Bukobawadau

ILIVYO SAFU MPYA YA WAKUU WA WILAYA MKOANI KAGERA

Safu ya zamani ya waliokuwa wakuu wa wilaya katika mkoa wa kagera, wa kwanza kutoka kushoto ni samwel kamote (bukoba) pili Hadija nyembo chato, Ernest Kahindi Biharamulo, Col Salum Nyakonji Ngara,Mama Mabula Muleba na Issa Njiku Missenyi

Mkoa wa Kagera umepata safu mpya ya Wakuu wa Wilaya katika mabadiliko yaliyofanywa na  Rais Jakaya Kikwete jana tarehe juma lililopita kwa kuwateua wapya 70, kuwabakiza kazini 63, kuwastaafisha 51, na kuwabadilisha vituo vya kazi baadhi yao.

Kati ya 70 wapya walioteuliwa mkoa wa Kagera umepata 3, ambao ni Richard Mbeho (Biharamulo), Constantine J. Kanyasu (Ngara) na Rodrick Mpogolo (Chato) ambayo sasa imehamia mkoa mpya wa Geita.

Kati ya 63 ambao waliobakizwa kazini na kuhamishwa vituo vya kazi  mkoa wa Kagera wamepangwa Zipporah L. Pangani (Bukoba), Lembris M. Kipuyo (Muleba), Darry Rwegasira (Karagwe), Lt. Col. Benedict Kitenga (Kyerwa Wilaya Mpya) na  Kanali Issa E. Njiku (Missenyi) ambaye amebakizwa katika kituo chake cha zamani. Aidha katika mkoa wa Kagera wamestaafishwa kazi waliokuwa Wakuu wa Wilaya wawili Samwel Kamote (Bukoba) na Col. Salum Nyakonji (Ngara).

Waliohamishwa vituo vya kazi kutoka mkoa wa Kagera ni Ernest N. Kahindi (Ngara) anahamia (Nyasa Wilaya Mpyao), Hadija H. Nyembo (Chato) anahamia (Uvinza Wilaya Mpya) na Angelina Mabula (Muleba) anahamia (Butihama Wilaya Mpya).

Akitangaza uteuzi huo mbele ya Wahariri wa vyombo vya habari, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema, “Zamani tulikuwa na wilaya 114 na baada ya Mhe. Raisi Kikwete kuridhia kuanzishwa kwa wilaya mpya 19, hivi sasa zimefikia wilaya 133. Kwa hiyo, tumebakizwa Wakuu wa Wilaya 63 na ukiongeza hawa wapya 70 unapata jumla yao ni 133,” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alisema miongoni mwa wakuu hao wapya wa wilaya, wengi wao ni vijana wenye umri kati ya miaka 30 hadi 45 na kwamba idadi yao inafikia 40. Alisema vilevile, idadi ya wakuu wa wilaya wanawake ni 43 sawa na asilimia 32.3.

Alisema wakuu wa wilaya watano kati ya 70 wapya walioteuliwa, wametokana na wabunge wa viti maalum. “Lengo letu ni kutaka kuandaa viongozi wapya wa baadaye kutokana na kundi hili,” alisema.

Alisema Wakuu hao wapya wanatakiwa kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi ili waapishwe na Wakuu wa Mikoa husika na kisha watatakiwa kuhudhuria mafunzo maalum ambayo yatafanyika Dodoma. “Tumeandaa mafunzo hayo maalumu kwa ajili ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Mikoa… siyo semina bali ni mafunzo na itabidi wapewe mitihani,” alifafanua.
Next Post Previous Post
Bukobawadau