Bukobawadau

OKUHA: THE CULTURE OF GIVING AMONG THE HAYA OF NORTH - WESTERN TANZANIA

                   Na  Festo  Mukerebe

Mnamo miaka ya 1980, niliandika makala ya Kiingereza yenye somo hilo hapo juu. Hivi karibuni, wakati naandika makala kuhusu baadhi ya mila na desturi za Wahaya zinazohitaji mtazamo mpya katika zama tulizo nazo leo, nimeikumbuka sana makala ile ya Kiingereza. Lakini kutokana na kutokukumbuka wapi nilizihifadhi nakala za makala ile, nikabaki kutumaini kuiona siku moja ili niweze kuisoma tena na, hali ikiruhusu, niweze kuifanyia rejea (Revisit) na kuipanua kwa kuipa mtazamo wangu wa kipindi tulicho nacho sasa.
Hata hivyo, wakati nasubiri ‘kuivumbua’ upya makala hiyo, nimejisikia kuandika, japo kidogo tu, kuhusu utamaduni wa ‘upaji’ miongoni mwa Wahaya Mkoani Kagera.
Siwezi kudai kuifanyia utafiti wa kina sana dhana hiyo ya ‘upaji’ ambayo ndiyo okuha, miongoni mwa Wahaya. Lakini hilo haliwezi kuwa sababu toshelezi ya kunizuia kuijadili kwa kutumia uzoefu wangu wa miaka mingi kiasi kama mwanajamii husika.
Umuhimu wa okuha, hauhitaji kupigiwa kinubi wala baragumu. Upana wake, kama msamiati, unatosha kutuonyesha jinsi okuha kulivyokuwa ni tunu inayothaminiwa sana katika utamaduni wa Wahaya. Kwa hakika, okuha ni dhana ambayo haina mshindani katika ‘kamusi ya Kihaya’ kwa wingi wa maana zake mbalimbali, ambazo baadhi yake zinaendelea kusikika zikitumiwa hadi leo.
Pamoja na kutokuwa gwiji wa lugha ya Kihaya, mimi binafsi nimeweza kukusanya maana zisizopungua dazeni kuhusiana na maana hizo. Kwa kuzitaja tu, maana hizo ni pamoja na okutangilila, okutwela, okukulata, okulongola, okuganuza, okugabila, okugaba, okubegela, okushalila, okuzilima, okubisila, okuhonga, okutekela, okulozya, okubegana, okueleza, na hata okuhao. Inawezekana kuwa yapo maneno mengine ya Kihaya yenye msamiati mpana kama hilo la okuha, lakini ninaamini kwamba yatakuwa ni machache sana.
Mbali na vitenzi nilivyoweza kuviorodhesha hapo juu na kuvihusisha na ‘kutoa’ tunu fulani zipelekwe au kuhamishiwa kwa mtu, ukoo, tabaka au watu wengine, vipo vitenzi ambavyo, japo sio kwa ukaribu wa kiwango cha uwazi, vinaweza kunyumbuliwa na kujenga taswira isiyokuwa mbali na dhana ya upaji. Kwa mfano, okulela maana yake ni kulea. Ni wazi kwamba muktadha wa neno hilo unaonekana zaidi katika mwelekeo wa upaji, okuha.
Hii ni kwa sababu kulea au kuhudumia, ni kitendo kinachohusiana kwa karibu na kutjiolea muda,  raslimali na mapenzi kwa mtu mwingine aliye na hali ya kupungikiwa au kutindikiwa na amali fulani katika maisha yake. Mwisho wa siku, kusema kweli, kulea ni kumpa mtu kitu ambacho kukikosa kwake kitu hicho kungelimsababishia mlengwa unyonge na mapungufu kiafya au kumpotezea maisha kabisa.  Hebu tulithibitishe jambo hili kwa mifano michache zaidi.
·         Okukulata:

Enzi za jadi, wakati bado mfumo wa kitabaka wa ukabaila (feudalism) bado unatawala katika jamii ya Wahaya, raia wa hadhi ya chini, yaani abailu (watwana), walilazimika kuwasilisha kwa watawala wao, sehemu ya mavuno ya kilimo na mazao ya mifugo. Mila hiyo ya kujinyenyekeza au kujipendekeza, ilijulikana kama okukulata. Kwa maana hiyo, sehemu ya mali iliyopatikana kwa jasho la watwana ilihamishwa bila shurti dhahiri na kupelekwa kwa mtawala, kwa matarajio kwamba mtawala naye angaliweza kumtunukia (kumulongola, kumugabila au kumutunga) shamba au mifugo mtwana aliyewasilisha.
Japokuwa hali hiyo inaonyesha  dhana ya ‘unequal exchange’ au ‘labour exploitation’ ilivyofanya kazi kuneemesha tabaka la mabwana, bado tunaona jinsi pande mbili zilivyopeana raslimali na kubadilishana tunu nyinginezo chini ya mfumo wa utawala wa kitabaka uliokuwepo.
  
