Bukobawadau

CHIRITOWAJA MTINDA :BUNGE HALIJATIBUKA,NI WATU WACHACHE WALIOTIBUKA.

 Mh. Chiritowaja Mtinda(Mbunge)

Na Prudence Karugendo

KUFUATIA kutetereka kwa hali ya kisiasa nchini, nimekutana na kuongea na mbunge wa viti maalumu kwa tiketi ya Chadema, Mheshimiwa Christowaja Mtinda, na yafuatayo ndiyo maongezi yetu.

Swali: Mheshimiwa Mtinda, naelewa kwamba kitaaluma wewe ni mwalimu na baadaye ukawa mhadhiri. Ni kitu gani kimekufanya uiweke taaluma yako hiyo adhimu pembeni na kuamua kuingia kwenye siasa?

Jibu: Kwanza si kweli kwamba nimeiweka pembeni taaluma yangu, ila ndiyo ninayoitumia vilivyo bungeni kuweza kufikisha ujumbe kwa serikali nini kifanyike katika sekta ya elimu. Maana huwezi kulizungumzia vizuri jambo ambalo huna utaalamu nalo. Hiyo ndiyo sababu yangu kuu ya kuingia kwenye siasa.

Swali: Kama uendeshaji wote wa maisha ya mwanadamu unaanza na elimu, kwa maana ya kwamba watu wote, wakiwemo wanasiasa, wanahitaji kupata elimu ya kutosha ili iwawezeshe kukabiliana vya kutosha na changamoto za majukumu yao, je, wewe umeridhika kuwa upande huo wa elimu kuko salama na hivyo kuamua kwenda upande mwingine uliko kwa sasa?

Jibu: Nadhani jibu langu la kwanza limejibu swali hili la pili, kwamba sekta ya Elimu ni sekta iliyotelekezwa na haiko salama. Ndiyo maana nikajitosa kwenda kuisemea bungeni ambako nina uhakika, kwa kushirikiana na wabunge wengine, tuna nafasi kubwa sana ya kuweza kuirudisha sekta hiyo kwenye mstari.

Swali: Kwa nini umeamua kuingia kwenye siasa kupitia njia ya upinzani badala ya kupitia chama tawala ambako baadhi ya watu wanakuona ni njia ya mkato kupata mafanikio kisiasa?

Jibu: Kwanza nimepitia upinzani kwasababu sipendi njia za mkato katika kuyafikia malengo yangu. Pia kuwa kwangu kwenye upinzani kunanipa uwanja mkubwa sana wa kuweza kuisimamia na kuishauri serikali bila woga na bila kuwekewa mipaka. CCM iko madarakani na inatumia kila mbinu ili iendelee kubaki madarakani, kwasababu hizo hakuna mbunge wa CCM ambaye atakuwa na ujasiri wa kuipinga serikali yake waziwazi bila kukemewa na kuonywa. Mifano ni mingi hasa kwa wabunge wachache waliojitokeza kuwa majasiri lakini linapokuja suala la kuweka maamuzi kichama wanakwama hata kama maamuzi hayo yana athari mbaya kwa wananchi walio wengi. Kwahiyo kupitia upinzani kunanifanya niwakilishe matatizo ya wananchi, hususani masuala ya Elimu, bila kubanwa wala kupewa maelekezo.

Swali: Wewe binafsi unaiangaliaje siasa, ni mfumo wa kuwakomboa watu toka kwenye ufukara na shida walizonazo au ni njia ya wanasiasa kujikomboa wao wenyewe na kujipatia maisha bora huku wakiwatumia watu kama mtaji?

