Bukobawadau

MIONGOZO YA KUWAHUDUMIA WAATHIRIKA WA UKATILI IMETOLEWA KATIKA MKUTANO WA VIONGOZI MKOANI KAGERA.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoa Mheshimiwa Zipporah Pangani akifungua Mkutano kwa Niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe.
 Wajumbe wa Mkutano Wakifuatilia mada Katika Mkutano wa Uhamasishaji Viongozi Kuhusu Miongozo ya Kuwahudumia Waathirika wa Ukatili wa Kijinsia na Watoto.
 Mkuu wa Wilaya ya Bukoa Mheshimiwa Zipporah Pangani na Kaimu Katibu Tawala Mkoa Bw. Fikira Kissimba Wakisikiliza Jambo Kwenye Mkutano wa Uhamasishaji Viongozi Mkoani Kagera Katika kuwasilisha Miongozo ya Kuwahudumia Waathirika wa Ukatili wa Kijinsia na Watoto
 Picha ya Pamoja ya Wajumbe wa Mkutano wa Uhamasishaji Viongozi Kuhusu Miongozo ya Kuwahudumia Waathirika wa Ukatili wa Kijinsia na Watoto Mkoani Kagera.
 
Mkutano wa kuhamasisha viongozi kuhusu mwongozo wa Kisera na Mwongozo wa kutoa huduma kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto umefanyika mkoani Kagera siku ya Jumatatu tarehe 2/07/2012 katika ukumbi wa Bukoba Hotel mjini Bukoba na kuhusisha wadau wa afya mkoa mzima wa Kagera.
Mkutano huo ulifanyika chini ya wataalam kutoka katika Wizar ya Afya na Ustawi wa Jamii, pia mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Zipporah Pangani. Mkutano huo wa kutoa miongozo ya kuhudumia waathirika wa Ukatili umefanyika baada tafiti zilizofanyika Tanzania na kubainisha kuwa kuna ukatili mkubwa unaotendeka katika jamii.
Katika hotuba yake Mkuu wa Mkoa iliyosomwa na Mhe. Zipporah aliishukuru Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kuandaa mkutano huo wa uhamasishaji ambapo alisema mkutano umekuja kwa wakati muafaka kwasababu Tanzania ni nchi mojawapo ambayo iliridhia mikataba mbalimbali inayohusu kuzuia ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia na watoto pia na haki za watoto.
Katika hotuba yake Mhe. Massawe alibainisha kiwango cha ukatili katika mkoa  wa Kagera  ambacho ni kutokana na utafiti uliofanyika  mwaka 2010 na kuonyesha kuwa wanawake na wasichana waliofanyiwa ukatatili kimwili toka wakiwa na umri wa miaka 15 ni asilimia 49.4, umri kati ya miaka     15-49 waliofanyiwa ukatili wa kisaikolojia ni asilimia 54.2, ukatili wa kingono ni asilimia 29.2.
Pia wanawake waliofanyiwa ukatili wakiwa wajawazito ni asilimia 17.4 na asilimia 80 walikubali kwamba kupigwa mwanamke kwasababu fulani inakubalika. Vilevile utafiti wa mwaka 2009 uliozinduliwa Agosti 2011 ulibaini kuwa watoto wengi wako katika mazingira hatarishi ya kufanyiwa ukatili wakiwa nyumbani au shuleni maeneo wanayoyatumia kwa muda mwingi kuishi kabla ya kufikia ujana.
Kutokana utafiti huo watoto wamekuwa wakiathirika na ukatili wa kimwili kutoka kwa ndugu na jamaa zao wa karibu au viongozi na walimu wanaowalea kabla ya kufikia umri wa miaka 18. Asilimia 30 ya wanawake wenye umri  kati  ya 13-24 na asilimia 14 ya wanaume wenye umri  kati ya 13-24 walilipotiwa kuathirika na ukatili wa kingono angalau mara moja kabla ya kufikia umri wa miaka 18.
Mwisho Mhe. Massawe alisistiza wataalam, wadau, na Halmashauri za Wilaya kuzingatia miongozo iliyotolewa na Wizara katika kutoa huduma kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto. Aidha pia kukusanya takwimu na kuzichambua kwa kina ili kuweka mikakati endelevu ya kuwahudumia waathirika wa ukatili katika mkoa wa Kagera.
Changamoto kubwa iliyojitokeza katika mkutano huo ni wilaya pamoja na mkoa kwa ujumla kutokuwa na sehemu maalum za kuwahifadhi waathirika wa ukatili mara pale wanaporipoti ukatili dhidi yao na kupewa huduma ya matibabu na hatua kuanza kuchukuliwa. Aidha pia miongozo mingi kutolewa bila kufikishwa kwa wananchi  au walengwa na kuishia makabatini.
Imeandaliwa na:
Sylvester Raphael,
Afisa Habari  Mkoa,
KAGERA.
Next Post Previous Post
Bukobawadau