·         Okuzilima:
Okuzilima ni kitendo kilichohusisha sherehe ya kijamii, ambacho kwacho  familia ya wazazi wa bibi harusi ilikusanya kwa njia ya michango (okutweza) na kupeleka mali (kuzilima), hasa mikungu ya ndizi (ebitoke) na vibuyu vya pombe (amalwa), kwa familia ambako binti yao ameolewa (chini ya mwavuli wa kumzawadia binti yao). Ni wazi kwamba mila hii  ilikuza na kuimarisha mahusiano mema na maelewano ya upendo baina ya familia mbili zilizooleana.
Aidha, mila hii pia ilisaidia kujenga mshikamano katika jamii pana ya  kijiji au ukoo, kwani watu wote walialikwa na kupata fursa ya kushiriki mchakato wa sherehe kwa michango yao ya hali na mali. Kuchangia huko ndiko okutwela, wakati kuchangisha au kuhamasisha michango ni  okutweza.
Kwa mfano watu waliweza kuchangia mikungu ya ndizi(ebitoke n’enkundi) ili kukidhi mahitaji ya zawadi, na chakula na pombe kwa ajili ya washiriki. ‘Siku ya Siku’, watu wengine, hasa vijana, walialikwa na kushirikishwa katika misafara ya kubeba zawadi husika. Misafara hiyo ilipambwa na kukolezwa kwa  shamrashamra ya sherehe za ngoma na nyimbo (ebizina). Siku hizi, fedha zinatumika zaidi katika kufanikisha mchakato wa mila hii.

·         Okubega:
Okubega au okubegela ni mila iliyotekelezwa na Wahaya katika ngazi ya kaya, hususan wakati wanafamilia wanajipatia mlo wao. Vitendo vya okubega viliimarisha upendo katika kaya na kuwatia hamasa wanakaya walioonyesha nidhamu, uadilifu, utiifu na utendaji bora wa majukumu.
Japokuwa hapakuwepo na mipaka maalumu kuhusu nani ampe nani zawadi ya kitoweo (omukubi) kama ishara ya shukrani au pongezi kwa tabia nzuri, adabu na utendaji uliotukuka, ni watu wa rika andamizi zaidi ndani ya kaya (hasa bibi), walioidhibiti zaidi mila hii ya okubega.
Kwa kawaida, kitoweo  (samaki, nyama au maziwa) kiligawiwa katika utaratibu wa hatua kadhaa. Katika hatua ya awali, bibi (mgawaji wa mafungu ya kitoweo) alimgawia kila mwanakaya fungu lake stahiki, kulingana na rika au hadhi yake ndani ya kaya.  Kadiri mlo ulivyoendelea, alifanya mgawo mwingine mdogo. Kwa kawaida, mgawo  huu nao uliwahusisha karibu watu wote wa kaya waliojumuika pamoja kwa chakula.
Lakini kulikuwapo na hatua nyingine zaidi, iliyohusu ugawaji wa fungu maalum ambalo bibi alikuwa amelitenga kando kwa madhumuni ya kuligawa kama tuzo kwa kuzingatia vigezo na sifa maalum. Mara nyingi, utoaji wa mgao huu wa ziada uliandamana na maneno ya  kukaripia, kusifia, kuhimiza, kufundisha, kuonya, kuadabisha, kuhamasisha na kuelekeza.

·         Okulongola:
Okulongola, ni kitendo cha hiari alichokifanya mtu kwa kusudi la kumuonyesha mwenzake jinsi alivyoridhishwa na kitendo kingine ambacho yeye mwenyewe alipata kutendewa huko nyuma. Waingereza hukiita kitendo kama hicho reciprocity. Sisi hatuwezi kukosea kukiita Nipe - Nikupe. Ni kitendo cha kurudisha fadhila.
Mfano mzuri hapa, ni mila nyingine ya Kihaya, ambayo kwayo mwanamke hutoka na kwenda porini (wakati wa msimu wa musenene) na kukamata senene kwa ajili ya mumewe. Baada ya kuwaandaa wale senene na kuwawasilisha kwa mumewe kwa wakati muafaka, hutazamiwa mume naye aonyeshe kufurahi na kuridhishwa na juhudi za mkewe, kwa kumnunulia mkewe zawadi maalum, hususan doti ya kitenge au khanga. Akifanya hivyo, anakuwa ametekeleza mila ya okulongola. Mambo yalikuwa vivyo hivyo kwa maswahiba walioshibana.

