Bukobawadau

CHADEMA MKOANI KAGERA WAISAMBARATISHA NGOME YA MAGUFULI.

 Mwenyekiti wa CHADEMA wa Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Wilfred Lwakatare akimkabidhi kadi ya uanachama wa CHADEMA Makonzela Phinias.
Mwenyekiti wa CHADEMA wa Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Wilfred Lwakatare akimkabidhi kadi ya uanachama wa CHADEMA Dk. Lukanima.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Kagera kimeisambaratisha ngome ya Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, baada ya kufanikiwa kuwahamisha viongozi na wanachama 80 wa CCM akiwamo kada maarufu, Dk. Benedictor Lukanima.
 
Viongozi na wanachama hao wa CCM wakiongozwa na Dk. Lukanima, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Norte kilichopo nchini Colombia, walitangaza rasmi kuvua gamba na kuvaa gwanda katika mkutano wa hadhara wa CHADEMA uliofanyika juzi kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Chato mjini, na kuongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kagera, Alfred Mganyizi Rwagatare(Rwaks).
 
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa jimbo na wilaya hiyo ya Chato, Wana CCM hao waliohamia CHADEMA walikiponda vikali chama tawala, kwa madai kwamba serikali yake imeshindwa kuwasaidia wananchi kuondokana na kero nyingi, ukiwemo umaskini wa kupindukia unaozidi kuota mizizi hapa nchini.

Baadhi ya viongozi wa CCM waliohamia CHADEMA ni pamoja na Makonzela Phinias ambaye alikuwa mjumbe wa UVCCM na mwakilishi wa mkutano mkuu wa Vijana Mkoa wa Geita, Masunga Maswanzali, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Nyasenga, Kijiji na Kata ya Ilemela, Josephat Manyenye ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM pamoja na Dk. Benedictor Lukanima, ambaye mwaka 2010 alishika nafasi ya pili katika kura za maoni ndani ya chama hicho tawala.
 
 Marejesho ya kadi.
 Ulinzi imara sehemu ya tukio.
Habari matukio juu ya vua gamba vaa gwanda ndani ya Chato.

 Akihutubia mkutano huo, Mwenyekiti wa CHADEMA wa Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Wilfred Lwakatare alimrushia kombora zito Waziri Magufuli kwa madai kwamba, kiongozi huyo ameshindwa kuondoa kero nyingi zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo, ikiwamo ya uhaba wa huduma ya maji, afya, elimu na fursa za kiuchumi jimboni humo.

Lwakatare alimuita Dk. Magufuli bingwa wa takwimu aliyeshindwa kuwaletea maendeleo wananchi wake, licha ya kuwa waziri kwa muda mrefu serikalini. "Magufuli ni bingwa mkubwa wa takwimu. Anaweza kuwaambieni hadi samaki walio na mimba Ziwa Victoria. Lakini ameshindwa kutoa takwimu za wanafunzi wanaokwenda shuleni bila viatu wala ‘yebo yebo’.

"Wakati umefika sasa wananchi wa Chato kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu 2015, pigeni kura za hasira baina ya CCM na huyu Magufuli, kisha kuwachagua viongozi wa CHADEMA kwa maendeleo yenu," alisema Lwakatare.
 
 Kwa upande wake, Dk. Lukanima aliituhumu CCM na serikali kwa kukosa mwelekeo wa kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi wake kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
"CCM imekosa mwelekeo. Mimi na usomi wangu huu siwezi kuendelea kuwa ndani ya CCM ambayo naiona haina faida kabisa kwa Watanzania wenzangu. Hivi niwaulize ni yupi mwenye unafuu aliyeshika chuma cha moto na aliyeshika ubao?

"Jibu ni aliyeshika ubao...kwa hiyo njooni tujiunge na CHADEMA kwa ajili ya ukombozi wa nchi hii. Mfano, hapa Chato hakuna fursa za kiuchumi, mashirika yamekufa, huduma za kijamii mbovu, na anayeng’ang’ania CCM ni sawa na usaliti mkubwa wa maendeleo ya taifa hili," alisema Dk. Lukanima.

Aliwaomba wananchi wa Chato, mkoa na taifa kwa ujumla kukiunga mkono Chama hicho cha CHADEMA, ili kujikomboa na adha mbalimbali zinazolikabili taifa na wananchi wake, na kwamba kilichomsukuma kuhamia chama hicho cha upinzani ni kwenda kuongeza nguvu katika vuguvugu la mabadiliko.
 
HABARI KWA HISANI YA G SENGO.
Next Post Previous Post
Bukobawadau