Jibu: Mfumo wa siasa kwa maana yake ukitumiwa sawasawa unaweza kabisa kuwakomboa wananchi toka kwenye ufukara na matatizo waliyonayo. Katika siasa kuna demokrasia ambapo wachache huchaguliwa kwa ridhaa ya wananchi walio wengi ili wawawakilishe katika nafasi mbalimbali za kisiasa ambapo watawawakilishia matatizo yao na kupatiwa ufumbuzi. Tatizo linakuja pale ambapo wanasiasa wachache wanaingia kwenye siasa wakiwa na malengo ya kujinufaisha wao wenyewe, na hawa mara nyingi hutumia umaskini wa wananchi kupata nafasi za kisiasa kwa kutumia pesa. Na wananchi kwa kuangalia shida ya leo na si ukombozi wa kudumu wanachagua pesa kuliko mtu na matokeo yake ni wanasiasa kuonekana wako pale kujinufaisha wao na si kutatua matatizo ya waliowatuma. Wananchi wana nafasi kubwa sana katika kuliondoa tatizo hili la wanasiasa wabinafsi kwa kutochagua pesa bali mwenye uwezo wa kuongoza. Hivyo siasa inaweza kabisa ikatumiwa kuwafanya wananchi kama mtaji endapo wao wenyewe watakubali kufanywa hivyo. Kumbuka ukipanda mchongoma utavuna mchongoma usitegemee kuvuna maembe.

Swali: Kama siasa inalenga kuwaondoa watu kwenye ufukara na kuwapatia maisha bora, ni kitu gani kinawafanya Watanzania wazidi kuwa mafukara mwaka hadi mwaka kwa zaidi ya miaka 50 tangu waanze kuendesha siasa wakiwa huru?

Jibu: Kama nilivyojibu hapo juu, tatizo si siasa bali ni aina ya viongozi tunaowachagua. Kama viongozi ni wabovu tusitegemee muujiza wa kutokomeza ufukara kwa wananchi kwa kuwategemea wachache waadilifu ambao nao hufanya kazi kwa vikwazo lukuki. Huwezi kuuondoa umaskini kwa kutegemea mfumo uleule, uongozi wa aina moja na fikra mgando, kwa chama kilekile chenye watu walewale tangu uhuru! Huu ni muujiza! Ikumbukwe pia kuwa kama viongozi hawajui ni kwanini wananchi wao ni maskini na mafukara watajuaje mbinu za kuuondoa ufukara huo? Ili daktari akutibu ni lazima ajue kwanza chanzo cha ugonjwa wako.

Swali: Sina shaka hata kidogo kwamba wanasiasa upande wa chama tawala, CCM, wanauchukulia upinzani wa kisiasa kama uadui wa kufa mtu. Unadhani kwa nini wanafanya hivyo, na wewe binafsi unauchukuliaje upinzani wa kisiasa?

Jibu: Jibu liko wazi, hakuna mtu anayekubali kunyang'anywa tonge mdomoni wakati ana njaa na amejiandaa kulimeza! Lakini hapa nikiri wazi kwamba wanasiasa wa chama tawala wanawaogopa wanasiasa wapinzani wa CHADEMA na si wengine, hii ni kwasababu wanaona wazi nafasi zao ziko hatarini kupokonywa. Na huu ndio ukweli ingawa kuna wachache wanaoona upinzani si uadui. Kwa upande wangu mimi nauona upinzani wa kisiasa si uadui wala ugomvi, bali kushindana kwa hoja za msingi na hatimaye kufikia malengo ya kuwaletea wananchi maendeleo. Kama ingekuwa ni uadui basi kusingekuwepo na demokrasia ya vyama vingi. Hivyo cha msingi ni kuheshimiana na kuvumiliana katika hoja tunazojenga ili hatimaye tufikie maamuzi ya busara.

Swali: Wewe ni mbunge wa viti maalumu, kama mama msomi wa kiwango ambacho hata baadhi ya wanaume wanashindwa kukifikia, unasemaje kuhusu viti maalumu? Kuna ulazima wowote wa viti hivyo kuendelea kuwepo?

