Bukobawadau

RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE AWASILI MALAWI KUHUDHURIA MAZISHI YA BINGU WA MUTHARIKA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Blantyre, Malawi leo jioni kuhudhuria Mazishi ya Profesa Bingu wa Mutharika, aliyekuwa Rais wa Malawi, aliyefariki tarehe 5 Aprili, 2012 Kufuatia matatizo ya Moyo.
Rais Kikwete ni miongoni mwa Viongozi wakuu Saba kutoka nchi jirani na Malawi.
Nchi hizo ni Afrika Kusini, Benin, Kenya, Msumbiji, Zimbabwe na Zambia.
Wakati huohuo Ikulu inapenda kukanusha taarifa zilizonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari kudai kuwa Rais ametofautiana na Waziri Mkuu kuhusu aina ya hatua za kuwachukulia Mawaziri wanaotuhumiwa na ubadhirifu katika Wizara zao.
Napenda kueleza Umma kuwa taarifa hizo si za kweli.



Pia nitumie nafasi hii kuwatahadharisha waandishi wa habari kuwa makini, waangalifu na wachambuzi wakati wa kupokea, kusikiliza na kuandika au kutangaza taarifa wanazopata.
Rais kikwete aliwasili kutoka Brazil alipokuwa amekwenda kwa ziara ya kikazi ya siku tano tarehe 21 Aprili, 2012.
Kwa hivyo basi Rais hajapata taarifa yeyote rasmi kutoka kwa Waziri Mkuu, na bado anasubiri kupewa taarifa hiyo rasmi kwa vile suala la tuhuma hizo limetokea Bungeni.
Na kama kuna Waziri ambaye ameandika barua ya kujiuzulu, basi atakuwa amemuandikia Rais na kama zipo Rais ndiye atakayezipokea na kuamua hatua inayofuatia.
Kwa hivyo sio busara hata kidogo kwa vyombo vya habari kueneza uongo na fitna zenye lengo la kuchonganisha si viongozi tu , bali hata viongozi na wananchi kwa ujumla.
Rais Kikwete anatarajia kurejea nchini leo tarehe 23 Aprili mara baada ya maziko



Next Post Previous Post
Bukobawadau