Bukobawadau

MKOA WA KAGERA WAPONGEZWA KWA KUENDELEA KUTUNZA MITI NA MAZINGIRA

Picha ya Nyoka.
Dr. Felician Kilahama Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki Wizara ya Mali asili na Utalii
Afisa Misitu na Mali Asili wa Mkoa wa Kagera Bw. Jaffary Omari Akifafanua Jambo Wakati wa Mkutano wa Majumuisho ya Ziara ya Dr. Kilahama Mkoani Kagera.


Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii Felician Kilahama ametembelea mkoa wa Kagera na kuitembelea misitu pia kukagua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa chini ya wizara hiyo.

Dr. Kilahama aliweza kupata fursa ya kutembelea shamba la miti la Lubale, Mapoli ya hifadhi ya Biharamulo  na Burigi, Misitu ya Murongo Ibanda na Rumanyika Wilayani Karagwe pia na Msitu wa Minziro Wilayani Missenye.
Mkurugenzi huyo wa Misitu na Nyuki katika majumuisho ya ziara yake aliusifu mkoa wa Kagera kwa kuweka juhudi za makusudi za kutunza misitu na mapoli. Pia aliwaomba maafisa misitu kuendelea kuweka juhudi zao kuendelea kutunza misitu pamoja na uchache wao.
Aidha Dr. Kilahama aliomba serikali kuendelea kuelimisha wananchi na serikali za vijiji na vitongoji juu ya umuhimu kuheshimu mipaka ya hifadhi zilizopo ili kulinda mali asili za nchi ambazo zitaliepusha taifa kupatwa na majanga  kama ukame ambavyo vimeanza kuwa tishio sehemu mbalimbali duniani.
Katika msitu wa Minziro Dr. Kilahama ameuomba uongozi wa mkoa kuharakisha taratibu za kuufanya msitu huo kuwa msitu wa asili ili uweze kutunzwa kwa karibu sana kwani msitu huo ni kivutio kikubwa cha asili ambacho kinaweza kuuingizia mkoa kipato kikubwa cha mapato na kuinua pato la mkoa.
Vivutio vya utalii vinavyopatikana katika msitu wa Minziro Wilayani Missenye ni pamoja na Nyoka ambaye ana umri wa miaka 209 mpaka sasa yuko hai, pia katika msitu huo kuna vipepeo vya aina mbalimbali wazuri wa kuvutia, kuna nyati wakubwa sana  aidha kuna nyoka mwenye pembe. Pia kuna ndege wanaoruka kutoka Ulaya na kuja katika msitu huo wa Minziro.
Akizungumzia faida za kuufanya msitu kutoka msitu wa hifadhi na kuwa msitu wa asili Dr. Kilahama alisema msitu ukishakuwa wa asili unatunzwa kwa karibu sana duniani kote pia unapata na ufadhili wa kutoka nje ya nchi na unakuwa kwenye rekodi za dunia ili kuhakikisha unadumu milele.
Wito, pamoja na kupongeza juhudi za wananchi wa mkoa wa Kagera kwa kupanda miti kwa wingi lakini Dr. Kilahama aliwasistiza sana Maafisa Misitu kuwafundisha wananchi jinsi ya kupanda miti kitaalam pia kuwaunganisha na kuanzisha chama chao ili walime miti kibiashara na kunufaika nayo kupitia chama hicho.
Mwisho  Dr. Kilahama alitoa wito kwa viongozi wote wa ngazi mbalimbali za serikali kushirikisha wananchi katika shughuli za uhifadhi wa misitu na mazingira ili wananchi wenyewe washirikishwe na kujua umuhimu wa misitu na kutunza mazingira.
Imetolewa na:
Sylvester Raphael
Afisa Habari Mkoa,
Kagera @2012
Next Post Previous Post
Bukobawadau