Jibu: Uwakilishi wa wanawake bungeni ni wa muhimu kwa wakati huu kuliko wakati mwingine wowote hasa ukizingatia ni kipindi ambacho maadili yameporoka katika ngazi zote za maisha ya mwanadamu. Nadhani kinachosumbua hapa ni tafsiri ya jina lenyewe “Viti maalum” ambalo limekuwa likipewa kila aina ya dhihaka kwa mwanamke na wakati mwingine kuonekana hata wanawake wenyewe wa viti maalum nao hawafai na hawana lolote. Nashukuru kwa wewe kuona kwamba elimu niliyonayo hata wanaume wengine hawana, lakini ni mbunge wa viti maalum. Na niseme wako wengi tu bungeni wenye elimu nzuri sana lakini wanabezwa kwa vile tu wameingia bungeni kupitia viti maalum. Kwahiyo niseme tu kwamba kinachotakiwa kwa sasa ni kutafuta namna nyingine iliyo bora zaidi ya uwakilishi wa wanawake bungeni kama ambavyo wengi wametoa maoni yao kwenye mchakato wa kuandika katiba mpya. Wanawake wanaweza kutengewa maeneo yao wakashindana na kupigiwa kura na wananchi ili kuongeza uwakilishi wao bungeni. Jina la viti maalum liondolewe kabisa maana linatumiwa vibaya kuwadhalilisha wabunge wanawake wa vyama vyote bila kujali mchango wao mkubwa bungeni.

Swali: Kama akina mama wanaweza kugombea majimboni na wakashinda, tena kwa kishindo, mifano hai ipo mingi. Bibi Titi Mohamedi tangu enzi za uhuru wa Tanganyika mpaka kwa Halima Mdee wa sasa, huoni kuwa viti hivyo maalumu vinaidhalilisha jinsia ya kike kwa kuifanya ionekane ni jinsia isiyoweza wakati siyo kweli?

Jibu: Ni kweli kabisa, kwa jicho la nje inaonekana viti malum vinaidhalilisha jinsia ya kike hasa pale ambapo itaonekana utaratibu wa kupata nafasi hiyo haukufuatwa ipasavyo. Lakini kwa jicho la ndani mimi nakataa kabisa kwamba viti maalumu vinadhalilisha wanawake. Nina sababu za msingi, mosi ni kwamba kwa utamaduni wa Kiafrika ukijumlisha mila na desturi za makabila mengi, mwanamke hakupewa nafasi kabisa ya kusimama mbele ya wanaume na kuanza kushindana kwenye mambo hasa ya uongozi. Kazi yake kubwa ilikuwa ni kulea watoto na kutunza familia. Sasa kwasababu hizi za kihistoria mwanamke ameendelea kuwa mnyonge na kubezwa hata pale ambapo anaonyesha kabisa ana uwezo sawa au hata pengine zaidi ya mwanaume. Hii hali imepelekea wanawake wengi kukosa ujasiri wa kupambana na wanaume majukwaani hasa pale anapokashifiwa mbele za watu. Ikumbukwe pia kwamba wanawake si watu wa kutukana hovyo na kusema hovyo, maana hayo si maadili yao, hivyo wameathiriwa sana na mfumo dume ambao kwa makabila mengi ya Kiafrika bado umeshika hatamu. Kwahiyo kwa kutambua hivyo Katiba yetu iliamua kuweka kipengele cha viti maalumu ili tuweze kupata wanawake wengi katika chombo cha maamuzi ambapo watapata nafasi ya kusemea mambo yao na hasa kurekebisha sheria kandamizi kwa wanawake. Kama nilivyosema awali, kinachogomba hapa ni jina lenyewe kupewa tafsiri mbaya. Lakini kwa hali iliyopo wanawake wameonyesha ujasiri mkubwa na ni haki sasa kwenda kupambana majimboni.

Swali: Kwa sasa Bunge limetibuka, badala ya waheshimiwa wabunge kukaa na kufikiria namna wanavyoweza kuisimamia barabara serikali ili iweze kuendesha mambo kiuadilifu kwa manufaa ya wananchi, kila mbunge anajaribu kubuni mpasho mpya ili amkandamize nao mbunge mwingine, hasa waliye tofauti kiitikadi. Unasemaje kuhusu tabia hiyo chafu iliyozuka kwa nguvu bungeni?

