Cheti alichotumia Mulugo cha Mhadhiri wa Mkwawa
Dar es Salaam. Imebainika kuwa mmoja wa watu ambao Naibu Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo (pichani)anadaiwa kutumia
jina lake kutafuta kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari ya Southern
mkoani Mbeya ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu kishiriki cha elimu Mkwawa
(Muce), kilichopo mkoani Iringa.
Mhadhiri huyo ni Dick Aron Mulungu ambaye alisoma na Mulugo katika Shule ya Sekondari ya Songea Wavulana kati ya 1994 na 1996 na alijiunga na shule hiyo baada ya kuhitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kafule, ambayo iko mkoani Mbeya.
Taarifa zinaonyesha kuwa Mulungu alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupata Shahada ya kwanza katika Elimu (BA Education) 2001 na baadaye alisoma na kupata Shahada ya Uzamili (MA Development studies ) 2007.
Alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi, mahojiano yalikuwa hivi:
Mwandishi: Hallow…(mwandishi akajitambulisha)
Mulungu: Sawa, unasemaje?
Mwanishi: Nazungumza na Dick Mulungu?
Mulungu: Ndiyo mimi.
Mwandishi: Hivi unamfahamu mtu anayeitwa Hamimu Agustino?
Mulungu: Aah… hivi ulisema unaitwa nani?
Mwandishi: Si nimeshajitambulisha jina na ofisi ninayotoka?
Mulungu: Nipigie kesho naona hapa kuna kelele.
Mwandishi: Mbona nakusikia vizuri tu?
Mulungu: Nipigie baada ya nusu saa basi.
Baada ya nusu saa…….
Mwandishi: Haloo… naona nusu saa imekwisha, uko tayari kuzungumza?
Mulungu: Huyo simfahamu.
Mwandishi: Kwani wewe si ulisoma Songea Boys?
Mulungu: Ndiyo
Mwandishi: Kwa hiyo humkumbuki mtu aliyekuwa akitumia jina hilo?
Mulungu: Huyo mtu namkumbuka ndiyo.
Mwandishi: Kwa sasa yuko wapi?
Mulungu: Siwezi kujua, si unajua tumesoma siku nyingi sasa huwezi kujua mtu amekwenda wapi… ni siku nyingi mno.
Mwandishi: Ahsante.
Chuo Kikuu na siasa
Taarifa zinaonyesha kuwa Waziri Mulugo alijiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania 2002 akitumia majina ya Philipo Hamimu Augustino na alisomea Shahada ya Sanaa katika Elimu (BA. Ed). Namba yake ya usajili chuoni hapo ni 08652/T.02.
Alipokuwa akiendelea na kazi ya ualimu Mulugo alianza harakati za kisiasa na ndipo alipoamua kwenda kugombea ubunge katika majimbo ya wilaya ya Chunya.
Kada wa chama cha NCCR Mageuzi wilayani Chunya, Nyawili Kalenda aliyejitambulisha kama mlezi wa siasa wa Waziri huyo alisema walifahamiana naye 2004 wakati Mulugo na rafiki yake walipokwenda kumtaka ushauri wa kugombea ubunge katika jimbo la Songwe.
Katika nakala za wasifu wake zinaonyesha
kuwa 2008 alishika nafasi ndani ya CCM ambazo ni pamoja na mjumbe wa
baraza la jumuiya ya wazazi wilaya ya Chunya, Katibu wa Elimu, Uchumi,
Malezi na mazingira wa jumuiya ya wilaya hiyo na mjumbe wa baraza la
wazazi mkoa wa Mbeya.
Kauli yake
Mulugo anasema madai hayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na amekuwa akiyajibu kwa kuwaonyesha vyeti vyake halali vya shule. “Hayo madai ni ya muda mrefu, wewe sijui utakuwa mtu wa 20 kuuliza swali kama hilo. Mimi vyeti ninavyo na hata ukitaka ushahidi nitakuonyesha,” alisema Waziri Mulugo.
Kauli yake
Mulugo anasema madai hayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na amekuwa akiyajibu kwa kuwaonyesha vyeti vyake halali vya shule. “Hayo madai ni ya muda mrefu, wewe sijui utakuwa mtu wa 20 kuuliza swali kama hilo. Mimi vyeti ninavyo na hata ukitaka ushahidi nitakuonyesha,” alisema Waziri Mulugo.
Licha ya kukiri kurudia darasa la saba, Waziri Mulugo alisema jina la Hamimu amekuwa akilitumia katika elimu tangu awali na kwamba hakuvunja sheria kufanya hivyo.
“Jina la Hamim ni la nyumbani Philipo ni jina langu la ubatizo, nadhani haya ni mambo ya kawaida na kweli nilipokuwa shule watu walikuwa wananifahamu kama Hamimu pia Philipo ni jina langu la ubatizo na kumbuka tukifika chuo huwa tunatumia jina la baba.
“Na pia ni kweli nilirudia shule kwa sababu wakati ule wa Mwalimu Nyerere na Mwinyi (Ali Hassan), sheria ilikuwa inaruhusu maana wanafunzi walikuwa wachache mno, fikiria katika darasa letu la saba tulimaliza watu saba tu. Baadaye sheria hiyo ilibadilishwa,” aliongeza.
Kuhusu jina la Dick Mulungu, alikiri kumfahamu mtu huyo na kwamba walisoma wote shule ya Sekondari ya Songea Boys. Hata hivyo, alipinga kutumia vyeti vyake.
Source;Mwananchi.