tumeyaacha yote yasikike ili hawa wao wapime kwamba haya yanayosemwa ni ya kweli au vipi,"alisema Lukuvi na kuongeza:
"Hotuba karibu kila paragraph (aya) ina maneno ya ajabu, Mheshimiwa Lema anasema, Tanzania siyo nchi ya haki, watawala wanatesa wananchi, na sasa tunadiriki kuhamasisha polisi wasitii amri za makamanda wao."

Kwa mujibu wa waziri huyo, hotuba hiyo ya Lema kwa niaba ya Kambi ya Upinzani inalenga kupotosha msingi wa amani ya nchi, ambayo ndiyo imejenga demokrasia iliyowezesha wabunge wote kuchaguliwa na kuingia bungeni.
Lukuvi ambaye alitumia Kanuni ya 68 kutoa taarifa kuhusu utaratibu, pia alikuwa akitaka mwongozo kwa mujibu wa Kanuni ya 64 (1) (a-g) akisema kwamba Lema ametoa taarifa zisizo za kweli bungeni na tuhuma kama hizo zinapaswa kuwa na uthibitisho.

Wakati Lukuvi akiendelea na maelezo hayo, ndipo zogo lilipoanza kwa wabunge Msigwa, Lissu na Lema kupinga ombi lake kuchukua muda mrefu tofauti na taratibu za Bunge hilo, hali iliyosababisha Naibu Spika kuwatimua bungeni.

Naibu Spika je?
Akizungumza na Mwananchi baada ya kikao kuahirishwa jana mchana, Ndugai alisema hafungwi na kanuni kuhusu muda aliopaswa kumpa Lukuvi na akiwa kiongozi wa Serikali alipaswa kupewa muda huo ili kutoa maelezo ya upande wa pili.

"Wao (wapinzani) wanamtazama Lukuvi kama Lukuvi, hawajui kwamba yule ni kiongozi wa Serikali anapaswa kupewa muda kwa nafasi yake hiyo. Kwanza waziri alivumilia wakati wote huo, lakini wao wameshindwa kuvumilia, hii haipendezi,"alisema Ndugai.

Mapema wakati akiahirisha kikao jana mchana, Naibu Spika alitumia dakika kadhaa kutetea uamuzi wake na kwamba amewatoa nje wabunge hao kwa kukiuka kanuni ambazo tayari alikuwa amewakumbusha jana asubuhi.
Next Post Previous Post
Bukobawadau