Jibu: Bunge halijatibuka lipo palepale na kanuni zipo palepale. Kinachotokea ni kwa wabunge wachache sana, tena wanafahamika mpaka kwa majina, ambao nikiri wazi wanakuwa hawana ujasiri na uelewa wa kutosha wa kilichowaleta bungeni badala yake wanaamua kuleta lugha za mipasho na mashindano ya matusi bungeni. Mbunge yeyote makini ambaye anafahamu wajibu wake sawasawa na anajua kujenga hoja imara huwezi kumkuta anatukana ama anaongea mipasho kama vile yuko kwenye ukumbi wa taarabu za akina mzee Yusuph ambao ndio fani yao. Kwahiyo mimi nasema tabia hii chafu inatakiwa ikomeshwe haraka iwezekanavyo ili watoto wanaofuatilia bunge wasije kuchukua mipasho hiyo wakidhani ni halali maana imetoka katika chombo kitukufu. Na kwa hili, kwakweli kiti cha spika kinatakiwa kifanye kazi yake sawasawa bila kupendelea upande mmoja. Ukitaka kumuua nyani usimwangalie usoni.

Swali: Bahati nzuri wewe sio mbunge wa mipasho, sijakusikia hata mara moja ukitoa mipasho, hata kama unaandamwa na hiyo mipasho kutoka upande wa pili. Tatizo hilo la wawakilishi wa wananchi kuanzisha miziki ya taarabu bungeni badala ya kuyajadili matatizo ya wapiga kura wao unadhani litamalizwa na nini?

Jibu: Nashukuru kwa kutambua kwamba mimi si mbunge wa mipasho. Tatizo hili litamalizwa kwa namna moja tu, wabunge wote bila kujali vyama vyao wawe wanasimama kwenye hoja iliyopo mezani. Kujibu hoja sio lazima ujibu kwa kubeza mtoa hoja ila unaweza kuijibu kwa kujenga hoja nzito yenye ushahidi wa kutosha bila kutumia maneno ya kuudhi wala matusi. Na kwa wewe ambaye utajibiwa kwa matusi, ustaarabu ni kuachana na mtoa matusi, jenga hoja ili kumfanya ajione mjinga. Kwa kufanya hivi kamwe hatutasikia taarabu, mipasho au matusi bungeni. Tunatakiwa kushindana kwa hoja na si kwa malumbano ya maudhi.

Swali: Je, ipo haja ya kuanza kuziangalia CV za watu wanaoutamani ubunge? Inawezekana upeo mfupi kifikra kikawa ndicho kizingiti kikubwa ambacho baadhi ya wabunge wanashindwa kukivuka katika kujenga hoja zenye changamoto maridhawa na hivyo kuishia kwenye mipasho na wakati mwingine matusi ya nguoni?

Jibu: Kuna haja tena kubwa sana kwa hii karne ya Sayansi na Teknolojia kuanza kuziangalia CV za wabunge. Na si CV tu bali mtu awe anafuatiliwa tabia yake tangu utoto wake maana CV inaweza kutengenezwa ikaonekana ni nzuri kumbe ni karatasi tu na si uhalisia wa alicho nacho mtu. Unafahamu wenzetu hawakukosea waliposema kwa tafsiri isiyo sahihi “Akili ndogo hujadili mtu bali akili kubwa hujadili mada au maarifa”. Hivyo inawezekana kabisa upeo mfupi unakuwa kizingiti au ushabiki wa chama unamfanya hata yule mwenye CV nzuri aache kuzungumzia mada iliyopo badala yake aanze kutoa mipasho. Mifano ipo wananchi wanafahamu.

Swali: Katika Bunge la sasa wabunge wa upinzani ni karibu robo ya wabunge wote, lakini mchango wenu umekuwa mkubwa kuliko wa robo tatu ya wabunge waliobaki. Inabidi wakati mwingine Spika au Naibu Spika wabuni kanuni za papo kwa hapo, zilizo nje ya Kanuni za Bunge, katika kukabiliana na changamoto za wabunge wa upinzani walio robo ya wabunge wote. Je, una lipi la kuwaambia wananchi kuhusu hali hiyo?