·         Okutangilila
Katikanchi ya Wahaya’ (Buhaya), pengine hakuna mila ambayo imeenea na kuzingatiwa zaidi kuliko Okutangilila. Huwezi kuingia katika mji wa Muhaya ukatoka bila kutangililwa, yaani kulakiwa kwa kahawa au pombe, kama ishara ya ukarimu na upendo. Hata awe masikini kiasi gani, Muhaya atafanya juhudi kubwa kuhakikisha anaweka nyumbani kwake akiba ya kahawa (emwani) za kutafuna kwa ajili ya wageni wanaoweza kumfikia hata bila taarifa; haijalishi wageni hao wanatoka masafa ya mbali au karibu.
Kaya masikini iliyotembelewa na mgeni inaweza kutindikiwa na huduma nyingine yoyote, ikiwa ni pamoja na kitoweo, kiasi cha mgeni huyo kulazimika kula chakula ‘maluma’, jambo ambalo ni fedheha ya kutosha kwa mwenyeji, lakini kahawa ya mgeni kutafuna itapatikana tu, japo iwe nusu ya kibaba. Miaka hii, pombe, hasa gongo (enkonyagi), inatumika zaidi kukidhi haja, lakini mila inakuwa timilifu ikihusisha pia kahawa za kutafuna.

·         Okubisila
Okubisila ni mila ya kujiandaa kwa mapokezi ya wageni mashuhuri, hata wale ambao hawakutaarifu mapema kuhusu ujio wao. Maandalizi hayo yanahusiana moja kwa moja na kahawa za kutafuna pamoja na pombe, kama ilivyoelezwa hapo juu, chini ya kipengele cha okutangilila.
Lakini katika mazingira ya magonjwa haribifu ya migomba (kama ‘mnyauko’) na  kupungua sana miaka hii kwa zao kuu la ndizi kama chakula, Muhaya atabangaiza kuishi kwa kula mazao ya nafaka na mizizi (mihogo, viazi, magimbi, n.k- vyakula vya misimu (emyaka) visivyokuwa na hadhi kubwa kama ndizi, au vyakula vya kununua madukani (unga wa mahindi na mchele), ili mradi tu ahakikishe hakosi mikungu michache ya ndizi shambani mwake kwa ajili ya mgeni anayeweza kujitokeza wakati wowote.
‘Vyakula’ vinavyopatikana kwa msimu kama senene, huhifadhiwa maalum kwa ajili ya kukidhi mila hii. Na hakuna kitendo chochote cha heshima kubwa zaidi anachoweza kufanyiwa mgeni, kuliko kukarimiwa kwa senene. Labda tutoe mfano mmoja kuthibitisha thamani ya senene kwa Wahaya. Mwanamke ambaye mumewe amefungwa jela kwa miaka kadhaa, atafanya kosa linaloweza kuhatarisha ndoa yake asipochukuwa tahadhari ya kujiandaa kuwasilisha malimbikizo ya senene aliowahifadhi mnamo misimu iliyomkuta mumewe akiwa kifungoni!
Na kama tulivyoona awali, akifanya hivyo, atastahili ‘kulongolwa’ na huyo mumewe aliyerejea kutoka jela.

·         Okuhonga
Katika maana yake ya kiasili, Okuhonga katika jamii ya Wahaya, hakukuhusiana na kutoa rushwa, kufanya vitendo vya kifisadi au kununua mapenzi ya mwanamke. Enzi kabla ya ujio wa Wazungu walioleta na kutupandikizia imani na taratibu zao za kumuabudu, kumcha na kumtukuza Mungu, nasi Waafrika tulikuwa na taratibu zetu za kuwaenzi miungu yetu.
Okuhonga, kulikuwa ni utaratibu wa kuwatolea miungu sadaka na zawadi mbalimbali ili iwapendeze kututunuku baraka na kutujalia neema na rehema tele katika maisha yetu ya kila siku. Na katika jambo hili, Waafrika hatukutofautiana sana na Wazungu wa Ulaya, karne za kale (eila lya kalanda).
 Miungu ya Wahaya, ilikuwa ni pamoja na kasi (mungu wa ardhi na kilimo), ilungu (mungu wa nyika na wanyamapori), lyangombe (mungu wa mifugo, hasa ng’ombe), mugasha (mungu wa Ziwa Lweru- Victoria), nyakalembe, (mungu wa ustawi wa wanawake na mambo ya uzazi), n.k.
Katika Agano la Kale, tunasoma sana habari za dhabihu na matambiko ya kuchoma na kuteketeza kwa ajili ya Mungu? Wahenga wetu nao hawakuwa mbali katika kuwatambikia miungu yao ili iwajalie neema walizozihitaji ili kukidhi shida zao lukuki maishani mwao na kuondokana na maangamizi yaliyowazinga? Na ndiyo tunavyofanya hata sisi leo, chini ya madhehebu yetu mbalimbali - kwa kutoa zaka na sadaka kwa ajili ya kusifu na kushukuru ? Kimsingi, ni dhana ile ile?
Kwa kuhitimisha maelezo haya ya utoaji na upaji kwa ajili ya miungu, okuhonga, Wahaya hawakukosa kukiri imani yao katika uweza wa miungu hao.  Kila walipobanwa na matatizo na kuelekea kukosa suluhu ya kutokea, walisikika wakiungama na kujinyenyekeza: “ tubihongele mukama mungu”.   
                Maelezo ya mifano hiyo hapo juu, yatoshe kuonyesha jinsi utamaduni wa Kihaya ulivyosheheni  utajiri mkubwa katika nyanja ya ukarimu na upaji, okuha.
Next Post Previous Post
Bukobawadau