Bukobawadau

JAMBAZI AUWAWA NA BUNDUKI TATU ZA KIVITA YAKIWEMO MABOMU VYAKAMATWA

Na Antidius Kalunde
Bukoba


JESHI la polisi Mkoani Kagera limefanikiwa kumuua jambazi katika majibizano ya risasi na kufanikiwa kukamata bunduki tatu risasi 246,mabomu ya kurushwa kwa mkono matatu na sare pea mbili ambazo zinafanana  kabisa na za jeshi la wananchi wa Tanzania.


Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa polisi Mkoani hapa Philp Kalangi amesema tukio hilo lilitokea tarehe
9 Juni majira ya saa 10 alfajiri katika eneo la Mavota-Tulawaka Wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera Mtu anayesadikiwa kuwa ni jambazi ambaye hafahamiki jina wala makazi yake aliuawa baada ya kupigwa risasi na askari polisi katika shambulizi.


Kamanda Kalangi, alisema tukio hilo lilitokea baada ya msiri kufichua mpango uliokuwa umepangwa na majambazi ambayo yalikuwa na lengo la kwenda kuvamia Mgodi wa Barrick Tulawaka ulioko Biharamulo Mkoani Kagera,jeshi la polisi baada ya kupata taarifa hizo mkuu wa upelelezi mkoa wa Kagera SSP,Peter Matage aliandaa mtego kupitia njia ambayo jambazi hilo lingetumia.


Alisema kutokana na taarifa za msiri jambazi huyo ndiye alikuwa kiongozi na alibeba silaha zote mwenyewe na tayari alikuwa amewatanguliza wenzake mbele ambao wangekutana eneo la tukio.


Kamanda alisema katika shambulizi hilo la kushitukiza na kurushiano risasi kati ya jambazi huyo na askari na hatimaye kuuawa kwa jambazi hilo na kukutwa na bunduki tatu ambazo mbili ni AK 47 ,SMG moja,riasi 246,mabomu ya kurushwa kwa mkono matatu,sare za jeshi la wananchi pea mbili na buti pea moja na makoti mawili ya mvua ambayo yalikuwa yamefungiwa bunduki mbili,na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali teule ya Biharamulo.

Kamanda Kalangi alisema katika tukio jingine jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa wanne waliokuwa wamepanga njama za kutaka kumuua ( ALBINO )aishie Wilayani Missenyi Mkoani Kagera.


Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Gaston Galela( 50 ),ambaye ni Mnyarwanda,alikamatwa akiwa Bwanga mkoani Geita kwa mganga wa kienyeji, Njenwa Charles ( 30 )msukuma na mkazi wa Mutukula Byamungu Felician ( 53 )mkazi wa Mutukula na Masanja Mabula ( 40 )mkazi wa Mutukula.


Alisema wamefanikiwa kuwatia mikononi  watuhumiwa hao kufuatia taarifa iliyotolewa kwa jeshi hilo kupitia kwa mpelelezi wa makosa ya jinai mkoani hapa Peter Matage aliyeandaa mtego wa kuwanasa na kufanikiwa.


Wakati huohuo jeshi hilo Mkoani Kagera limefanikiwa kumkamata Chamilion Kamugisha miaka ( 20 )mkazi wa Hamugembe Manispaa ya Bukoba  Juni 5 majira ya saa 10.00 asubuhi eneo la Mutukula Wilaya Ya Missenyi akiwa na noti bandia US Dollar 1000,wakati akiwa katika harakati za kubadilisha katika fedha za kitanzania.


Kamanda  wa polisi Mkoani hapa ambaye ndiyo mara yake ya kwanza kufanya kazi mkaoni Kagera amewataka wananchi wa Kagera kuwa na ushirikiano na jeshi la polisi sambamba na kuachana na mila potofu huku akisema mali azipatikani kwa imani za ushirikina ni juhudi na maarifa.
Next Post Previous Post
Bukobawadau