Jibu: Ninaloweza kuwaambia wananchi ni kwamba kamwe wasikubali kukata tamaa kwa yanayotokea kwa sasa, maana ukombozi wao umekaribia. Wananchi wa Tanzania popote walipo watuunge mkono kwa kazi tunayoifanya maana sauti yetu ni sauti yao, hivyo popote walipo wasibweteke nao wawe walimu kwa wengine maana asali ni tamu lakini ili uipate ni lazima ukubali kuumwa na nyuki.

Swali: Je, una mpango wa kwenda jimboni kuomba ridhaa ya wapiga kura ili wakurudishe bungeni katika uchaguzi ujao? Na kama mpango huo upo, ni jimbo gani unalolitamani na unalo lipi la kuwaeleza wapiga kura ili waanze kujiandaa mapema kuzikwepa siasa za maji taka zilizozoeleka wakati wa kampeni?

Jibu: Nina mpango wa kwenda kugombea jimboni tena kwa nguvu mpya, ila kwasasa naomba jimbo nisiliseme maana hili lipo ndani ya chama changu kwa vile bila chama kunipa ridhaa kwa muda uliowekwa itakuwa si busara kwa mimi kuanza kusema sasa hivi. Muda muafaka utakapofika na chama kikinipa ridhaa mambo yote yatakuwa hadharani.

Swali: Sasa turudi kwenye taaluma yako. Kwa sasa elimu nchini imeangukia pua. Pamoja na kushusha kiwango cha alama za kufaulu bado wanafunzi wanafeli kwa kiwango cha kutisha! Imefikia hata wanafunzi wasiojua kusoma wala kuandika wanaburuzwa kwenda kidato cha kwanza! Wewe kama mwalimu na mhadhiri unafikiria ni nini kifanyike kuondoa aibu hii?

Jibu: Ni kweli kwamba kiwango cha elimu yetu kimeshuka na kinatia aibu. Pamoja na jitihada za serikali ya CCM kujivuna kwamba imeweza kuanzisha shule nyingi za kata na kuwezesha idadi kubwa ya watoto kwenda shule, bado sikubaliani na huu mkakati wa kuangalia wingi wa shule na watoto bila kwanza kuangalia ubora wa shule hizo. Hakuna asiyefahamu shule bora inatakiwa iweje. Shule za kata hazina walimu wa kutosha hasa wa Sayansi na Hesabu, hazina maabara, mabweni, maktaba, vyoo, madawati, vitabu nk. Waalimu wanaishi katika mazingira magumu, maslahi yao ni duni kupita kada zote za watumishi, na wanaidai serikali mabilioni ya stahiki zao. Hizi zote ni sababu tosha na nyingine nyingi zinazodumaza Elimu yetu. Cha kufanya hapa ni kujitazama upya kama Taifa wapi tumepotoka. Ni vizuri sasa kuangalia bajeti inayotengwa kwenye Elimu kama inakidhi mahitaji ya kuboresha elimu yetu kwa matatizo yote niliyoyataja. Ni wakati wa wanasiasa kuwa wakweli na kuacha kudanganya umma kwamba tuna shule nyingi wakati wanafunzi hawana watu wa kuwafundisha na hakuna vifaa vya kujifunzia. Ni wakati wa wanasiasa kusutwa na dhamira zao na kujiuliza ni kwanini sisi hatupeleki watoto wetu kwenye hizi shule za kata na badala yake tunawapeleka kwenye shule bora za kulipia au nje ya nchi, kama kweli hizi shule ni nzuri kama tunavyozisifia bungeni kila kukicha? Tuangalie pia Sera ya Elimu. Hii sera ya mwaka 1995 imeshapitwa na wakati na Wizara imekuwa ikisema italeta rasimu ya sera mpya ya Elimu ya mwaka 2012 lakini mpaka sasa bado iko kwenye mchakato usioisha. Bila sera bora ya elimu ni kwa vipi tutaboresha elimu yetu? Ifahamike kuwa sera ya elimu ndiyo inayotoa mitaala ya elimu, na mitaala ya elimu inatoa mihutasari ya masomo. Kama hili halifanyiki tusitegemee muujiza wa elimu yetu kuinuka. Jambo lingine la kuangaliwa hapa ni kanganyiko wa suala zima la Elimu kuwa TAMISEMI na wakati huo huo kuwa wizara ya Elimu.Hili ni tatizo kwa vile usimamizi na uwajibikaji unakuwa mgumu maana wizara hizi mbili zinategeana linapokuja suala la nani awajibike ikitokea hitilafu. Mfano, matokeo mabaya ya kidato cha 4 mwaka jana, wa kuwajibishwa ni TAMISEMI au Wizara ya Elimu?

Swali: Je, serikali inatakiwa ifanye nini kuhakikisha inairudisha hadhi ya uwalimu iliyopotea na kuwafanya watu wakwepe kujulikana kuwa ni walimu?

Jibu: Serikali iliharibu sana kuanzisha mafunzo ya muda mfupi ya Waalimu wa Cheti na Stashahada pindi mipango ya MMEM na MMES ilipoanza ili kukabiliana na upungufu mkubwa wa walimu. Walimu wa Cheti badalaya kufundishwa kwa miaka miwili kama ilivyokuwa mwanzo wao wakawa wanafundishwa kwa miezi 9 tena wale waliofeli na waliokaa nyumbani muda mrefu sana. Na katika kufundishwa huko walikuwa hawafundishwi “content” ya somo bali namna ya kulifundisha somo hilo (Teaching Methodology). Sasa mtu aliyefeli Jiografia badala ya kufundishwa tena aifahamu vizuri anakwenda kufundishwa namna ya kuifundisha, hapo unategemea nini? Asiyejua kumfundisha asiyejua unategemea uvune nini? Hali kadhalika na walimu ngazi ya stashahada nao wakawa wanafundishwa hivyohivyo badala ya miaka 2 wao wakafundishwa kwa wiki 6 tena nao ni wale waliofeli. Hiyo heshima ya mwalimu itatoka wapi? Huo mshahara mzuri watampangia vipi wakati watu mitaani wanawaita walimu wa yeboyebo au vodafasta? Hii imeharibu kabisha heshima ya mwalimu. Cha kufanya ni kurudisha utaratibu wa zamani wa kuwachukua wanafunzi waliofaulu kwa daraja la kwanza na pili ndio wapelekwe vyuo vya ualimu kusoma. Tuachane na hizo div. 4 za kuungaunga kuwapeleka ualimu. Na tuache kabisa siasa na mizaha kwenye suala zima la Ualimu.

Swali:Wakati fulani ulikuwa waziri kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, lakini baadaye ukawa husikiki tena kwenye wizara hiyo. Nini kilitokea na sasa uko wapi?

Jibu: Ni utatratibu wa Chama Changu kubadilishana nafasi za uongozi ili tutakaposhika dola 2015 kila mtu awe na uzoefu wa kuongoza sehemu mbalimbali. Hivyo ni utaratibu wa kawaida uliotumika wa kumuweka mtu mwingine kushika nafasi hiyo. Kwasasa mimi ni mbunge wa kawaida na ni mshauri wa mambo ya Elimu kwa yeyote anayehitaji ushauri wangu.

Swali: Mwisho, unavyoona wewe au kufahamu, ni kipi kinachopaswa kukifanya chama cha siasa kijivune kuwa kina mafanikio? Umri wa chama, ushindi wa kishindo, mahudhurio ya watu kwenye mikutano ya hadhara au utatuzi wa kero za wananchi?

Jibu: Nashukuru kwa kunijibia. Kwa ukweli hapo jibu ni utatuzi wa kero za wananchi ndicho kitu ambacho chama chochote cha siasa kinapaswa kujivunia. Ushindi wa kishindo wa kuwanunua watu na kuutumia umaskini wao kushinda si jambo la kujivunia hata kidogo. Kama kuna chama cha siasa kinajivunia ushindi wa kishindo bila kuondoa kero za wananchi chama hicho hakifai hata kutamkwa mbele za watu.

Mheshimiwa Christowaja Mtinda nakutakia kila la kheri katika harakati hizi za kisiasa.

Aksante sana!

prudencekarugendo@yahoo.com

0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau